07 January 2011

Serikali itailipa Dowans-Ngeleja

Na John Daniel
  
HATIMAYE serikali imetangaza rasmi kuwabebesha wananchi msalaba wa kuilipa Kampuni ya Dowans dola za Marekani milioni 65 karibu sawa na sh. bilioni 94 za Tanzania, huku ikikanusha sh. bilioni 185 zilizotajwa awali. Pia imeweka
wazi wamiliki wa Dowans na wakurugenzi wa kampuni hiyo huku ikionesha kuwa hakuna Mtanzania hata mmoja anayeoneshwa kwenye nyaraka za usajili kuwa anahusika nayo.

Akitangaza maamuzi ya serikali jana, Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja alisema uamuzi kuwa huo umefikiwa baada ya ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na wanasheria waliokilisha TANESCO katika usuluhishi wa mgogoro huo mahakamani, Kampuni ya Rex Attorneys.

"Kutokana na ushauri uliotolea na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wanasheria wa TANESCO kwamba kupinga tozo/uamuzi huo hakutafanikisha azma yoyote isipokuwa kuchelewa kwa utekelezaji.

Serikali haina budi kutekeleza uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo na kuepuka gharama zaidi ikiwa maamuzi ya ICC yatapuuzwa," alisema Bw. Ngeleja na kuongeza "Katika mgogoro wa kwanza TANESCO wanatakiwa kulipa fidia kwa Dowans Holding SA (Costa Rica) na Dowans Tanzania Limited jumla ya dola za Marekani 65,812,630 badala ya dola milioni 149 zilizokuwa zinadaiwa na Dowans," alisema.

Alisema kabla ya uamuzi huo Bw. Werema alipitia hukumu hiyo pamoja na sheria zinazotumika kuendesha ushauri huo na kuridhika kuwa hakuna sababu ya kukata rufaa.

Alisema Dowans iliwasilisha madai ya dola za Marekani milioni 149 na kwamba baada ya jopo la watatuzi wa migogoro kusikiliza ilihukumu TANESCO kulipa dola 65 karibu sawa na sh. bilioni 94 za Tanzania.

Alisema hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) unataja riba ya asilimia 7.5 endapo TANESCO itachelewa kulipa.

Waziri Ngeleja alikanusha taarifa zilizotolewa awali na baadhi ya vyombo vya habari (si Majira) kuwa fidia hiyo ilikuwa ni dola milioni 149 sawa na sh. bilionbi 185 na kusisitiza kuwa taarifa hizo zilikuwa za uongo.

Kuhusu mgogoro wa pili alisema TANESCO iliamuriwa kuilipa Kampuni ya Richmond dola za Marekani 50,000 kwa kuikashifu badala ya dola milioni 169 iliyodaiwa na kampuni hiyo.

Alisema baada ya maamuzi hayo kutolewa na ICC Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO ilishauriwa na wanasheria waliyokuwa wakiitetea Kampuni ya Rex Attorneys Advocates kukubaliana na hukumu hiyo bila kuipinga.

Hata hivyo, Waziri Ngeleja alisisitiza kuwa licha ya serikali kukubali kutekeleza hukumu hiyo haitalipa fedha hizo kama hukumu hiyo haitasajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania. Wamiliki wa Dowans "Kwa mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA) wamiliki/wanahisa wa Dowans Tanzania Limited ni wafuatao:"Dowans Holding S.A (hisa 81) na Portek Systems and Equipment PTE Limited ya Singapore (hisa 54).

Wakurugenzi wa Dowand Tanzania Limited ni Andrew James Tice (Mcanada), Gopalakrishnan Blachandran (Mhindi), Hon Sung Woo (msingapore), Guy Arthur Picard (Mcanada), Suleiman Mohamed Yahya Al Adawi (Raia wa Oman) na Stanley Munai (Mkenya)," alisema Bw. Ngaleja.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Bw. Ngeleja alikanusha sheria zilizopo kuilazimu kila kampuni kutoka nje kuwa na mwanahisa mzalendo na kusisitiza kuwa Dowans haina mmiliki Mtanzania.

"Si kweli kwamba sheria inalazimu kila kampuni kutoka nje kuwa na mwanahisa mzalendo, na katika kampuni hii ya Dowans hakukuwa na Mtanzania, hiyo sheria ipo kwa baadhi tu ya biashara si zote," alisema Bw. Ngeleja.Kuhusu taarifa za wamiliki wa Dowans kukwepa kusajili hukumu hiyo Mahakama Kuu ya Tanzania Waziri Ngeleja alisema:

"Kama hao wamiliki walienda Wizara ya Fedha huenda walipeleka kadi za salamu za mwaka mpya au kusalimia marafiki zao, haiwezekani wakapeleka madai kabla ya kuandikisha hukumu yenyewe Mahakama Kuu," alisisitiza.

