31 January 2011

Mama Maria: Kuilipa Dowans tatizo kubwa

* Ataka CCM, wanachama watafakari kabla ya kulipa

Na Daud Magesa, Butiama
                                   
MJANE wa Hayati Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere ameibuka na kusema kulipa mabilioni ya fedha kwa kampuni ya
Dowans ni sawa na kuwaingiza wananchi kwenye matatizo makubwa.

Mama Nyerere  amekitaka Chama Cha Mapinduzi  (CCM) na wanachama wake wakae watafakari kwanza kabla ya kulipa fedha hizo, zinazokadiriwa kufikia sh. bilioni 94, kwa kuwa suala hilo litafanya CCM ama isiaminike, au wananchi waichukie.

Aliitaka serikali kuwawajibisha wote wanaohusika na Dowans ili kurejesha maadili ya uongozi kama ilivyokuwa wakati wa mwalimu, badala ya kukurupuka  kulipa sh. bilioni 94 bila kuangalia athari watakazopata wananchi.

Mama Maria Nyerere alitoa kauli hiyo nyumbani kwake Mwitongo, Butiama, juzi, wakati akizungumza na Kamanda wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Mbeya, Bw. Mwakajumilo Isaac ambaye pia ni Mhasibu Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mbeya, waliomtembelea baada ya kuanguka hivi karibuni na kuumia wakati akielekea kanisani.

Alisema  kwamba jahazi hili (Tanzania) linaelekea kuzama  kutokana na vurugu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, na hivyo  kuwataka Watanzania watambue kuwa, 'sote tutaangamia kutokana na athari za machafuko hayo'.

Alisema kuwa baadhi ya viongozi na Watanzania wamepoteza maadili na hivyo kutoa kauli zinazoweza kuiingiza nchi  kwenye machafuko kwa maslahi ysao binafsi, na kwa manufaa yao kisiasa.

Baadhi ya kauli hizo, alisema ni zinazohusiana na mifarakano ya kidini, na nyingine kuhusu na suala la dowans , ambayo alikuwa anaifuatulia kwenye televisheni.

Kuhusu mabadiliko ya katiba, Mama Nyerere alisema amekuwa akifuatilia mijadala mbalimbali kwenye runinga na kuona ulivyopamba moto, na hata kijijini kwake, Mwitongo, nako mjadala unaendelea.

Alisema kwamba Watanzania waendelee kuwa watulivu na mijadala hiyo iendeshwe kwa kushirikisha wadau na viongozi kutoka makundi yote kwa haki na usawa, huku wakizingatia umoja, amani na utulivu wa taifa ili kuenzi mazuri yaliyoachwa na waasisi wa taifa hili kwa manufaa ya wote.

Mjane huyo wa Baba wa Taifa alieleza kuwa  viongozi mbalimbali, wananchi na wadau wote wawe watulivu huku wakiliombea taifa wakati mchakato wa katiba mpya ukisubiriwa
kuanza.

Akigeukia sera ya Kilimo Kwanza, aliwaeleza makada hao wa UV-CCM kwamba watu hawapendi tena kilimo, hasa vijana wenye nguvu ,wamekuwa wakikimbilia mijini kufanya biashara na kusababisha maeneo mengi ya vijijini kukabiliwa na tishio la njaa huku mabepari nao wakipigania kuondoa historia nzuri ya taifa.

“Vijana wangu, hakuna mtu ambaye angependa kuwa maskini, lakini pia huwezi kuwa tajiri kwa njia za mkato, hasa kwa hawa watumishi wa umma, jambo kubwa ni viongozi kuzingatia na kufuata maadili kama ilivyokuwa kwenye uongozi wa serikali ya awamu ya kwanza ya  hayati Mwl Julius Nyerere kwa kuthubutu kuwaondoa wasiofaa na kuwataja hadharani,” alisema na kuongeza:

“Serikali inapaswa  iwaondoe wanaoiharibia, hata kama wanafahamiana. Pia ikihakikisha kauli za watu na wanasiasa zisizofaa kwa Watanzania, zenye lengo la kuhatarisha amani hazipewi nafasi na hatua kali zichukuliwe kwa wale wanaotoa kauli za uchochezi ili kuliangamiza jahazi la taifa letu lenye historia ya pekee na mfano kwa mataifa mengine”.

Alitoa wito kwa viongozi wa serikali kuhakikisha misingi yote ya taifa iliyoasisiwa  na viongozi waliotanguliwa wanaendelea kuilinda wakiweka  mazingira mazuri kwa kuboresha huduma mbalimbali za kijamii hususani vijijini ambako utoaji wa  huduma hauridhishi na hauna tija.

