25 January 2011

Leonardo aonja kipigo cha kwanza Inter Milan

MILAN, Italia 

KOCHA mpya wa Inter Milan, Leonardo amekutana na kipigo cha kwanza katika mechi zake sita alizoiongoza timu hiyo baada ya kuchapwa mabao
3-1 na Udinese.

Kipigo hicho kimetoa mwanya kwa timu yake ya zamani AC Milan, ambayo iliichapa Cesena kuendelea kutesa kileleni mwa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi nne.

Ushindi wa mabao 2-0 wa timu inayoshika nafasi ya pili, Napoli kwa timu inayoshika mkia, Bari unaelezewa kusababisha madhara kwa Inter Milan ambayo inashika nafasi ya tano ikiwa na mechi moja mkononi kwa kuwa nyuma kwa pointi tisa kwa vinara wa ligi hiyo, AC Milan na pointi tano nyuma ya Napoli huku ikiwa katikati ya kampeni za kuwania ubingwa huo.

Katika mbio hizo za kuwania ubingwa,  Lazio ilichapwa mabao 3-1 na timu ya Bologna na Juventus, ikatoka suluhu na klabu ya zamani ya kocha, Luigi Del Neri, Sampdoria katika mechi iliyokuwa ya vuta ni kuvute huku ikishuhudiwa  Alessandro Del Piero, akikosa nafasi ya wazi katika muda wa nyongeza.

Mchezaji wa Inter Milan, Dejan Stankovic ndiye aliyeipatia bao la kwanza timu yake baada ya kupokea pasi kutoka kwa Thiago Motta, lakini bao hilo likasawazishwa na beki wa  Udines, Cristian Zapata kwa shuti la  guu la kushoto lililomshinda mlinda mlango, Luca Castellazzi.

Mfungaji bora wa ligi hiyo ya Serie A, Antonio Di Natale ndiye aliyepachika bao la pili dakika ya 25 kwa mpira wa adhabu na Maurizio Domizzi akaongeza la tatu baada ya kumchambua mlinda mlango, Castellazzi kipindi cha pili.

Tangu kocha huyo Leonardo awasili katika timu hiyo, ili kuchukua mikoba ya kocha Rafa Benitez Desemba 24 mwaka jana mabingwa hao wa Ulaya wameshashinda mechi tano mfululizo, hali ambayo ilikuwa imefufua matumaini ya kwamba kikosi hicho kwa sasa kimerejea katika njia ya ushindi kabla ya kukutana na kisiki hicho.

“Tulianza vyema lakini baadaye, Udinese wakawa kwenye kiwango cha hali ya juu,” kocha huyo wa zamani wa AC Milan, Leonardo ambaye wachezaji wake Julio Cesar, Wesley Sneijder na Diego Milito wapo nje ya uwanja wakiwa majeruhi," aliiambia Sky.

“Endapo watakuwa wakicheza namna hiyo itamuwia vigumu kila mtu kuwafunga,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment