17 January 2011

Wasomi wamshukia Jaji Mark Bomani

*Ni kwa kutetea malipo kwa kampuni ya Dowans
*Wasema, kama hakurubuniwa, anazeeka vibaya


Na John Daniel
SIKU moja baada ya aliyewahi kuwa mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mark Bomani, kudai kuwa malipo ya sh. bilioni 94 kwa
Kampuni ya Dowans haikwepeki, wanazuoni nchini wamemshangaa Mzee huyo na kudai kuwa kama hakurubuniwa na wahusika wa kampuni hiyo basi anazeeka vibaya.

Wakizungumza na Majira jana wanazuoni hao walisema hawakutarajia kauli kama hiyo kutolewa na Jaji Bomani kwa kuwa ni moja kati ya watu wenye heshima ambao wangeweza kuisaidia serikali badala ya kutoa kauli zenye utata.

"Mimi nilifikiri kwamba Jaji Bomani angetoa ushauri kwa serikali kuwaeleza Watanzania nini kilichomo ndani ya kesi hiyo ya Dowans, hadi sasa wananchi hawajui ukweli kama Mkataba wa Richomnd ulikuwa halali au la, na kama haukuwa halali ndiyo hiyo ya Dowans au ni vitu viwili tofauti.

"Lakini pia kuna kampuni iliyowakilisha TANESCO kwenye kesi hiyo, wananchi wanataka kujua kama kampuni hiyo ina uhusiano wowote na Richmond iliyofutwa au sivyo," alisema Profesa Mwesiga Baregu.

Prof. Baregu ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha jijini Mwanza alilinganisha kauli ya Jaji Bomani na ile ya Mwanasheria Mkuu wa sasa, Jaji Frederick Werema ambayo pia ilipingwa vikali na Watanzania.

Alisema suala la malipo ya Dowans linagusa maslahi ya umma, hivyo ni lazima serikali ichukue taadhari kubwa kabla ya kuitekeleza ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa kina kwa wananchi na si kuharakisha malipo kama inavyoshauriwa na Jaji Bomani.

"Jaji Bomani angeshauri kwanza serikali kuwa wazi kwa wananchi kueleza nini kiini cha tatizo hilo, ni uzembe wa watendaji au udhaifu wa wanasheria kama inavyodaiwa, ieleze hatua zilizochukuliwa dhidi ya walioingiza taifa katika mkataba huo kabla ya kukubali malipo," alisisitiza Profsa Baregu.

Alionya kuwa iwapo serikali itaendelea na mfumo wa kufunika mambo muhimu yanayohitaji maelezo ya kina ili kuondoa mawazo potofu, wananchi watafikia hatua mbaya ya kukosa imani na serikali na kujenga chuki kwa viongozi.

Kwa upande wao wanafunzi wa mwaka wa tatu wa kitivo cha Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliozungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa kwa ma hofu ya kushughulikiwa walisema wanadhani Jaji Bomani anapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa kauli yake ya jana.

"Sisi wanafunzi wa sheria Chuo Kikuu cha Dar es saalam hatukutegemea mwanasheria wa miaka mingi kama Jaji Bomani aongelee suala la Dowans ambalo liko kwenye mchakato wa mahakama, lengo lake nini kama si kuifluence mahakama?" aliohiji mwanafunzi mmoja katika ujunbe wao walioituma Majira.

"Ni aibu kuwa hata wazee kama Bomani wanarubuni na mafisadi kwa pesa na kuwasaliti wananchi masikini, amezeeka vibaya," iliongeza sehemu ya ujumbe huo.

Walisema walitegemea Jaji Bomani kuisaidia serikali kutafuta njia ya kurejea upya uamuzi huo katika kipengele cha uhalali wa mkataba kati ya Richmond na serikali ambayo ndio iliyorithiwa na Dowans.Walisema iwapo mkataba wa Richmond haukuwa halali ni vipi ikirithiwa na Dowans inakuwa halali, na kuitaka serikali kutoa ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo kwanza.Katika mazungumzo yake na gazeti hili jana, Jaji Bomani alitoa kauli ambayo haikutarajiwa na umma ya Watanzania kuitaka serikali kulipa Dowans kwa maelezo kuwa kutofanya hivyo kunaweza kuigarimu zaidi Taifa.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki hii, Jaji Bomani alisema ni vigumu Mahakama Kuu kutengua hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC Court) kama hakukuwa na kasoro zozote katika utoaji hukumu hiyo.

