19 January 2011

Mgawo umeme sasa balaa

*Wanafunzi wa vyuo vikuu waja juu wagoma
*TRA 'Long room' shughuli za siku zakwama


Na Tumaini Makene

KATIKA hali inayotishia tatizo la mgawo wa umeme nchini kuanza kuathiri sekta nyeti nchini, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) kilichopo Chang'ombe Dar es Salaam  jana waligoma kwa
saa kadhaa kuendelea na masomo wakilalamikia masuala kadhaa likiwemo tatizo la mgawo wa umeme chuoni hapo.

Hali hiyo imekuja siku moja baada ya wanafunzi wengine wa  Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE)mkoani Iringa nao kugoma, huku kati ya masuala waliyolalamikia mojawapo likiwa ni tatizo la umeme linalotokana na mgawo, usiojulikana mwisho wake, unaoendelea nchi nzima.

Wakati wanafunzi wakiathiriwa na matatizo ya mgawo wa umeme nchini unaoendelea bila mamlaka husika kueleza bayana ni lini utakoma, kitengo kingine nyeti cha serikali katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) maarufu kama 'Long room' juzi wafanyakazi na wateja waliokuwa wakiendelea na mchakato wa kukamilisha taratibu za kuchukua mizigo yao, walilazimika kukwama baada ya jenereta lililokuwa likitumika kutokana na mgawo wa umeme, kupata hitilafu.

Wakizungumzia sababu za mgomo wao wanafunzi wa DUCE ambao madai yao yanafanana na wenzao wa MUCE, yaani kucheleweshewa fedha za kujikimu, ukosefu wa umeme wa uhakika na tatizo la vitambulisho vya bima ya afya kwa ajili ya matibabu yao walisema kuwa hadi jana walikuwa hawajui watapata lini fedha za kujikimu.

Walieleza kuwa walipaswa kupata pesa hizo tangu wiki iliyopita, lakini wameshangazwa na ukimya wa mamlaka husika kushindwa kutoa fedha hizo wanazotegemea kwa matumizi na kugharamia maisha yao ya kila siku  chuoni hapo.

Wakitolea mfano wa usumbufu wa tatizo la umeme chuoni hapo, baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Majira, walisema kuwa moja ya jengo la mihadhara ya masomo ambalo limeanza kutumika hivi karibuni, limejengwa kwa vifaa vya kisasa, kiasi ambacho kama hakuna umeme wa uhakika, hawawezi kuendelea na masomo.

"Mbali ya suala hilo la fedha kuna tatizo la umeme...mambo mengi sasa hayaendi kwa sababu ya mgawo wa umeme unaotuathiri huku jenereta letu likiwa bovu tangu mwaka jana na hatujui litatengenezwa lini...lakini pia bajeti ya hilo jenereta inakwenda wapi, kama halifanyi kazi...?

"Hilo jengo unaloliona hapo, lina 'Lectrure rooms( jengo la mihadhara) halina muda mrefu tangu lianze kutumika...limejengwa kisasa sana, kiasi kwamba vitu vyake vingi vinatumia umeme.

"Kwa mfano huwezi kusoma mle bila kuwa na 'power point'(mashine ya kusaidia kukuza maandishi na vielelezo ubaoni) hiyo mara nyingi kwa sababu umeme unasumbua na hakuna jenereta, vipindi vingi vimekuwa vikishindikana kufanyika, hasa vile vyenye hadhara kubwa kama wanafunzi mia tano," alisema mmoja wa wanafunzi hao aliyetambulika kwa jina moja la Mayunga.

Mwanafunzi mwingine wa mwaka wa kwanza ambaye jina lake halikupatikana mara moja, alisema kuwa wanakabiliwa na tatizo la kutopata matibabu ipasavyo kwa sababu hawana vitambulisho vya bima ya afya, pamoja na kuwa walishavilipia sh. 50,000, kwa kila mmoja, mapema wakati wa kusajiliwa kuingia chuoni, lakini mpaka leo hawajavipata.

"Kulipia vitambulisho sh. 50,000 ilikuwa ni moja ya sharti muhimu wakati wa usajili, bila hivyo mtu asingeweza kupata usajili, lakini tunashangaa tangu wakati huo hatujapata vitambulisho, hivyo hatuwezi kupata matibabu.

"Kila tunapofuatilia hatupati majibu yanayoeleweka hapa chuoni...watu wanaohusika na bima hiyo tumejaribu kuwauliza wanasema kila mara kuwa hawajapata fedha hizo kutoka chuoni hivyo hawawezi kutoa vitambulisho bila fedha hizo," alisema mwanafunzi huyo wa kiume.

Majira jana lilishuhudia takribani wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza chuoni DUCE, wakiwa nje ya madarasa wakishinikiza wapatiwe fedha hizo za kujikimu, baada ya kuwa wameishi maisha ya kubahatisha na wasiwasi tangu Januari 15, siku ambayo walipaswa kupata fedha zao za awamu ya pili, kwa muhula wa kwanza wa masomo, mwaka 2010/2011.

