Na Suleiman Abeid, Shinyanga
HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga imeendesha operesheni ‘Safisha Mji’ kwa kumwaga vyakula vya mama lishe, kuzoa viatu madukani na
kukamata baiskeli za wananchi zilizokuwa zimeegeshwa nje ya maduka na masoko vikidaiwa kuwa ni uchafu, ikisaidiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Mbali ya tukio, pia wakazi wa manispaa hiyo wameshangazwa na kitendo cha kutumika kwa FFU waliokuwa na bunduki, mabomu ya kutoa machozi na simu za upepo (radiocall) mikononi badala ya askari mgambo wa manispaa kama ilivyokawaida na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi.
Opresheni hiyo iliyofanyika wiki iliyopita ilisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wajasriamali wadogo na wafanyabiashara wa maduka ya mabegi na viatu huku akina mamalishe wengi wakilia, wakilalamika kukatika kwa mitaji yao na kudai watashindwa kurejesha mikopo waliyokopa.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati na maeneo tofauti juzi baadhi ya wakazi hao walielezea kushangazwa kwao na kitendo cha manispaa kuamua kukamata baiskeli za wananchi zilizokuwa zimeegeshwa kando ya maduka au masoko ambapo walisema walipofuatilia walielezwa kuwa zilikuwa zimeegeshwa ovyo.
“Kwa kweli kama ni uonevu huu sasa umevuka mipaka, tangu lini baiskeli ikawa uchafu au ikawa na eneo maalumu la kuegeshwa? mimi niliegesha baiskeli yangu nje ya soko la nguzo nane nikaingia ndani kwa ajili ya kununua mahitaji ya nyumbani, niliporudi nikakuta watu wa manispaa wakisomba baiskeli na kuzipakia katika lori lao,”
“Nilijaribu kuuliza nikaelezwa kuwa zimekutwa zimeegeshwa ovyo hivyo ni sawa na uchafu na kama nahitaji kurejeshewa baiskeli yangu nilipe shilingi 5,000 kama faini, wapo waliolipa, binafsi nilishindwa nikaacha wakaondoka nayo pamoja na baiskeli za watu wengine,” alieleza mmoja wa wazee ambao baiskeli zao zilikamatwa.
Kwa upande wake mmoja wa akina mamalishe ambao walikamatwa na vyakula vyao kumwagwa alisema kitendo hicho kimemweka katika wakati mgumu kutokana na kwamba fedha aliyokuwa akitumia kama mtaji wa biashara yake ilikuwa ni ya mkopo.
“Walininyang’anya sufuria langu la mihogo wakamwaga, sufuria wakabeba, nilipoomba wanirudishie waligoma na kunitaka nilipe shilingi 5,000, niliwaeleza sina bali nina shilingi 3,000, mgambo mmoja akazipokea lakini ajabu hawakunirudishia sufuria langu wakaondoka nalo pamoja na hela zangu,” alieleza mmoja wa mama ntilie huku akibubujikwa machozi.
Naye mfanyabiashara ya viatu na mabegi katika majengo ya ofisi za CCM mkoani Shinyanga alidai maofisa hao wa manispaa wakiwa na polisi wanne wenye silaha na mgambo walifika dukani kwake na kumzolea viatu na mabegi yaliyokuwa yamening’inizwa mlangoni kwa ajili ya kuvutia wateja.
“Kwa kweli nilishangazwa na kitendo hicho, hivi viatu na mabegi yalikuwa juu yakining’inia kama ‘show’ kwa wateja, lakini walichukua na kutupia ndani ya gari lao, hakuna kilichoorodheshwa ili nikiamua kuvifuata niweze kuvitambua, vyote vilikuwa vikichanganywa ovyo na vya watu wengine,” alieleza mfanyabiashara huyo.
Mfanyabiashara huyo alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha uongozi wa manispaa kuamua kukamata bidhaa zilizoko madukani na kuwaacha wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi ambao wengi wao wameweka nondo, mapipa na matoroli, wanazouza nje katika maeneo ya watembea kwa miguu.
Kwa upande wake ofisa afya katika manispaa hiyo, Bw. Elly Nakuzela alikiri kuendeshwa kwa oprsheni hiyo huku akikanusha madai ya waliokamatwa kutozwa shilingi 5,000 na kwamba madai hayo yalisababishwa na hasira za watu kukamatiwa mali zao.
