26 January 2011

Madai ya walimu waliokosa ajira yatua OWM

Na Benjamin Masese

HATIMAYE sakata la baadhi ya walimu waliohitimu mafunzo yao ya ualimu mwaka 2009/2010 na kushindwa kuajiriwa limetinga katika Ofisi za Waziri Mkuu (OWM) na
kuungwa mkono kwamba wana hoja za msingi za haki ya kuajiriwa.

Tofauti na juzi ambapo walimu hao walitinga ghafla katika ofisi za Waziri Mkuu kwa maandamano baada ya kushindwa kupata majibu mazuri kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Hamisi Dihenga, ambapo walikumbana na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) getini na kuwataka kufuata utaratibu wa kuonana na viongozi husika, jana walipata mapokezi mazuri na maelezo ya kutia matumaini.

Hata hivyo, jana walimu hao walipokewa na Katibu wa Waziri Mkuu na msaidizi wake baada ya kutimiza taratibu zote zilizotakiwa ambapo walifanya kikao cha pamoja kwa saa kadhaa kusikiliza madai yao na hatua zilichokuliwa na wizara husika.

Viongozi hao walisema kuwa kwa mujibu wa maelezo ya walimu hao, kama kweli hawakusema uongo au kuchanganya mada, wanatakiwa kuajiriwa kulingana na mikataba na miongozo kutoka vyuoni walikosomea.

Walisema kuwa kutokana na madai hayo kuwa na mlolongo mrefu wa maelezo, watahitaji kutafuta ukweli katika upande wa pili wa wizara, ili kujua utaratibu uliopo wa kutoa ajira kwa mwaka huu na kuahidi kutoa jibu kamili kesho.

Hata hivyo viongozi hao waliwataka walimu hao kuwapa  hoja zao za msingi kimaandishi zitakazowasaidia watakapokutana na upande wa wizara ambapo walimu waliandika na kuwakabidhi muda huo.

Akizungumza na Majira, Msemaji wa walimu hao, Bw. Bakari Achimwale kutoka chuo cha walimu Shinyanga, alisema kuwa ameeleza ukweli wa mambo yalivyo pamoja na majibu waliyokuwa wakiyapata kutoka kwa wizara ya elimu tangu wiki iliyopita hadi juzi walipopata majibu yasiyoridhisha na kuwakatisha tamaa.

Alisema wao kama walimu halali waliosoma vyuo vinavyotambulia, hawatakubali kupoteza ajira yao kutokana na uamuzi mbovu uliotolewa na Wizara ya Utumishi kuajiri walimu 9,226 na kuacha wengine wenye vigezo kwa kisingizio cha kufeli somo moja.

Alisema utaratibu huo wa kuajiri walimu waliofaulu masomo yote ni mgeni kwao, na katika mikataba ya chuo hawajawahi kuusikia.

Juzi Bw. Dihenga alitoa tamko kwamba wizara haina mpango wowowte wa kuajiri walimu wengine huku akisisitiza kwamba lazima walimu waliofeli kujisajili upya kwa lengo la kurudia mtihani wao kabla ya Mei mwaka huu ili kuangaliwa upya.

Alisema kuwa kulingana na maagizo kutoka wizara ya utumishi ya kutoajiri tena walimu, aliwataka walimu hao kulipia fedha zao Baraza la mitihani la taifa (NECTA) kurudia mtihani na si vinginevyo.

1 comment:

  1. NAPENDA KUWATAHADHARISHA PIA WALIMU HAWA KUWA HIYO NI RASHARASHA TU YA MAMBO WATAKAYOKUTANA NAYO KWENYE AJIRA. HATA KAMA WATAPATA AJIARA ZAO KITAKACHOFUATA NI KUPATA MISHAHARA NA HAPO ITAKUWA DANADANA KATI YA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI, UTUMISHI NA HAZINA. SAMBAMBA NA HIYO VITUO WATAVYOPANGIWA VYA KAZI NI VIJIJINI HAKUNA USAFIRI, UMEME, NA PIA FEDHA ZA KUANZIA KAZI HAKUNA. MWISHO WAKUMBUKE KUWA KUPATA NAFASI ZA MIJINI NI NDOTO KWAO LABDA UWE MTOTOT WA MAWAZIRI.

    ReplyDelete