24 January 2011

Fuateni utaratibu kuteketeza dawa-Wizara

Na Grace Michael, aliyekuwa Singida

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema kuwa hakuna njia ya mkato wanayoweza kuitumia waganga wakuu, wakuu wa vituo vya kutolea huduma pamoja na
Bohari ya Dawa (MSD) katika uteketezaji wa dawa zilizoharibika bali kupata vibali vya kuteketeza dawa hizo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki mkoani Singida na Bw. Dedan Jones ambaye ni Mratibu Upatikanaji wa Dawa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika semina iliyoandaliwa na MSD ambayo iliwakutanisha wafamasia, waganga wakuu wa wilaya, mikoa, wataalamu kutoa wizarani na wadau wengine.

Hatua hiyo ilitokana na maswali yaliyoibuliwa na washiriki wa semina hiyo ambao walilalamikia mlolongo mrefu wa upatikanaji wa kibali cha kuteketeza dawa zilizoharibika katika vituo vyao.

Ili uweze kuteketeza dawa zilizoharibika ni lazima uwe na kibali cha kufanya hivyo, kwani ikumbukwe kuwa dawa hizo ni mali ya serikali hivyo ni lazima ikaguliwe...tunajua mlolongo uliopo ni mrefu unaosababishwa na kutaka kujua sababu hasa ya kuharibika kwa dawa hizo,” alisema Bw. Dedan.

Kutokana na hayo alisema kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na wizara ili kuona kama mlolongo huo unaweza ukapungua ili dawa zilizoharibika ziweze kuteketezwa kwa wakati.

Akizungumzia suala hilo, Mchambuzi wa Takwimu za Dawa wa MSD, Bw. Lameck Kipiliango alisema kuwa MSD inatarajia kuteketeza dawa zilizoharibika baada ya kufanikiwa kupata kibali cha kuruhusu uteketezaji huo hivyo akawataka wadau wengine kuhakikisha wanafuata taratibu.

MSD iliteketeza dawa mwaka 2004 na tangu kipindi hicho ilikuwa haijateketeza tena lakini kwa sasa imefanikiwa kupata kibali cha kuchoma dawa hizo baada ya kupitia taratibu zote zilizopo na baada ya khapo tutakuwa tunaomba kibali kila baada ya robo mwaka ili kuepukana na mlundikano wa dawa
zilizoharibika,” alisema Bw. Kipiliango.

No comments:

Post a Comment