Alipoulizwa uhalali wa kodi za Watazania kutumika kulipa fidia kwa kampuni hewa kama ilivyobainishwa na Kamati Teule ya Bunge iliyosababisha Richmond kufunga virago alisema hawezi kuzungumzia masuala ya Bunge kwa kuwa yalishafungwa."Nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa kisheria, kilichopo hapa ni hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ambayo sisi tunaiheshimu, hata sisi tumewahi kushinda madai yetu kama vile kesi ya City Water mbona hatukuhoji hivi," alisema Bw. Ngaleja.

8 comments:

  1. Hili ni changa la macho kwa Wadanganyika

    ReplyDelete
  2. Sikilizeni nyinyi watanzania. Lipeni deni hili mara moja halafu mijipange upya munaposaini mikataba.

    Hapa mushafyekwa!

    Na mukithubutu kukaidi, riba (kuanzia) ya shs laki 9 kwa saa inawasubiri kwa masaa yote mutayochelewesha!

    ReplyDelete
  3. Wakati mahakama ilipoamuru pawepo mgombea binafsi, serikali ilikata rufaa mara moja, lakini hukumu hii ya kuwalipa Dowans, kampuni ya wapambe wa CCM, hakuna kukata rufaa. Kinachosemwa ni kuwalipa mara moja! Makubwa haya

    ReplyDelete
  4. Waziri kweli umejipanga katika kuwaweka sawa wanahabari.Chakufurahisha ni kwamba mpaka majina mmeweza kuyaazima kutoka kwa washikaji zetu.Kampuni ya simu za simu za mikono zinapo funguliwa hata mawaziri huwa wanahudhuria,lakni kwa hii ya Dowans hata hao wabia hawajawahi kuonyesha sura zao siku ya ufunguzi(kukabidhiwa) mitambo ya richmond.

    Kweli tujipange tena,bado mengi yatakuja na hivi mmejiroga kumtia ndani Slaa.

    ReplyDelete
  5. Unajua, vile viongozi wa serikali wanavokula mali uma, basi sasa hapa wamepatikana!!!!

    Nakuhakikishia hata hao viongozi wetu INAWAUMA sana pesa hii yote iteke nchini kwenda kwa kasharika tu......

    Funzo kubwa Tanzania: Munapoona Raha Kula mali ya rushwa na kuwazulumu wenzenu Maulmivu yanakurudieni kwa njia yeyote ile. Ni Hakika kabisa, Vigogo vinatoka jasho hapa!!!! Wanatoka jasho shenzi!!

    Utawachezea raia wa kawaida, ila kuna wenye akili kuliko nyinyi vigogo. Wamejua vipi kuwavua mikanda ya viuno mwaka huu.

    Nyie wengine mupo hapa mumetumwa tu na vigogo kuchemsha siasa na vukuto - ili wapate wasaidizi kwenye kilio chao na wapate kukwepa malipo. Waacheni walie na wao kama tunavolia sisi kila siku.

    Shenzi!! Lipeni sasa! Tunakufa sote, sio sisi tu. Inawauma sana, japo na sisi tunaumia.

    Nyamazeni mulotumwa!! Shambi wametenda wao, wanaka watu walie nao.

    ReplyDelete
  6. Utapeli Tanzania ni sawa na hewa ya Oxygen. Watanzania wengi ni matapeli pia! kwa vile utapeli umeshawaenea katika mishipa yenu ya damu, sasa munakula mulichokipanda.

    Jasho na dhuluma za wale mulowatapeli, sasa zinakausha rasilimali zenu. Kilio chao BWANA MUNGU amekipokea na SASA anawadhibu ili mupate kusafisha safu zenu katika maisha

    ReplyDelete
  7. hiyo ndiyo shida ya kukosa uzalendo na nchi yako.mpaka lini wasomo watanzania mtaanza kuipenda nchi yenu ili muwapunguzie wananchi waliowaamini matatizo?ikiwa mlisomeshwa ili muwe waelevu,ni vipi mnaendelea kuwa mbumbumbu?mtaendelea kudharauliwa na mataifa makubwa,kwani mnakubali upuuzi ambao wenzenu hawawezi kuukubali.

    ReplyDelete
  8. rostam ukilipwa tu tafuta nchi ya kuishi mshatufanya mabwege sana ndani ya nchi yetu.Nyerere angekua hai Rostam ungetafuta pakutokea kwenda kwenu Iran.

    ReplyDelete