*Ni kuhusu kuridhia mabadiliko ya katiba 2011
*CUF wahoji, ni kuweka viraka, au katiba mpya
Na Rabia Bakari
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuweka wazi msimamo wa kauli yake kuhusu mabadiliko ya katiba, endapo inawekewa viraka ama inaandikwa upya. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu
Naibu Katibu Mkuu Bara, Bw. Julius Mtatiro, alisema kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa wakati wa kuukaribisha mwaka mpya, imejaa utata mkubwa, na haikuwa wazi kwa wananchi kiasi cha kuchanganya watu.
"CUF kinaunga mkono kauli ya Rais ya kuanzisha mchakato wa katiba lakini tunatilia mashaka aina ya katiba ambayo anaitaka kutokana na maneno ambayo aliyatumia katika hotuba yake.
"Nikimnukuu hapa anasema 'Jambo la nne ambalo tulikubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi Yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne'."
Kauli hii ya rais ina utata mkubwa kwani hakutaka kusema wazi anasimamia lipo kati ya katiba mpya au kuweka viraka kwa katiba iliyopo," alisema Bw. Mtatiro.Aliongeza kuwa wanaitilia mashaka kauli hiyo kutokana na ukweli Rais Kikwete na watendaji wake wamekuwa wakitofautiana katika suala hilo.
Aliwataka watendaji hao kuwa ni Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, ambao wote kwa nyakati tofauti walisema katiba mpya kwa sasa haiwezekani, na hakuna umuhimu, bali kinachowezekana ni kuifanyia marekebisho hii ya sasa.
"Sote tunafahamu kuwa rais wetu hana utaalamu wa mambo ya kisheria, inapotokea watendaji wake wa karibu na wataalamu wa sheria wanatofautiana naye kimtazamo kiasi cha wao kusema hadharani misimamo yao, halafu rais naye anakuja na msimamo wake, inaleta mashaka," alidai.
Akitoa msimamo wa CUF katika hilo, Bw. Mtatiro aliitaka ikulu itoe ufafanuzi wa kauli ya rais ili wadau na Watanzania wote wajue rais anaangukia katika msimamo upi.
Alidai kuwa nia matatarajio ya CUF kuwa Rais Kikwete atakidhi matakwa ya Watanzania walio wengi ambao wanahitaji kwa dhati uwepo wa katiba mpya itakayoandikwa upya ili kukidhi kizazi cha sasa.Aidha alisema CUF wanamtaka Rais Kikweta kuwapumzisha watendaji wake walioonekana kuropoka kwa madai kuwa watakuja kumtia aibu kama ya viongozi waliopita.
"CUF inawaomba Watanzania wakae tayari kuishinikiza serikali iwapo watatokea wajanja wanaotaka kutupatia katiba yenye viraka, iwapo tutaandika katiba mpya chini ya Rais Kikwete atakuwa rais wa pekee Tanzania katika kuimarisha mfumo wa demokrasia na atakumbukwa mno na vizazi vyote," alidai Bw. Mtatiro.Sambamba na hayo, pia Bw. Mtatiro alisema CUF inaenda kuishtaki serikali kwa wananchi kwa njia mbalimbali kutokana na kuwapa gharama kubwa, kutokana na kupanda kwa gharama za umeme.
Alisema serikali ya CCM haina ubunifu wa vyanzo vya umeme, wakati vipo vingi na hivyo kusababisha mzigo mkubwa wa gharama kwa wananchi na kudidimiza uchumi.Aliongeza kuwa japo rais alizungumzia suala la umeme katika hotuba yake lakini hajajibu maswali ya wananchi na wala hajatoa suluhisho litakaloleta unafuu wa maisha ya Mtanzania katika matumizi ya nishati hiyo.
"Wakati pakiwa na ongezeko kubwa la bei za umeme, lakini nishati hiyo haipatikani na hata pale inapopatikana haitoshi, na serikali ya CCM bado inajipa matumaini kuwa hali hii itaimarika lakini muda unavyozidi kwenda ndiyo matumizi ya umeme ambao haupo yanaongezeka kutokana na ongezeko la watu, wawekezaji nakadhalika," alisema Bw. Mtatiro.
