20 January 2011

Gerrard ataka Dalglish aendelee kuinoa Liverpool

LONDON, Uingereza

STEVEN Gerrard anamuunga mkono kocha mpya wa muda wa timu hiyo, Kenny Dalglish kupata mkataba wa kudumu wa muda mrefu baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi sita katika msimu huu.Kocha huyo
amechukua mikoba ya kuinoa timu ya Anfield baada ya kumtimua, Roy Hodgson kutokana na matokeo mabaya.

Lakini nahodha wa timu hiyo, Gerrard anataka kuona King Kenny anakuwa kocha kamili kwa mara ya pili kwa Liverpool.

Alisema anatamani wamalize msimu wakiwa na matokeo mazuri, ili aweze kupata mkataba wa muda mrefu na kuongeza kuwa yuko tayari kujituma kwa ajili ya matokeo mazuri ya kocha huyo.

"Mimi siwezi kuongopa, wakati Kenny aliposema alikuwa anakuja nyuma, ilikuwa ni kuinua ari kubwa. Ninampenda binafsi na nimefurahia siku chache za kufanya kazi naye pamoja.

Alisema siku chache tangu kuanza kwake kazi, ameona tayari timu imeanza kuwa na mwelekeo mzuri kwa wachezaji kuwa na ari uwanjani.

Licha ya matokeo ya kufungwa mechi mbili na sare moja tangu
Dalglish kuanza kazi, timu imeboreka kiuchezaji na Gerrard anaamini kocha huyo aliwahi kuichezea timu hiyo anaweza kuendelea kuinoa baada ya msimu huu kuisha.

Gerrard alisema kocha huyo ana uwezo wa kuwaunganisha wachezaji na ni wakati wao kuungana naye kwa ajili ya kuleta matokeo mazuri. Alisema matokeo mabaya ni kitu ambacho kila mmoja kwenye klabu hiyo kinamsikitisha, lakini kunapokuwa na matokeo mabaya si vyema kumlaumu mtu mmoja.

Kutokana na ufundishaji wake, wachezaji wamekuwa wakijituma katika mazoezi kutokana na kuwa na mahusiano mazuri na wachezaji.Wakati huohuo, Liverpool imetangaza kumuuza winga wake Ryan Babel na timu ya Ujerumani, Hoffenheim itamchukua.

Hatua hiyo imekuja wiki moja tangu Dalglish, kuanza kukisuka kikosi chake na inadaiwa kuwa atauzwa kwa pauni milioni saba.Mchezaji huyo anakubaliana kuhusu maslahi yake na miamba hao wa Ujerumani.

No comments:

Post a Comment