19 January 2011

FA yamshitaki Rafael Kamati ya Nidhamu

LONDON, England

CHAMA cha Mpira wa Miguu Uingereza (FA) kimemshtaki mchezaji wa Manchester United, Rafael katika Kamati ya Nidhamu kuhusu utovu wa nidhamu aliouonesha katika mchezo ulioikutanisha timu yake na Tottenham.Beki huyo
wa kushoto, raia wa Brazil alitolewa nje ya mchezo huo dhidi ya Tottenham, uliofanyika Jumapili  kwenye Uwanja wa White Hart Lane alitolewa nje baada ya kupewa kadi mbili za njano.

Akiwa tayari ameshapewa kadi ya kwanza ya njano katika dakika 45 za kwanza, Rafael alioneshwa kadi nyingine ya njano kipindi cha pili baada ya kumfanyia madhambi mchezaji, Benoit Assou-Ekotto.

Hata hivyo katika mashtaka hayo, FA inamshtaki kuhusu tabia chafu aliyoinesha dhidi ya mwamuzi, Mike Dean wakati akimtoa nje ya uwanja ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alikuwa akipinga kutolewa nje kabla ya kupiga teke kinasa sauti cha kurushia matangazo ya televisheni, wakati akitoka nje ya uwanja.

Kutokana na dhabu hiyo, kocha Sir Alex Ferguson alikataa kutoa kauli yoyote kuhusu kutolewa nje Rafael, zaidi ya kumpongeza kwa kazi nzuri aliyokuwa akiifanya wasifungwe.

No comments:

Post a Comment