"Kwa kesi za usuluhishi kama hii hukumu hii inaweza kutenguliwa tu kama hao wapatanishi hawakuwa na sifa za kuwa wapatanishi kitu ambacho hapa hakiwezi kutumiwa kwa kuwa katika suala hili, hawa walikubaliwa na pande zote," alisema Jaji Bomani na kuongeza;

"Hukumu hii inaweza kutenguliwa tu kama ikidhihirika kwamba wamepewa rushwa kwa kutoa hukumu ya namna hiyo. Vinginevyo Mahakama Kuu haijihusishi na kuingilia kesi yenyewe.""Mimi kwa upande wangu kama nilivyokwisha kusema siku za nyuma jambo hili liishe ili mitambo hiyo itumike hapa nchini kuzalisha umeme tuondokane na hali ya mgawo na upungufu wa umeme na hilo ndilo jambo muhimu kwa uchumi wa nchi.

11 comments:

  1. Jamani Watanzania mliosema ipo sheria inayowezekana hayo malipo yasilipwe kwa kusajili kesi ya kupinga mahakamani,sasa fanyeni hivyo,acheni kumshambulia huyo mzee maana mambo ya sheria ni magumu,na wewe profesa Baregu ni msomo na hapo ulipo taaluma ya sheria ipo kwa nini hamfanyi cha kuzuia hii kulipwa,tuachane na malumbano ya kisiasa au kutafuta umaarufu kwenye jambo.KAMA KUZUIA MALIPO MAHAKAMANI KUNA WEZEKANA BASI FANYENI HARAKA

    ReplyDelete
  2. Huyu Bomani ni mtu wa ajabu sana. Ina maana duniani hakuna mitambo ya umeme hadi tusubiri mitambo ya Dowans kama siyo kuendeleza ufisadi!!

    ReplyDelete
  3. Deni la Dowans bado lina utata.

    Tukitazama kisheria tutazungumza kama Jaji Bomani lakini kijamii na kisiasa tutazungumza kama wadau wengine ambao pia wanaongozwa na uchungu wa ukali wa maisha na mfumuko wa bei, mfano Umeme wenyewe, gas nk!

    Mimi nashauri kama ipo mianya ya kisheria ambayo tunaweza kuitumia tusilipe deni hilo bila kuathiri uchumi wetu basi na tufanye hivyo, lakini kama mianya hiyo haipo nawaomba sana Watanzania tulipe deni hilo ili tuepuke Interest rate tuliyowekewa ya Asilimia 7!

    Natambuwa kuna maswali mengi kuliko majibu kwa nini tulipe haraka, kulipa huku haraka haina maana Bunge lisijadili suala hili na kuafiki. Kama kuna wanasheria kama wanahakika na loop holes za kisheria kuondokana na tatizo hili watusaidie kuondokana na zigo hili ambao watanzania tunakaribia kubebeshwa kutokana na kutokuwa na dhamira safi kutoka kwa viongozi waliotufikisha hapa.

    Lissu, Baregu, Marando nk mtusaidie si kama mnavyofanya sasa! kuzungumza Magazetini hakutasaidia kufikia suluhu ya jambo hili bali tulitie vitendeno maneno yenu.

    Mimi kwa upeo wangu mdogo wa kisheria jambo hili naona ipo baadhi ya mianya kisheria juu ya usuluhisi wa jambo hili kama vile tunavyoambiwa, ipo harufu ya rushwa ndani ya mikataba hii lakini hukumu imetoka kuwa tulipe! Mmoja kakwepa na kakimbia kamkabidhi DOWANS lakini bado tunaambiwa tulipe kwa mtu tusiyeingia naye mkataba huu!

    Lakini kwa upande mwingine Mikataba ni mikataba tu hata uwe mbaya au mzuri kiasi gani. unapovunja mkataba zipo gharama zake ikiwa ni pamoja na kulipa! Sasa sisi viongozi wetu wametuingizia RICHMOND, kampuni ya Kitapeli, na sote tunakiri hivyo, na tapeli huyo baada ya kuona mambo magumu hata kupelekea Waziri Mkuu LOWASA kujiuzulu naye akakimbia na kumkabidhi DOWANS! Sheria inasemaje, tunamlpia DOWANS au RICHMOND?

    Watanzania wanataka kujuwa mambo haya pamoja Mshirika wa makampuni hayo ambaye ni mtanzania kama sheria ya uwekezaji inavyoelekeza kwamba kama mtu au kampuni kutoka nje ya nchi inakuja kuwekeza nchini basi ni lazima iwe na mwenyeji wake hapa nchi ambaye atachukuwa hisa ya asilimia 25 ya mtaji! Ni nani Mtanzania huyu?!