Wakizungumza na Majira, wanafunzi hao walisema kuwa sababu kubwa iliyowafanya kuchukua uamuzi wa kugoma kuingia madarasani, ni kucheleweshewa fedha hizo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Jitihada za Naibu Makamu Mkuu wa DUCE anayeshughulikia Utawala, Mipango na Fedha, Profesa Bavo Nyichomba, kuwatuliza wanafunzi hao walioonekana kuwa na munkari wakilalamika wamekuwa wakiishi maisha ya dhiki, ikiwemo kula kwa shida, ziligonga mwamba mwanzoni, wakisema hawakubali kurubunika kwa ahadi ya 'kesho, kesho'.

Baada ya mvutano wa zaidi ya nusu saa, huku wanafunzi hao  wakisisitiza kuwa hawataweza kuingia madarasani na kusoma hadi hapo watakapopata fedha, hatimaye walikubaliana na kauli ya Prof. Nyichomba kuwa watapatiwa fedha hizo leo, Jumatano.

Akizungumza na waandishi wa habari baadae, Prof. Nyichomba alisema kuwa wanafunzi hao wanapaswa kuushukuru uongozi wa DUCE kwa jitihada uliofanya kushughulikia suala hilo la upatikanaji wa fedha zao za kujikimu.

"Unajua wanataka fedha zao ambazo walipaswa wapewe tangu tarehe 15, lakini wakawa hawajapata...sasa kutokana na utaratibu mgumu wa kibenki kama zingepitia katika akaunti zao moja kwa moja kutoka bodi ya mikopo, wangechelewa kuzipata...hivyo sisi kama walezi wa vijana tukajitolea kubeba mzigo huo.

"Tukazungumza na watu wa Bodi waziweke fedha hizo katika akaunti yetu ya chuo...tangu mapema tulijua tutawapatia Jumatano (yaani leo), lakini tuliwaambia Ijumaa, maana hawa vijana ukiwaambia kuwa itakuwa Jumatano halafu ikawa vinginevyo hawawezi kukuelewa...lakini tulijua kesho watapata fedha zao.

"Tayari tumeshazungumza na benki, maana nao wanahitaji muwapatie taarifa siku moja kabla ili wajiandae, tayari tumezungumza nao, ili tuchukue fedha na kesho (leo) vijana wapate," alisema Prof. Nyichomba.

Jitihada za Majira kutaka kupata majibu sahihi ya sababu zinazokwamisha wanafunzi wa elimu ya juu kupata fedha zao za kujikimu kwa muda muafaka, lakini wanapogoma zinapatikana, hazikuweza kuzaa matunda baada ya kufika Bodi ya Mikopo na kuelezwa kuwa wafanyakazi hao hawatoi huduma wakati wa mchana, kwani ni muda wa chakula.

Kwa tukio la jana, DUCE sasa kinakuwa chuo cha nne wanafunzi wake wakigoma takribani ndani ya mwezi mmoja, baada ya Chuo Kikuu Cha Dodoma, Chuo Kikuu Ardhi, kufanya hivyona kufuatiwa na MUCE juzi.

Pamoja na kuwepo madai mengine kama hayo ya matatizo ya umeme, bima za afya, ubovu wa miundombinu na huduma zingine za kijamii, uhaba wa wakufunzi na vifaa vya ufundishaji, upatikanaji wa fedha za mikopo, kwa ajili ya kulipia ada ya mafunzo chuoni, kujikimu, mafunzo kwa vitendo, limekuwa sugu, tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo, takribani miaka sita iliyopita.

5 comments:

  1. Vilio vya wengi ni umeme hakika inatupa wakati mgumu sana na inachangia gharama za maisha kupaa,tunasikia ahadi nyingi za matumaini na tuna uvumilivu sana watanzania,lakini inaonyesha kama kuna hujuma maana, tuliambiwa maji yamepungua,baada ya muda maji yamejaa lakini hakuna mabadiliko na ndio kwanza tatizo likazidi, baadae takaambiwa mitambo ya Kidatu,mtera,pangani na Songas imeharibika!! baada ya muda tukaambiwa imetengemaa mara mashine ya Somanga kumeleta hitililafu mara uzalishaji wa gesi umepunguwa hivi ukweli ni upi? Maana gesi tunayo nyingi sana na kuna kisima kipya hata kuanza kutumiwa bado na hicho kina gesi mara dufu ya hiki cha sasa!!ukienda kidatu unaweza kukuta mashine zaidi ya 3 haziwashi ukiuliuza hupati jibu!! inaonyesha kuna hujuma/miradi ya wakubwa wenye malengo yao,athari zake vitu majumbani,madukani,ktk bucha nk, vinaharibika ktk majokofu, wasomi hawawezi kujisomea na kufanya mambo muhimu bila umeme ,kazi zinalala maofisini urasimu ndio unazidi,ajira zinapotea, mahitaji mengi yamepaa kwa ajili ya kufidia gharama kwa wenye majenereta,yaani umeme ni nusu ya maisha, hivi kweli huu mgao ni wa dharura au wa kupikwa?nina wasiwasi hata huo mradi wa mchuchuma utasusua hivyohivyo na utafikia hata 2015 haujaanza,tujianagalie tulikuwa wapi tuko wapi na tunaelekea wapi,sasa milioni moja ni kama lakimoja!! Inatisha na inakatisha tamaa