Alidai kuwa kwa hali ya wazi Rais Kikwete ameaihidi utekelezaji wa miradi mingine kadhaa itakayotoa takriban megawati 1,130 katika kipindi cha 2011-2013, jambo ambalo litakuwa maajabu ya dunia."Yaani serikali iliyoweza kuongeza uzalishaji wa megawati 145 tu katika kipindi cha miaka mitano, itaweza vipi kuzalisha megawati 1,130 kwa kipindi cha miaka mitatu? Watanzania wanadanganywa mchana kweupee tena bila chembe ya aibu.
Katika kuungana na Watanzania kuishinikiza serikali isitafute unafuu wa mikataba feki na ya kifisadi kama Dowans na kadhalika kupitia migongo yao, CUF kinajiandaa kuishtaki serikali kwa Watanzania kupitia njia mbalimbali, ili tusaidiane kuishinikiza, kwa sababu hawakuichagua ili iwacharaze bakora kiasi hicho," alisisitiza.
Watanzania jamani tusiingize siasa kwenye jambo mhimu kama katiba. Kwa hiyo tuwe waangalifu na kauli zetu. Si kwamba kila kilichoko kwenye katiba ya sasa ni kibaya. Yapo mengi mazuri sana kwenye katiba yetu ya sasa. Tena ilitungwa wakati hakuna tension kama ilivyo sasa. Tena wakati ule neno kubwa lilikuwa mshikamano. Leo hata watu wanapofikiria juu ya katiba mpya mawazo yao yote yako kwenye maslahi yao binafsi. Kila mtu anataka kuona maslahi ya kikundi chake. Hiyo ni hatari sana kwa usitawi wa taifa letu. Kuna watu tayari wanajitayarisha kutaka makabila yao, dini zao zipendelewe kuliko makabila mengine au dini nyingine zipendelewe kuliko dini zingine. Hapo ndipo zogo litakapoanzia. Ni mhmu kwa serikali yetu kuwa makini sana katika kipindi mhimu cha uhai wa taifa letu. Kuundwa katiba mpya si kigezo cha kubeza kila kilicho kwenye katiba yetu ya sasa
ReplyDeletejaani hii inashangaza, katiba ya sasa inalinda masilai ya ccm na viongozi wake hasa mafisadi kama mkuu alivyokuwa anawanadi majukwaan, ndo maana hawataki kubadili katiba mpya ,hivi ni halali kutooji matokeo ya rais wakat ya wabunge na madiwani yanawoiwa, watanzania tushikamane hii katiba ya sasa itatupeleka pabaya.
ReplyDeleteBila CHADEMA kukuacha bungeni wanainchi wasingeweza kupata mukari wa kubadilishwa katiba. Hongera Chadema, message sent and delivery, CCm mcjifanye nyie ndo mmebadilisha katiba, wazo hilo hamkuwa nalo CCM. vyama vya upinzani unganeni ili katiba isichakachuliwe
ReplyDeleteJamani Watanzania someni katiba,muelewe maana yake na inaeleza nini? kuna watu wanaimba tu,mnaimbishwa tu,katiba ina mambo mengi sana ya msingi yanayotakiwa sasa hivi kuwekwa ndio maana watu wengi tumefurahia masuala ya katiba mpya kukubaliwa na Rais.wewe kama mdau wa katiba hebu jiulize nini kinakusibu,achana na vyama vya siasa hawa wanasomba hazina yetu kuanzia ruzuku,marupurupu ya wabunge,mishahara ya wabunge,kiinua mgongo cha wabunge,upendeleo katika mambo ya kijamii kama vile kesi ya mbunge mahakamani ya kuua itachukua miezi miwili kusikilizwa yako utaozea jela miaka kumi unaambiwa uchunguzi unaendelea,angalieni mambo ya msingi yanayokuumiza ,wanasiasa wameteka nyara hoja hii kwa maslahi ya vyama vyao na wenyewe binafsi.hebu bwana mkubwa juu tuambie katika kifungu gani cha katiba kinalinda au kutamka kulindwa kwa mafisadi. Tuache ujinga tusome katiba iliyopo sasa hivi ina kasoro gani na kisha tuwe tayari kutoa mapendekezo kwa katiba ijayo,hivi katiba mpya ikibadilishwa kwa kuwekwa tume huru ya uchaguzi na matokeo ya urais yahojiwe mahakamani ndio imekidhi mahitaji ya Watanzania?
ReplyDelete