    Maswali yote haya lazima yajibiwe, na Bunge lazima liyajadili kwa kina na uwazi mambo yote haya na hatimaye turidhie juu ya hatari ya kulipa ama kutokulipa deni hili!

    Watanzania kama watajibiwa maswali yao haya kiufasaha wataondokana na dhana inayotawala sasa hivi kuwa Fedha hizi zinakwenda kwa Rostam, Lowasa na Jk kufidia gharama zao za kampeni ya Uchaguzi mkuu 2010!

    Hebu tuondowe dhana hizi kuweka uwazi zaidi mchakato huu lakini la zaidi tuangalie baada ya kulipa nini kifuate kwa wale wote waliohusika kutufikisha hapa!

    Ni wazi kuwa Watanzania wanahitaji mkono wa sheria ufanye kazi juu yao kwa kuchezea na kupindisha sheria juu ya upatikanaji wa zabuni ya kufua umeme iliyopewa kampuni ya kitapeli, isiyo na sifa ya kufua umeme ya RICHMOND!

    Matokeo yake watu wamejiuzulu lakini hakuna hatua ya kisheria iliyochukuliwa juu yao leo Watanzania tunasubiri kubebeshwa zigo la DOWANS kama mwenda wazimu anayebebeshwa zigo la makopo azunguke nayo mitaani asijuwe mwisho wake na kesho atabebeshwa zigo gani. Huku wahusika wakiendelea kuwa watu MUHIMU kwa Serikali!

    Lazima ifikie wakati tuseme sasa NO! Enough is enough!

    By Carwin

    ReplyDelete
  4. Karamagi aliridhia mkataba wa Richmond uhamie Dowans akiwa nchi za nje. Hakusubiri hata kurudi. Maana aliambiwa na mtandao wao kwamba mambo huku magumu. Wapi na wapi Costa Rica na Bongoland. Biashara ingine yao ni ipi hao C. Rica? Nchi hii imechaguliwa kwa sababu ya masharti yao ya Kiuwekezaji kujaribu kufukia hii issue. Town mission kwa wa TZ wa leo noma. KUWENI WAJASIRI TU SEMENI TULIKOSEA HAPA TUKALA CHONDE TUSAMEHENI. WABONGO NI WATU WAZURI WACHA MUNGU WAIMBA KWAYA WATAWASAMEHE TUENDELEE NA KAZI YA KUJENGA TAIFA

    ReplyDelete
  5. Naungana na waliotoa maoni hapo juu kuwa hili swala sasa lisizungumwe kisiasa. Wale wanaopinga kulipwa deni hili watwambie ili sisi tusioelewa sheria ni kwanini hatutakiwi kulipa. Nina uhakika wale wanaopinga wanajua kilichokwenye hukumu hiyo wayaorodheshe ili kutuelimisha sisi wananchi wa kawaida. La sivyo utakuwa ni mchezo wa kuchonganisha viongozi na wananchi na itafikia mahala hii haitawalika. Ngeleja alishatoa maelezo ya Dawons ni ya nani akawataja wenyenayo. Sasa wanaosema Dawons in ya Rostam, JK, Lowassa, nk watoe ushahidi na kama ikithibitika ndipo nguvu ya umma ichukuwe mkondo wake. Nyie wasomi mnaosema vitu hivi kama hamna uhakika mnatumia hisia tu, basi nyie ni watu wa kuogopwa kama ukoma lakini kama mnayosema yana uhakika kuweni wajasiri tupe ushahidi wenu. Kama Dawns in ya JK nk naungana kusema hili deni lisilipwe. Lakini nasema kama Dawns ni ya JK tanesco wangekuwa na ubavu wa kuvunja mkataba? Wanasiasa na wasomi twambie ukweli. Tanzania ya leo hakuna kitu kilichofichika.

    ReplyDelete
  6. Mafisadi wana mtandao mrefu sana na mpana unaoweza kumkamata yeyote anayeweza kusaidia maslahi yake awe waziri, mwanasheria, polisi, viongozi wa dini, wanasiasa au yeyote anayeweza kulainisha upatikanaji na ulindaji wa maslahi yao. Wana pesa na vyombo vya habari vinavyosaidia ulindaji wa maslahi yao. Dawa ni moja tu! nguvu ya umma itumike, maana hali ilivyo sasa hakuna mtu wala taasisi yoyote inayoweza kukwepa mitego ya mafisadi nchini isipokuwa nguvu ya umma tu. Wananchi tuolozeshe mafisadi wote na mali zao, maana jamii tunawafahamu wote na mali zao zilipo na njia wanazotumia kutuyumbisha kama taifa. Tujichukulie hatua mikononi kuikomboa nchi hii, kama vile amini alivyofanya kule Uganda.