Alisema uduni wa huduma hizo husababisha jamii kulalamikika kutokana na wananchi wengi wa kipato cha chini kukosa huduma za afya, maji, elimu, barabara, bei nzuri  ya mazao na upatikanaji rahisi wa nishati ya umeme.

Aliwaasa  Watanzania kuacha kukubali kutumiwa na watu ambao malengo yao ni kujinufaisha kisiasa na kupata umaarufu ,huku wakiliacha taifa likiangamia kutokana na kutaka kuwagawa kwamkuzungumzia ukabila, udini na rangi vitu ambavyo wakati nchi ikipata uhuru Mwl. Nyerere na waasisi wengine walivipinga kwa nguvu zote, na hadi leo tu wamoja.

12 comments:

  1. Seriakli zote zinazoingia matatani au vurugu au vita na mapigano yasioisha ni Serikali isyo sikivu na haiko makini ktk utendaji wake. Na sasa Serikali yetu haiko makini,haisikizi vilio vyetu, ubinafsi umewajaa miyoni mwao, kibri,jeuri na kila mmoja anakuwa anasema vyake wengine wana busara lakini wengine utumbo mtupu.Lakini kila jambo lina kiongozi wake hapa Raisi wetu JK amaezidi kuwa kimya watu wanataka kumsikiza kauli zake za kukemea, na kutoa maamuzi yanayohitaji matendo yasiyo na vikao lakini inaonyesha anaachia watu wazidi kulumbana wanatukakanana na mwisho akija tamka itakuwa (too late)majuto mjukuu, chelewachelewa utamkuta mtoto si wako,hivi leo
    Raisi kakubali Katiba mpya lakini mpk leo hajatangaza hiyo kamati,bei ya umeme inapigiwa kelele kakaa kimya wakati gesi ni yetu, mafuta yamepaa ilikuwa sababu dunia nzima hali ngumu lakini leo hali iko swafi bei imeganda huko huko juu kakaa kimya,malipo ya dowans ni yeye wakutamka nini uamuzi wake kakaa kimya,Mikopo ya vyuo wanaohusika wanaboronga kakaa kimya, au anajiona anamaliza muda wake?Anataka iweje au mambo yake anaona yanamwendea sawa? Nchi inazidi kumegeka maadili haina heshima inapotea,aangali nyakati zinavyobadilika aache ukimya, awawajibishe wanaozembea arejeshe maadili mema na akemee yote maovu na kutoa amri za utekelezaji, anatakiwa aseme au atoe kauli 1> Malipo dowans yasilipwe
    2>Umeme ushuke bei 3>Kamati ateue ya katiba
    4> Avunje bodi ya mikopo vyuo vikuu na aamrishe mara mnoja wapewe mikopo
    5>bei ya mafuta ishuke hali ni ngumu,aanagalie Misri,Tunisia nk

    ReplyDelete
  2. Kiburi cha CCM na serikali yake kimewafanya wawe na dharau na kufanya mambo kimabavu bila aibu na bila kujali matokeo yake. Chama kimekumbatia ubinafsi, ufisadi, rushwa, uongozi mbovu na ukiukaji wa haki. Matendo yake yamesababisha nchi kudidimia kwenye umaskini na kuporomoka kwa huduma za jamii - hasa afya na elimu. Fedha ambazo zingeboresha huduma za avya na elimu zimeishia kwenye mifuko ya vigogo wa serikali na CCM ambao wanawadharau wananchi wa kawaida na kuwacheka wanapohoji uhalali wa malipo ya Dowans. Sasa wameanza kuwa na kigugumizi: mara lazima zilipwe, mara zisilipwe. Hii ndiyo aina ya mijitu inauyotawala nchi. Angefufuka Mwalimu leo yangekimbilia baharini.

    ReplyDelete
  3. Hapa lazima kuna tatizo ambalo limemkaba rais wetu. Kwa nini hana ujasiri kukemea uonevu huu wanaotendewa wananchi. Kwa nini anakaa kimya?
    Wasaidizi wake na CCM mbona hammsaidii. Au mnataka ashindwe kabisa, ili iweje?