“Ni kweli tuliendesha operesheni usafi katika mitaa ya mjini, lengo letu ni kutaka kuuweka mji katika hali ya usafi, kabla ya kufanya zoezi hilo tulipita tukiwatangazia wafanyabiashara wote wanaofanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa kuondoa biashara zao, lakini juzi tulipopita tulikuta bado wapo tuliamua kuwakamata,” alieleza.
Bw. Nakuzela alifafanua kuhusiana na suala la kutumia polisi wenye silaha kuwa lilisababishwa na baadhi ya wafanyabiashara waliogoma kukamatwa kwa mali zao na kutishia kuwapiga maofisa afya, hivyo ikabidi kuomba nguvu ya polisi hao.
Alikanusha madai ya kuwepo kwa mianya ya rushwa katika operesheni hiyo kutokana na kutowakamata wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi wanaoweka bidhaa zao nje katika maeneo ya watembea kwa miguu, akisema kuwa baada ya muda si mrefu wataanza pia zoezi la kukamata vifaa hivyo vinavyowekwa bila mpangilio.
Pia alifafanua juu ya uamuzi wa kuzikamata baiskeli za wananchi zilizokuwa zimeegeshwa nje ya maduka na masoko kwa kueleza kuwa wenye baiskeli hao walikuwa wameziweka ovyo katika maeneo yasiyoruhusiwa (japo hakutaja maegesho rasmi kwa ajili ya baiskeli) na kudai kuwa uegeshaji huo unachangia uchafu katika mji.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alikiri polisi kushiriki katika operesheni hiyo ya safisha mji baada ya kuombwa na watu wa manispaa waliodai kuwepo kwa dalili za kutokea hali ya uvunjifu wa amani wakati zoezi hilo likiendelea.
Inspecta General(IGP) Said Mwema hebu tueleze watanzania utaratibu wa kutumia FFU ukoje? Inashangaza kuona tunatumia bunduki na silaha nzito kutishia watanzania ambao wanawalipa mishahara kupitia kodi wanazotoa. lakini kinachosikitisha zaidi ni uwezo wa askari hawa wa FFU katika kutuliza ghasia ni mdogo mno na wahitaji training,. Tumeangalia kwenye runinga zetu fujo zilivyotulizwa Arusha, chuo kikuu cha Dodoma(UDOM) na katika uchaguzi uliopita kule temeke,mwanza na kwingineko. kwanza hawana discipline kwenye riot drill wanatakiwa wapelekwe kwenye mafunzo vinginevyo hawa ni wauaji kwa sababu riot drill haina uhusiano na risasi ya moto, kupiga watu virungu, kuchania watu nguo, kuvunja vioo vya magari na kushiriki kuiba vitu vya watu . Jifunzeni kwa wenzenu Misri rate ya kutumia silaha ni pale tu inapotokea hakuna jinsi. majibu ya IGP huwa yanipa wasiwasi kama na yeye anakuwa makini nionavyo mimi hupokea ripoti ambazo hasomi ama kwa kuamini makamanda wake na napenda kukuonya kuwa TV NA REDIO SIO MAHALI PA KUFANYIA KAZI. Uliwahi kuona wapi mkuu wa jeshi la polisi kila mara anaonekana akiongea kwenye vyombo vya habari mambo ambayo hayatatuliwi au ufumbuzi wake uko mbali. polisi ni jeshi na siyo SIASA.
ReplyDeleteHivi shinyanga yangetokea madhara ungejibu nini safari hii maana Arusha ulipoteza hela ya walipa kodi kwa kuonyesha VIDEO ya matukio yaliyochaguliwa kutetea uamuzi mliochukua. JAMANI DAMU YA WATANZANIA MNAYOMWAGA INAWALILIA MWOGOPENI MUNGU.
Saidi Mwema alifanya kazi nzuri sana alipokuwa RPC Mbeya! Basi. Uwezo wake ulikuwa limited on Police Commissioner level. Nafasi aliyo nayo sasa inamzidi kimo. Inasikitisha kuona amepewa tu kwa vile ni Ndugu ya Salma Kikwete. Si unajua tena Mzee hana kauli kwa Mama. Hata akisema aruke kichura kwenye viwanja vya Ikulu ataruka tu.
ReplyDelete