    ReplyDelete
  2. Leo napenda kuzungumzia tatizo moja tu la Long Room hapo TRA kwani tatizo la Matatizo ya yanayoikabili Elimu ya Juu tayari nilishayafanyia utafiti na nakala za utafiti huo tayari nilishawakabidhi mamlaka husika, moja ni kupanua wigo wa kifedha kwa Bodi ya Mikopo na pia kufunguwa matawi ya kikanda kwa bodi hiyo nchi nzima. Mapendekezo hayo kwa kiasi kikubwa naona yanafanyiwa kazi kwani Projection nilizozifanya inaonesha hadi kufukia mwaka 2015 tutakuwa tuna wanafunzi wenye sifa ya kujiunga na vyuo vikuu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 185,000 nchi nzima.

    Tafiti hiyo ina kichwa cha habari "The Problem Facing Higher Education In Tanzania 2006" Inapatikana CDTI Tengeru Arusha na Bodi ya Mikopo HESLB.

    Leo napenda nizungumzie tatizo la "Long Room" Long Room ni sehemu muhimu ambapo Serikali inajivunia kwa ukusanyaji woote wa kodi nchini. Fedha yoote tunayosikia itakusanywa kwa njia ya kodi asilimia kubwa inakusanywa kutoka eneo hilo, lakini tatizo lililopo ni u slow wa kutoa mizigo, mara utasikia systerm imegoma, tumegombana na TICS, hapo meli imeshaingia na mtoa mizigo mara kadhaa yupo kwenye hatari ya kuingia kwenye storage charges hata kama yeye si muhusika wa kadhia ya TRA na Washirika wake.

    Tatizo la Generator kutokufanya kazi kwa ufanisi hasa katika mgao huu wa umeme halijaanza jana, kila mara utasikia generator limegoma, system haijarudi kana kwamba TRA haina Competent System Administrators. Sasa wanaoumia ni wadau wa mwisho wa utoaji mizigo ambao ni sisi wananchi wa kawaida. Maana kwa mzigo ukikaa siku moja tu bandarini kwa kuzidisha siku zilizopangiwa tunalipa US$ nyingi sana, hili Serikali tunaomba mliangalie upya kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa sisi walipa kodi!!

    Matatizo ya nchi hii ni mengi basi tusimamie eneo hili japo lituokowe. tunapoteza mataifa mengi sana kufanya kazi na sisi kutokana na ubovu wa huduma za kupakuwa mizigo na kulipia kodi ulio na urasimu!

    Serikali hebu ingilieni kati suala hili! Ongezeni standby generators hata kama manne pale TRA au iwepo huduma ya moja kwa moja ya Umeme kuwa hakuna kuzima Umeme kama ilivyo mahospitalini na Sehemu nyeti!

    Pia muwapeleke upgrades course hao IT experts wa TRA kwani haipendezi kila mara kusikia System ipo down au internet imekata nk ili hali wao wapo kwa ajili ya kuporesha huduma ya IT kwa mlipa kodi hapo TRA.

    Kama wateja hawagomi hapo TRA basi tusiwalazimishe wajipange kugoma ili kuboresha huduma hapo TRA na Bandarini. Tufanyie kazi haya maoni na mengine yaliyotolewa na wadau wengine wa TRA na Bandari!

    Carwin

    ReplyDelete
  3. CARWIN ni mchochezi

    ReplyDelete
  4. HAMNA SABABU YA KUKOSA UMEME TRA MAJENERETA YAPO ILA NI MIPANGO YA ULAJI TU, MTAISHIA KUPIGA KELELE ZA MAFISADI KUMBE NYIE WENYEWE NDIO MAFISADI. HIYO NI DEAL TU. HAMNA SABABBU YA KUKOSEKANA UMEME

    ReplyDelete
  5. Huyo aliyejenga hoja ya kusema kuwa CARWIN ni mchochezi huna hoja! Pinga hoja kwa kufikiri usiwe mvivu wa kufikiri! Tunahitaji kuboresha Taifa letu kwa kukusanya kodi na kupanua wigo wa kodi ndiyo tufike.

    Kama limekugusa jipange kurekebisha uozo uliopo TRA na Bandarini lakini tunahitaji maoni yenye staha kama ya CARWIN kutusogeza mbele!

    ReplyDelete