19 January 2011

Kijiji cha Kunduchi hatarini kutoweka

Na Job Ndomba

KIJIJI cha kihistoria cha Kunduchi Pwani jijini Dar es Salaam, kipo hatarini kutoweka kutokana na maji ya nguvu ya bahari yanayodaiwa kusababishwa na kingo zilizojengwa na baadhi ya hotel za kitalii zinazozizunguka kijiji hicho.Akizungumza na
Majira juzi, Mwenyekiti wa Mtaa Kijiji cha Kunduchi Mtongani,  Bw.Richard Rusisye alisema, kijiji hicho cha kihistoria kinachoaminika kuwa na makaburi yenye zaidi ya miaka 1000,

Alisema kuwa  kitatoweka endapo hatua za kuzuia mmonyoko huo kutokana na kwa eneo hilo pekee kubakia bila kingo za kuzuia maji na hivyo kuonekana ni sehemu pekee ambapo maji yanaweza kuendelea kupunguza sehemu ya ardhi ya kijiji hicho.

"Kijiji hiki ni cha kihistoria na kinaaminika kuwa,kina makaburi yenye miaka zaidi ya 1000, lakini kipo hatarini kutoweka kwakuwa kinamalizwa na maji ya nguvu ya bahari yanyoendelea kupunguza sehemu ya ardhi ya Kijiji hiki kutokana na baadhi ya hoteli kuweka kingo za kuzuia maji na kuliacha eneo la kijiji hicho pekee," alisema  Bw.Rusisye.

Alisema,hatua za haraka zinahitajika kukinusuru kijiji hicho, kwani bila kufanya hivyo ile hali ya kitalii iliyonayo kijiji hicho inaweza kupotea.

Aliongeza kuwa, licha ya uongozi wake kwenda kuzungumza na baadhi ya hoteli zinazozunguka kijiji hicho ili kuweza kusaidia kupunguza kasi ya maji yanyosababisha kuondoka kwa ardhi ya eneo hilo na kutokana na wao kujenga vizuizi pekee, lakini hatua hizo ziligonga mwamba kutokana na wao kushindwa kutoa ushirikiano.

"Mara kadhaa tumeweza kuwafuata wenzetu hawa ili tushirikiane kujaribu kutatua tatizo hili lakini hawajaweza kutoa ushirikiano hali inayonifanya sasa niweze kuomba nguvu nyingine ya ziada itumike ili iweze kukinusuru kijiji hiki," alisema Bw. Rusisye.

Sambamba na hilo, alizitaka hoteli zinazozunguka Kijiji hicho kushiriki katika utunzaji wa mazingira, kwakuwa  wao ni sehemu ya jamii na hivyo kutakiwa kushiriki katika shughuli hiyo.

Alisema utunzaji wa mazingira, si tu kwa kufanya usafi bali pia kwa kuangalia uharibifu unaotokea kandokando ya ufukwe wa Bahari ya Hindi, pamoja na kuitunza mikoko ambayo ni moja ya rasilimali za taifa.

No comments:

Post a Comment