    ReplyDelete
  4. Safi sana mama Maria Nyerere. Nashangaa watu wanapoteza muda wakati mmiliki wa dowans anajulikana ni Rostam Aziz. Soma hapa ukitaka kujua jinsi yeye alivyo mmiliki wa Dowans:

    http://www.theeastafrican.co.ke/news/Ruling%20party%20MP%20wins%20big%20in%20Dowans%20settlement/-/2558/1097932/-/a7t6a3/-/

    ReplyDelete
  5. hiyo website unayoitaja inaaminika maana watanzania sasa hivi wanapenda umbeya,sina maana ya kufurahia Dowans kwa sababu suala hili wameliingilia mawakili waadilifu basi ukweli utafahamika. website inatengenezwa na watu kwa malipo na inaweza ikaandikwa chochote tu. Mama Maria nakuunga mkono watu wote wabaya mafisadi na wanaochochea vurugu kama za Arusha wasionewe haya,waliohusika na kadhia ya Richmond hatimaye Dowans wasionewe haya,viongozi wabovu wasiojali wananchi pia waondolewe,serikali ni dhaifu,wezi wa mali ya uma wanapelekwa mahakamani wanacheka hata hofu hawana,mahakimu,majaji,polisi,mawakili wamekuwa watoaji roho za masikini,CCM yenyewe imekuwa si chama cha wanyonge tena na hata hao wengine wa vyama vya upinzani ni wanafiki tu waliokwisha wasoma wajinga wa kitanzania na kuwarubuni eti wanaweza kuwatatulia matatizo yao kwa mkupuo,hakuna raha bila kujituma,niliwahi kuandika hapa kuwa wanakimbia vijijini na kuwaacha mama zao na dada zao wakitaabika na huku mjini ndiko wanatumiwa kuandamana na kufanya fujo wakasema nawatukana.uongozi kila sehemu nchi hii umeoza kuanzia kwenye siasa mpaka kusiko na siasa,

    ReplyDelete
  6. kwanza nakupa pole mama maria nyerere kwa maumivu makali yaliyokupata. naamini utapona. maadili(ethics) aliyoacha mwalimu JK nyerere huwezi ukayapata sasa hivi ukizingatia nchi imekumbwa na wimbi la mafisadi kukumbatiwa na chama. inakuwa vigumu sana kuwanyooshea vidole mafisadi hasa ikizingatiwa kuwa wao wamechangia kuingiza madrakani CCM kwa asilimia zaidi ya 80%. kinachotakiwa ni utashi kwa watanznia kujiuliza kwa dhat je CCM IENDELEE KUTAWALA? wewe muangalie katibu mkuu wa CCM wanatakiwa wamuonee huruma sana kwani uwezo wake wa kutathimini na kutolea maelezo umefikia mwisho akiongea utadhani comedian au mganga wa kienyeji Kikwete anatakiwa alione amwoondoa haraka makamba vinginevyo anakidharirisha chama.
    suala la dowans lilipokelewa kwa shangwe kuanzia kamati ya mwakyembe ilipowasilisha ripoti yake na watanzania tulifurahi tukijua rais amerahisishiwa kazi na hakukuwa na sababu ya kuendelea na malumbano na watu matapeli. mimi sina interest ya kuwajua dowans kwani ni kampuni halali ninachotaka kwa namna yoyote ile serikali iepuke kuwalipa kwa kufuata mtiririko wa watu wenye akili. jamani tepushe balaa hili mkiwalipa dowans ninahakika yanayotokea misri na hapa yanakuja. together we stand.

    ReplyDelete
  7. haya ndiyo majibu niliyofatilia kwenye wesite iliyotajwa hapo juu,tujaribu kuwa wakweli tupate solution ya kweli,tena nimecopy ulichoandika nikapaste

    Your search -
    http://www.theeastafrican.co.ke/news/Ruling%20party%20MP%20wins%20big%20in ... - did not match any documents.

    Suggestions:

    •Make sure all words are spelled correctly.
    •Try different keywords.
    •Try more general keywords.
    •Try fewer keywords.

    Majungu hayafai kwani kila mtu tayari anajua uovu wa viongozi kwa kampuni hii ya Dowans lakini tuwe awkweli tutatue tatizo

