26 January 2011

RPC akiri askari kushiriki ujambazi

Na Gory Mhiliwa, Arusha

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limethibitisha kuwa  askari wake wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mwenye namba G.6825 PC Elias Matiku ndiye
alihusika katika tukio la kumpiga risasi dereva teksi, Bw. Jamal Abdul (32) na baadaye kupora gari na fedha Januari 16, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Bw. Thobias Andengenye, alikiri askari huyo kutambuliwa na baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo na kuweka wazi kuwa anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

"Kuna waliokuwepo kwenye tukio kama kule kwenye kituo cha mafuta walichopora, walitaja baadhi ya vitu na umbo lake alivyokuwa siku ya tukio. Uchunguzi wetu wa awali unatuonyesha kweli siku hiyo nguo alizokuwa amevaa na umbo walilosema ni lake," alisema Kamanda Andengenye.
 
Alisema kwa sasa wanamshikilia, na kwamba dereva teksi atakapopona naye atapelekwa kituoni hapo kwa ajili ya utambuzi zaidi.

Alisema siku ya tukio Januari 16, mwaka huu saa 11.00 alfajiri eneo la Ngarenaro Dereva teksi huyo mwenye gari namba T. 976 AJZ Toyota Mark 11 akiwa eneo la Shivaz Kaloleni alitokea mtu mmoja aliyevaa koti kubwa jeusi, na viatu vyeusi na mkononi akiwa na silaha na kuomba  kupelekwa kituo cha Polisi ngarenaro.
 
Kamanda Andengenye alisema koti hilo lilikuwa la kuzuia baridi lakini silaha aliyokuwa ameshika haikujulikana ya aina gani, ingawa dereva huyo alisema ni SMG.

Alisema baada ya makubaliano ya kumlipa sh. 3,000 waliondoka na kwamba walipofika eneo la standi ya mabasi ya Kimotco mtu huyo alimpiga risasi mkono wa kulia na kisha kupora gari hilo.
 
Alisema baada ya tukio hilo mtu huyo aliondoka na gari hadi kituo cha mafuta kinachomilikiwa na Bw. Suleman Nkya na kumkuta muhudumu aliyejulikana kwa jina la Yasri Mohamedy au Shabani na kuagiza kuwekewa mafuta. 

"Wakati anawekewa mafuta ghafla akambadilikia na kupora fedha sh. 350,000 za sarafu na kukimbia na gari hilo ambapo wakati anakimbia aligongana na gari lenye namba T.412 BMH Toyota Hiace kituoni hapo kisha akatelekeza gari hilo kituoni hapo.

Alisema baada ya tukio hilo Polisi walipoanza kufanya mahojiano walibaini katika maelezo ya awali kuwa askari huyo amehusika.

Alisema kutokana na maelezo ya awali ya Dereva huyo ni kwamba siku ya tukio saa 10 za usiku katika eneo la Shivaz mtaa wa Kaloleni akiwa ameegesha gari lake alitokea mtu mmoja akiwa amevaa mavazi ya jeshi la Polisi na kumtaka ampeleke katika kituo cha polisi cha Ngarenaro baada ya makubaliano ya kulipwa sh. 3,000.
 
Alisema mara baada ya kufika karibu na kituo hicho askari huyo alimwamuru dareva huyo kusimama na alimtaka ampatie sh. 7,000 ili ampe noti ya sh. 10,000.
 
Alisema wakati dereva huyo aliyetambulika kwa jina la Jamal Abdul (32) akijaribu kutoa chenji ya sh.7,000 ili apewe sh. 10,000 askari huyo aliyekuwa ametoka nje ya gari ghafla aliikoki silaha yake na kumfyatulia risasi moja iliyompata sehemu ya shingo na kutokeza upande wa pili na kumjeruhi pia katika bega la kushoto.

Baada ya tukio hilo, askari huyo aliondoka na teksi hiyo na kwenda kwenye tukio la uporaji wa fedha kwenye kituo cha mafuta.

16 comments:

  1. Du,pole sana Kamanda Andengenye,wangekuwa wale ma RPC vikongwe wangejidai kutetea askari wake ,thanks for your transparency.I like your style.Keep it up Ande.