    ReplyDelete
  7. Wewe upatu saidi ujui unachosema. Jamani tutumie mtandao huu kutoa maoni yenye akili.

    ReplyDelete
  8. kuna watu wanatoa maoni yao hapo juu wanatukera sana,hivi wewe unataka ueleweshwe nini wakati unatambua kuwa dowans ni mikataba ya udanganyofu,leo tunapinga mtu mwingine anaibuka na kusema sisi tunaopinga tutoe ufafanuzi? hivi hili nalo linahitaji uwe umekwenda shule? wanajiofanya hawalifaham wanatupumbaza na maneno maneno

    ReplyDelete
  9. WATANZANIA TUHAMUE MOJA TU KAMA WALIVYOFANYA WEZETU KULE TUNISA... KILA KINACHO ONGELEWA HAPA KUHUSU RICHMOND/DOWANS KWA NJIA MOJA AU NYIGINE NI KUTUPUMBAZA TU. KAMA SERIKALI IMEHAMUA KUTUZUNGUSHA MBUYU BASI WANANCHI TUZUNGUKE UPANDE WA PILI TUKUTANE KATI TUJUE MKWELI NI NANI.... NI NGUMU NA UMWAGAJI DAMU UNAWEZA KUTOKEA LAKINI NI KWA NIA NJEMA KWA WANANCHI WALIO WENGI, UJASIRI ULIOTIMIKA KULE ARUSHA NA ZAIDI KWA WENZETU WA TUNISIA NDIO NJIA PEKEE. NAOMBA ISIELEWEKE NACHOCHEA VITA WATANZANIA TUMEBURUZWA KWA MUDA MREFU NJIA YA MOTO MOTO.

    ReplyDelete
  10. Watu wengine ni wehu hawajui wanalosema. Hii yote in elimu ndogo ya watanzania walio wengi Tunisia. Tunisia wana historia ambayo imewafikisha hapo. Watanzania jamani huko bado hatujafika. Nguvu ya umma inatumika as last resolt na sidhani kama viongozi wetu wameshatufikisha hapo. Viongozi wetu wa juu kama rais na waziri mkuu ni watu wanaosikia na wako tayari kubadilika. Sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kubadilisha katiba tuweke nguvu zetu huko tuhakikishe tunakuwa na katiba yenye usawa na kujenga mazingira ya kuwaletea maendeleo watanzania. Watu wengine msianze kuropoka mambo ambayo hamyajui. Yaliyotokea Iraq, Afganstan, DRC Congo, hata Tunisia yawe ni fundisho kuwa mabadiliko ya mtutu wa bunduki huwa yanachukuwa muda mrefu kufikia kile kilichokusudiwa, na sidhani kama watanzania tumeshafika huko. Viongozi wetu wanashaurika na kusikiliza. Narudia hatujafika huko. Tukifika huko nitakuwa tayari kuingia mitaani. Nyinyi watu wa chadema mnapoingia mitaani na kufanya fujo, kumbuka bado wapo wafuasi wa vyama vingine ambao hubaki nyumbani, nao wakitokea mitaa haitakalika. Kikwete bado ana wafuasi wengi kwa sasa kuliko mwanasiasa yoyote yule. Hivyo chungeni kauli zenu mnapoongelea nguvu ya umma. UMMA, YAANI WATANZANIA WALIO WENGI HAWAPO NYUMA YENU. MSIJIDANGANYE. Njia sahihi kwa sasa hivi katika Tanzania kuelekea mabadiliko ni kutumia mazungumzo kwa matabaka yote.

    ReplyDelete
  11. Kwani tatizo liko wapi,huyo Profesa Baregu siasa imemtia wehu,hivi huko ulaya uliwahi kusikia profesa ni mwanasiasa basi kama wapo ni mmoja katika million hivyo kuonyesha hamna tija kwenye fani hiyo,angesema mtu wa chama kingine angeambiwa uzee unampeleka pabaya,wewe upo kwenye hazina ya wasomi,basi jipangeni mkapinge hilo acheni kucheza na layman wasiojua sheria ili mpate umaarufu.SHERIA IPO NENDENI MAHAKAMANI MSIKAE MKASABABISHA WAZEE WA WATU WANATUKANWA BURE NA WAVUTA BANGI. MNAELEWA WAZI SHERIA ZILIVYO NA ZINAVYOKINZANA ZENYEWE KWA ZENYEWE. HII SIASA INATIA WATU WAZIMU MAANA HATA PENYE UKWELI MTU HUPINGA ILI KONDOO WAKE WAMSIFIE

    ReplyDelete