19 January 2011

TAS Taifa yakanusha tuhuma dhidi ya wizara

Na Anneth Kagenda

CHAMA cha Albino Tanzania (TAS), kimekanusha shutuma zilizotolewa na Chama cha Albino Mkoa wa Shinyanga kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inawafanyia majaribio walemavu wa ngozi na kwamba majaribio hayo
yanaweza kuwasababishia madhara makubwa vikiwemo vifo.

Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Bw. Ernest Kimaya ilisema kuwa chama kina msemaji wake mkuu ambaye ni yeye na kwamba taarifa zilizotolewa na viongozi wa Shinyanga sio msimamo wa chama cha Albino Tanzania.

"Chama kimefanya kazi kubwa kukaa na wizara kujadili upatikanaji wa mafuta ya kulainisha ngozi na kuzuia mionzi ya jua, hatimaye wizara ilikubali na kuanza utaratibu huo mwaka 2010 mwishoni," ilisema.

Ilieleza kuwa wizara iliwapatia mafuta hayo na chama kuyapeleka kwa mtaalam ambaye ni mshauri juu ya mafuta ya ngozi na kuwambia kwamba yanafaa na kwamba wanaweza kugawa kwa wananchi wote wa Tanzania.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa zoezi hilo limeleza chama hicho kikiwa kinasoma mapungufu yaliyopo katika shughuli na mwisho kikakaa na viongozi wa wizara ili kujadili mapungufu na kujadili maboresho ya shughuli  husika.

"Kwa hiyo viongozi wa mkoa walipaswa kuleta mapendekezo yao Makao Makuu ya Chama cha Albino Tanzania, maelekezo ambayo walipewa wafanye hivyo na Katibu Mkuu na kila jambo linalofanyika katika chama lina hatua zake za kupitia hadi kufikia kuwa tamko la chama," ilieleza taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa matamko ya mikoani yanaweza kutolewa na Mwenyekiti wa Mkoa kwa kupata baraka kutoka Makao Makuu na kusema kuwa Chama kinaiomba serikali kuelewa na kwamba kipo nayo bega kwa bega kushirikiana kwa masuala mbalimbali kwa manufaa ya Albino wa Tanzania.

kauli hiyo imekuja baada ya  Chama cha Walemavu wa Ngozi Albino (TAS) Mkoa wa Shinyanga kusema kuwa baada ya kupokea mafuta aina ya ENAT Natural vitamin E cream kutoka nchini Australia, wamebaini kwamba yana madhara makubwa kwao na hayafai kutumiwa na albino hapa nchini.

No comments:

Post a Comment