    ReplyDelete
  2. ASANTE RPC Andengenye, mimi na wana morogoro tufafahamu ueledi na utendaji kaziwako mzuri, na hii ni kutokana na Mungu uliye naye ndani mwako tunayemfahamu. mengine yanayokupita kimo wanakuchafua bure, yapo juu ya uwezo wako, wanakulazimisha urudi Misri; na kwa hakika utakula maziwa na asali ya mwitu, hawakupati. sema ile kweli nayo itakuweka huru.

    ReplyDelete
  3. Hongera sana Afande RPC Andengenye, Kazi ulioifanya ni nzuri sana.kasoro ya ni kutoa amri ya kuua wanachama wa Chadema.Inabidi hiyo dhambi ukaitubu haraka kabla hujaharibikiwa.

    ReplyDelete
  4. Nakupongeza sana kamanda Andengenye, kinachotakiwa kifanyike, huyo askari achukuliwa hatua kali na za haraka ili liwe fundisho kwa wengine.Ndani ya mwezi mmoja awe kesha ingia jela

    kijana wako - Morogoro

    ReplyDelete
  5. Sasa Andengenye kwa nini IGP Mwema anaukuingilia kwenye anga zako kidogo unaingia kingi?
    Kafute basi hiyo kesi unayowashtaki kina Slaa na wenzake. maana unajua kabisa vijana wako, na inawezekana huyu jambazi aliyeua alikuwepo kufanya fujo kwenye maandamano ya amani ya CHADEMA. Tuhakikishie kama huyu jamaa hakuwepo. na kama alikuwepo inawezekana aliua mmoja au kujeruhi waandamanaji.

    Unatakiwa uvisafishe vikosi vyako vyote ili tuamini kuwa unawajibika. La sivyo mimi sikupi pongezi wakati wapigania haki wameingia kaburini na wengine wanauguza vidonda, huku wengine wakistakiwa bila sababu.

    Kama huwezi achia ngazi, tutakuona unatufaa.

    ReplyDelete
  6. Hata hivyo police walijaribu sana kuficha kitendo hicho cha mwenzao hadi walipoona maji yanawafika puani. Kumbuka majeruhi alipelekwa kituo cha polisi lakini hawakumpa msaada wowote. Bila shaka walitaka afe ili ushahidi upotee, bila kujua mhalifu alishaonekana na watu wengine. Kushiriki kwa polisi katika uhalifu kunawafanya watu kuhisi kwamba polisi wamekuwa wakishiriki katika uhalifu na hata mauaji bila kugunduliwa.

    ReplyDelete
  7. Acheni kuchafua andengenye, ni kamanda mzuri anayejua kazi yake. Mnampa lawama zisizo zake

    Kwanini hamuoni kama waandamanaji wa CHADEMA ni wakorofi? Serikali imekataza maandamano wao hawasikii, hawajui kuwa Serikali imepewa mamlaka na Mungu? Acheni kuongea tu, tumieni busara

    ReplyDelete
  8. Nchi haiwezi kujigamba kwamba ina amani wakati watunza amani (polisi) wa nchi ndio majambazi wanaoua raia na kupora mali zao. Ukatili wa kinyama tuliouona ukifanywa na hao "vijana" wa IGP kule Arusha unaonyesha dhahiri aina ya "walinda usalama" tulio nao. Kula rushwa hakujatowatajirisha vya kutosha, sasa wameingilia mauaji ya kikatili na uporaji. Kiama!

    ReplyDelete
  9. Hiyo polisi jamii yenu ni polisi jambazi

    ReplyDelete
  10. Huyu askari alikuwa kazini au mstaafu?? Kama alikuwa kazini, basi Jeshi la polisi linatakiwa kuangalia kwa undani mishahara ya maaskari, na kuwafanyia uchunguzi wa kisaikolojia kupima imani na uaminifu wa maaskari

    ReplyDelete
  11. Serikali ya CCM haitoki kwa mungu ndio maana imejaa laana serikali inayotoka kwa mungu ni ile iliyochaguliwa na wananchi wengi na inayosapotiwa na viongoz wa dini mfano serikali ya kikwete 2005-2010 si hii ya 2010-2015 serikali inayotoka kwa mungu haiuwi raia wake katiba inasema polisi haina mamlaka ya kuamua maandamano yafanyike au la Mbona songea maandamano ya CHADEMA SONGEA YAMEFANYIKA KWA AMNI huko Arusha wanaona CHADEMA ikiingoza halmashauri mafisadi watagundulika uozo wao kwani wengi wamewekeza huko.

