04 January 2011

Mahabusu waliovua nguo kushtakiwa

Na Cresensia Kapinga, Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linatarajia kuwafikisha mahakamani mahabusu 23 wanaokabiliwa na kesi za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha kujibutuhuma mpya
za kufanya fujo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Ruvuma kwa kuvua nguo na kusababisha mahakama hiyo kusimamisha shughuli zake kwa muda.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Bw. Michael Kamuhanda alisema kuwa kitendo cha mahabusu hao kufanya fujo
Desemba 27, mwaka jana majira ya saa 6:30 mchana, mahakama ililazimika kusimamisha kesi ambazo zilikuwa zisikilizwe tarehe hiyo kwa muda.

Alifafanua kuwa kitendo hicho licha ya kusababisha usumbufu mkubwa mahakamani hapo, pia kilisababisha uvunjifu wa amani katika eneo la serikali ambapo watu wengi walijitokeza kuwaona mahabusu hao wakivua nguo zao na kubaki watupu,
jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi

Alieleza zaidi kuwa taratibu zote za kuwafikisha watuhumiwa mahakamani zimekamilika na kwamba wakati wowote kuanzia sasa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanaowakabili.

Katika madai yao, mahabusu hao walielekeza shutuma zao nzito kwa ofisa upelelezi mkoani Ruvuma kuwa yeye ndiye sababu na chanzo cha kesi zao kucheleweshwa wakidai kuwa amekuwa akitaka wampe fedha huku wao wakiwa ni watoto wa wakulima ambao hawana uwezo wa kifedha.

Walidai kuwa kutokana na hali hiyo ya kucheleweshewa kusikilizwa kwa kesi zao wamemuomba Bw. Kamuhanda afike kusikiliza kilio chao jambo ambalo halikuwezekana mpaka
alipofika Mkuu wa Kituo cha Polisi, Bw.Peter Kubezya na kujaribu kuzungumza nao kwa muda wa zaidi ya saa moja.

Katika mazungumzo hayo, mahabusu hao walimtaka
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Christine Ishengoma afike asikilize kilio chao cha muda mrefu bila mafanikio.

Kamanda Kamuhanda alisema kuwa watuhumiwa hao ni wa kesi za
mauaji na unyanganyi wa kutumia silaha ambazo ni zote ni za mwaka huu tofauti na wanavyodai wao.

Alisema kuwa baadhi yao wanadaiwa kuhusika na uporaji wa silaha mbili aina ya SMG na risasi sitini za jeshi la polisi mjini Songea tukio ambalo lilihusisha kuwajeruhi vibaya askari polisi wawili.

Alisema kuwa wengine wanatuhumiwa kwa mauaji ya kinyama ya mama na mwanawe yaliyotokea katika mtaa wa Lizaboni siku chache baada ya tukio la kuporwa kwa bunduki mbili, mauaji ya mfanyabiashara mmoja katika mtaa wa Bombambili mjini
Songea na mauaji ya dereva taxi wa mjini hapa.
 
Hata hivyo, Bw. Kamuhanda alisema kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mwanasheria wa serikali wanafanya jitihada za kuhakikisha upelelezi wa kesi hizo unakamilika na wanatendewa haki, kinyume na malalamiko yao.

No comments:

Post a Comment