07 January 2011

CHADEMA yashinda umeya Mwanza

Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

BAADA ya malumbano ya muda mrefu kati ya vyama vitatu vya siasa kuhusiana na uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, hatimaye hali hiyo ilifikia kikomo jana baada ya madiwani wa
CHADEMA kuibuka washindi katika kinyang'anyiro hicho.

Vyama vyenye madiwani katika halmashauri hiyo ni CCM, CUF na CHADEMA ambavyo vikuwa na mvutano hadi kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa na kuwapo tishio la uvunjifu wa amani kutokana na madai ya ukiukwaji wa baadhi ya taratibu.

Lakini kinyume na matarajio ya wengi, jana uchaguiz ulifanyika kwa utulivu na Diwani wa Kata ya Nyakato, Bw. Josephat Manyerere (CHADEMA) kuibuka mshindi wa kiti cha meya baada ya kupata kura 17 na kumshinda Diwani wa Kata ya Mkolani, Bw. Stanslaus Mabula (CCM) ambaye alipata kura 15.

Katika uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya Mahina, Bw. Charles Chichibela  pia wa CHADEMA alichagulilwa kuwa Naibu Meya wa jiji hilo kwa kupata kura 17 na kumshinda diwani pekee wa CUF wa kuchaguliwa, Bw. Daud Mkama ambaye alipata kura 15.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Zitto Kabwe pamoja na wananchi kadhaa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo, Bw. Wilson Kabwe ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo, alilazimika kumtoa nje ya ukumbi huo Katibu wa CHADEMA mkoani Mwanza, Bw. Wilson Mshumbusi kwa madai ya kuwaandikia vimemo madiwani wa chama hicho wakati yeye akiwa ni mtazamaji.

Awali yalizuka malumbano makali ndani ya ukumbi huo katika ya madiwani wa CCM, CHADEMA na mkurugenzi wa halmashauri,  ambapo madiwani wa CHADEMA walitaka achaguliwe diwani mmoja kati yao kusimamia uchaguzi huo na kwamba mkurugenzi huyo abaki kuwa katibu.

Hali hiyo ilipingwa vikali na madiwani wa CCM pamoja na mkurugenzi mwenyewe, akidai kuwa kanuni za uchaguzi huo zinamtaka yeye kuongoza kikao hicho cha uchaguzi na kwamba vikao vya kawaida ndivyo vinatakiwa kuongozwa na meya au
naibu meya.

Hata hivyo, malumbano hayo yaliisha baada ya madiwani wa CHADEMA waliokuwa wakiongozwa na Mbunge wa Nyamagana, Bw. Ezekia Wenje pamoja na Mbunge wa Ilemela, Bw. Highness Kiwia kukubali mkurugenzi huyo kuongoza kikao hicho.

Eneo la halmashauri ya jiji hilo lilikuwa na ulinzi mkali wa askari wa Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU) ambao walivalia rasmi huku wakiwa na mbwa kwa ajili ya kudhibiti fujo zozote ambazo zingeweza kujitokeza, lakini hali ikawa ya utulivu.

Uchaguzi huo uliahirishwa Desemba 17 mwaka jana baada ya madiwani wa CHADEMA kukataa utaratibu wa kupiga kura za siri kwa kwenda pembeni kidogo katika sehemu maalumu iliyokuwa imeandaliwa katika ukumbi huo, kitendo walichosema kiliandaliwa ili kuwarubuni baadhi ya madiwani wake.

FFU kwa kushirikiana na askari wa jiji waliwapekuwa watu waliopita katika lango kuu la kuingia katika ofisi za halmashauri hiyo kwa lengo la kuimarisha usalama kutokana na kuwepo tishio la baadhi ya wananchi kufanya fujo katika uchaguzi huo.

Wakati huo huo, Bw. Zitto Kabwe alisema kuwa chama hicho hakitaki kusikia kwamba halmashauri zinazoongozwa na chama hicho zinanyooshewa kidole na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwamba zinajihusisha na ubadhirifu wa fedha za wananchi.

Alisema madiwani pamoja na watendaji katika halmashauri hizo watakaofanya ubadhirifu wa fedha za wananchi watachukuliwa hatua mara moja ili chama hicho kizidi kujenga imani kwa wananchi kwamba kipo kwa ajili ya maslahi ya umma.Bw. Kabwe aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, muda mfupi baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

"Natoa wito kuwa hatutaki kusikia vitendo vyovyote vya ubadhirifu katika halmashauri zetu ili wananchi waone jinsi ambavyo fedha zao zinastahili kusimamiwa kwa ajili ya maendeleo yao. hali hiyo pia itatoa mwanga jinsi ambavyo CHADEMA inaweza kusimimia mapato ya serikali kwa ujumla," alisema Bw. Zitto.

Akitolea mfano wa Mwanza, Bw. Zitto alisema kuwa mapato ya halmashauri ya jiji hilo ni makubwa kwa vile yanazidi bajeti ya zaidi ya wizara tano, na kwamba yakisimamiwa vizuri huduma za jamii katika jiji hilo zitakuwa bora na hivyo kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema kuwa chama hicho kitahakikisha kwamba jiji la Mwanza linashamiri na wananchi wanapata ajira ili kupunguza umaskini miongoni mwao, kwa vile kuna vyanzo vingi vya mapato pamoja na fursa nyingi za kiuchumi kutokana na jiografia yake.Kwa mujibu wa Bw. Zitto, jiji hilo ndilo kitovu cha nchi za maziwa makuu, hivyo ni vema rasilimali zilizopo hapo zikasimamiwa vizuri kwa ajili ya kuendeleza jiji hilo kwa maslahi ya wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

1 comment:

  1. Ninawapongezeni sana CHADEMA. Wananchi wanaIMANI kubwa na nyie, HIVYO MSIWAANGUSHE.

    WAONYESHENI WANACHI KWA VITENDO KWAMBA CHADEMA NI TEGEMEO LAO KWA MAENDELEO, HAINA UFISADI NA INAPIGA VITA UFISADI KWA VITENDO

    NA ZAIDI SANA

    CHADEMA NI CHAMA MBADALA WA CCM KUANZIA SASA

    ReplyDelete