    ReplyDelete
  12. Mimi siyoni sababu za kumpongeza huyo RPC kwa kuwa hakuna matukio makubwa ya kutisha ya UJAMBAZI hapa nchini ambayo hayahusishi askari ama toka JW au Polisi. Kumtaja askari huyo ni baada ya kubanwa na raia wema tu vinginevyo asingesema.

    ReplyDelete
  13. HEHE HEE. MNASAHAU KUWA HUYO ASKARI ALIYEHUSIKA NI MMOJA KATI YA WALE WATU WA INTELIGINNGENSIA (duuh, mniwie radhi ngeli haipandi), ... oohh, yes nimekumbuka! Ni 'INTELIGENSIA'? AMA KWELI NIMETOKA JASHO KULITAFUTA HILO BOMBA. YOTE HII NI POLISI WANASISYEMU WASOMI KUJARIBU KUITAALAMUSHA KAZI YAO ILI WALALAHOI WAONE NI BOOOOOOONGE LA KAZI, NA BOOOONGE LA UTALAMU.

    SASA HII NI PRUUF TOSHA TU WA AINA YA WATU AMBAO SERIKALI YA SIIISYEEM IMEWAWEKA KATIKA VYOMBO VYA UTENDAJI. WASIMSINGIZIE MTU HAPO. HICHO KIKOSI CHAO CHA INTELIJENSIA KIMEJAA WATUMISHI WENYE MIENENDO KAMA HIYO. NDIO AMBAO SERIKALIYA SISYEMU IMEWAAMINI.

    ReplyDelete
  14. HUO SI UUNGWANA KOSA LA ASKARI MMOJA ALIYEKOSA MAADILI KUWA KOSA LA POLISI WOTE JARIBU KUTFAKARI VIZURI.TATIZO AJIRA ZA ASKARI POLISI ZIPITIWE UPYA.TABIA NJEMA IWE NI KIGEZO CHA KWANZA NA SI UREFU N.K.

    ReplyDelete
  15. KWANZA JIULIZE WEWE UNGEKUWA NI ANDENGENYE UNGEFANYA NINI DHIDI YA WALE WAHARIFU?AU HAWAJUI KWAMBA WALIFANYA KOSA?ULIZA MISRI KILICHO TOKEA.WANASIASA WASITUSEMEE WANAINCHI ZAIDI YA MILIONI 40.

    ReplyDelete
  16. Weee EDWARD. Kilichotokea IJIPTI ni kuwa baada ya kuona wamezidiwa, POLISI wakavua magwanda na kuingia mtaani kuanza KUPORA. Hiyo ilikuwa kwa sababu mbili mahsusi:

    1. Kulipa kisasi na kukomoa wananchi baada ya kuiharibu dili yao na serikali maana waliahidiwa pesa nzuri na serikali iwapo wangezima lile vuguvugu la ukombozi. Ilibidi wafidie mahela waliyoyakosa kwa kuiba na kupora. Polisi wa bongo hawana tofauti na hao (hata commisioned officers wanaomba bakhshishi hadharani), yaani hata wale 'walioona ndani ya darasa kunafananaje', kwani wengi wa mapolisi wetu ni WANAINTELIGENSIA, yaani mambumbumbu.

    2. Serikali iliyopoteza uhalali iliishiwa na mbinu za kuwatawanya waandamanaji. Kete/karata ya mwisho iliyobaki ilikuwa ni kuwaamuru akina bob Makunja (polisi) kufanya uporaji ili kuwafanya waandamanaji waache kuwa mitaani nakukimbilia nyumbani kwa kuhofia kuporwa mali zao na familia zao kudhurika. Unaona hapo hiyo serikali dhalimu haiangalii madhara ya matendo na maamuzi yao, wanachojali ni kujaribu kuwa madarakani tu. Kwa sisyemu yetu, kete/karata iliyobaki kwao ni kutumia uchochezi wa udini.

    Mwananchi na wewe EDWARD,FIKIRI kabla ya kufanya maamuzi, unless umejaliwa kuwa na ubongo wa panya au panzi au senene!

    ReplyDelete