04 January 2011

CUF yataja mafanikio yake 2010

Na Peter Mwenda

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kitaboresha mafanikio yaliyopatikana 2010 kwa kuwa chama pekee cha upinzani kuwa na wabunge wengi wa kuchaguliwa na
chama cha kwanza cha upinzani Tanzania kuingia serikalini kwa mujibu wa katiba upande wa Zanzibar.

Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema kuwa mafanikio mengine ni kuwepo wa mshikamano ndani ya chama ambapo viongozi na wanachama wamekuwa hawahitilafiani katika masuala ya msingi.

Alisema utaratibu wa shughuli za chama umefanywa kwa kufuata katiba ya chama na misingi mikuu ya uendeshaji wa chama bila kugongana kitaratibu na kiutendaji.

Aliongeza kuwa mafanikio mengine ni ya uteuzi wa wagombea wa urais Jamhuri ya Muungano na Zanzibar ambapo kilisimamisha wagombea wanaokidhi sifa za kuongoza nchi kwa mafanikio.

Bw. Mtatiro alisema mafanikio katika uchaguzi mkuu kwa kupata idadi ya wabunge kutoka sifuri mwaka 2005 hadi wawili mwaka jana upande wa Tanzania bara; na wabunge 19 mwaka 2005 hadi 22 mwaka 2010 upande wa Zanzibar.

Alisema idadi ya madiwani imepanda kutoka 96 mwaka 2005 hadi 152 mwaka 2010 upande wa Tanzania bara; na kuwa chama hicho ndicho kilichoimarisha utaifa mwaka 2010, kwa kupata wawakilishi na wabunge kutoka katika kila upande wa muungano.

"Kwa mfano, tumepata wabunge bara, Unguja na Pemba lakini CCM wamepata wabunge bara na unguja peke yake na CHADEMA wamepata wabunge bara peke yake," alisema Bw. Mtatiro.

Alisema CUF imendelea kupata wabunge wengi wa kuchaguliwa kuliko vyama vingine vyote vya upinzani, mwaka huu 2010 imepata wabunge 24 waliochaguliwa kwa kura na wananchi.

Bw. Mtatiro alisema kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kulikotokana na kura za maoni ya wananchi wa Zanzibar walipoamua kuwa kuanzia uchaguzi wa 2010 chama kitakachoshinda uchaguzi kwa upande wa Zanzibar kitatoa rais na kitakachokuwa cha pili kitatoa makamu wa kwanza wa rais.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa baada ya uchaguzi mkuu, CUF imekuwa ya pili Zanzibar na hivyo maamuzi ya wananchi ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa yakatekelezwa.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema CUF imekuwa chama cha kwanza cha upinzani Tanzania kuingia serikalini kwa mujibu wa katiba upande wa Zanzibar.

3 comments:

  1. Ni mwanzo mzuri kwa wana cuf sasa mumeshaingia madarakani tunawaaomba mufanye kazi kwa ari na nguvu ili mupate kuwatumikia wananchi muda wa siasa sasa umekwisha tufanye kazi tujikomboe kwa umasikini

    ReplyDelete
  2. Lakini ni keli CUF lazima tukubali kuwa imepiga hatua kubwa sana. Lakini pia inaonyesha umuhimu wa kubadilisha Katiba. Si vizuri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania(tanganyika na Zanzibar) awe amechaguliwa upande mmoja tu wa muungano na upande wa pili uwe umemkataa kabisa. Huyo atakuwa Rais wa bara na atakuwa hana jukumu kwa Zanzibar. Ilikuwa alau Rais wa Jamhuri ya Muungano apate alau asilimia 40% ya kura za upande wowote wa Muungano ndio awe Rais.

    Tunataka mabadiiliko

    ReplyDelete
  3. wakati bara mko hoi utuambie wakati wakina Lwakatare wapo kwa upande wa bara tu

    ReplyDelete