    ReplyDelete
  8. Kwa mtu mwenye akili timamu, anayobusara ya kuweza kuangalia mambo yanayoendelea katika taifa letu na kutoa mwelekeo halisi wa taifa kwa siku za usoni. Nachoweza kusema wazee wetu Mama Maria Nyerere na Mzee Cleopa Msuya wameonyesha hisia zao, baada ya kuhojiwa na waandishi wa habari. Katika maelezo yao wote wameonyesha hali ya mwalekeo mbovu wa taifa letu. Hili limejitokeza kwa serikali kuendelea kukumbatia viongozi na watendaji wakuu wasio na uzalendo hata kidogo kwa taifa. Viongozi ambao wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao kuliko ya taifa. Kwa miaka hii tumeshuudia nchi ikiingizwa kwenye mikataba mibovu, ambayo imekuwa ikiigharimu serikali mabilioni ya pesa na kumkandamiza mtanzania mmaskini.
    Tukumbuke kwamba raslimali za nchi hii ni za watanzania wote, kuendelea kutumia raslimali hizo kuwanufaisha mafisadi kutaongeza mvutano wa kitabaka kati ya viongozi matajiri na wananchi wao maskini. Kama onyo hatua za haraka zichukuliwe koundoa na kupunguza pengo la watu maskini na watu matajiri ambao ni wachache (Viongozi)
    Nimesema viongozi kwa kuwa katika nchi hii viongozi wa serikali ndio wanaothaminiwa zaidi kimaslahi na serikali yetu kuliko hata wataaalamu. Sasa imefika kipindi mtu anaamua kuacha taaluma (utaaalamu)wake na kuingia kwenye siasa, kufuta maslahi bora. Katika chaguzi mbili zilizopita tumshuhudia wimbi la waadhiri wakimiminika katika siasa na kuacha kazi zao vyuoni.Watanzania uzalendo wa Baba wa taifa mmeupeleka wapi?

    ReplyDelete
  9. Watasema nini juu ya Rostam Azizi ambae ni mfadhili wao mkubwa. Kina William Ngeleja walipewa mamilioni ya kampeni zao na ni huyo huyo Rostam ambae amekuwa anawa black mail viongozi wengi ndio maana wanashabikia Dowans ilipwe. Hii ni pay back time. Raisi atasema nini wakati yeye na Makamba wanamuogopa huyo Azizi zaidi ya wanavyomuogopa Mungu wao.

    ReplyDelete
  10. Sisyemu ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Naafiki hilo. Ukifanya kazi unakamuliwa na sisyemu. Ukilima unakamuliwa pia. Wakulima na wafanyakazi wanakamuliwa na sisyemu, uwe mwanachama au la!

    Njia ya kuepuka na kukamuliwa huko sio kuwa mwoga au kuendekeza uwoga. Lazima ujuwe kuwa hivi sasa wewe mwananchi unalaliwa na sisyemu. Umelaliwa! Ni jukumu lako kuamua kupigania kutolaliwa au kuendelea kulaliwa.

    Iwapo utaogopa kupambana dhidi ya kulaliwa, basi pigana. La sivyo, usilalamike, endelea kusema sisyemu juu, makamba juu juu ... uup moreee!

    Ni muhimu kukiri kuwa iwapo tutaamua kupambana, lazima purukushani itatokea - tutapata madhara mbalimbali na tofauti kati yetu. Hiyo itawahusu wale ambao hivi sasa wameng'ang'ania madaraka (sisyemu). Kama yule mshee alivyosema, ishu hapa ni kuwa hivi sasa sisyemu wanastarehe kutokana na rasilmali ambazo wanyonge (wewe mkulima na mfanyakazi) tunanyimwa, wakati sie kila siku tunaamka saa 10 asubuhi ili kupata kipato cha kuwaongezea sisyemu na serikali yao.

    Tukiamua kupambana ili kujikomboa ni kuwa sote tutakuwa 'on the mooove'. Wote tutaathirika, hivyo kufanikiwa kuwapunguzia ile gepu ya starehe waliyonayo hivi sasa pamoja na dharau wanazotuonyesha. Hii ndiyo hofu kuu waliyonayo hawa watawala.

    Uamuzi upo kwetu, kunyoa au kusuka.

    Mama Nyerere, tunakuheshimu sana na maoni yako ni muhimu - lakini yamekuja wakati ambao sio wa mijadala bali eksheni. Hawa watu mliwalea na sasa wameota mizizi ambayo ni lazima ing'olewe.

    Watanzania tusimame. Tumekalishwa vya kustosha

    ReplyDelete
  11. Malkiory asante sana kwa hiyo taarifa ya mmiliki wa Dowans kwamba ni Rostam...kweli happo hakuna siri tena huyu muhindi asilipwe hizo hela!!!!!
    Haiwezekani taifa zima liumie kwasababu yake...

    ReplyDelete
  12. Hiyo link(website) ipo na ina hizo taarifa, labda internet yako ilikuwa na shida lakini hiyo kurasa ipo kwenye hiyo tovuti....

    ReplyDelete