Na Elizabeth Mayemba
KLABU ya soka ya Yanga inatafuta sh.bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda na jengo la Mtaa wa Mafia, Kariakoo Dar es Salaam.Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema
wamepanga kujenga uwanja mkubwa wa kisasa na jengo lao la Mafia ambalo litakuwa la ghorofa 10.
"Mambo yanakwenda vizuri, na Kamati ya miradi iliyochaguliwa chini ya Mwenyekiti wake Mbaraka Igangula, inafanya vizuri kazi hilo, hivyo kila kitu kitakwenda sawa," alisema.
Alisema Kampuni ya Ujenzi ya NEDCO, ndiyo iliyopata tenda ya kusimamia ujenzi wa uwanja na jengo, ambapo wameanza kwa kuchora ramani ya uwanja.
Sendeu alisema klabu hiyo imebuni mbinu ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo watakuwa wakiandaa chakula cha jioni na kualika watu mbalimbali kwa lengo la kuomba michango.
Msemaji huyo alisema mchezaji wao Shamte Ally, anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa matibabu wiki mbili zilizopita, na ameanza kufanya mazoezi mepesi ya kutembea mwenyewe.
Alisema mwanzo alikuwa akitembelea magongo, lakini sasa anaweza kutembea mwenyewe na Januari 8, mwakani atamtoa bandeji ngumu (POP).
Wakati huo huo, uongozi huo umesema kwamba, mazungumzo kati yao na klabu ya Tang Long ya Vietnam inayomhitaji kiungo wao Abdi Kassim 'Babi', yanaendelea vizuri.
Sendeu alisema klabu hiyo imeomba imnunue mchezaji huyo kwa dola 35,000 za Marekani, lakini uongozi wa Yanga umetaka walipwe dola 40,000.
"Hata hivyo, tutafikia muafaka na kumruhusu akacheze huko, na tutampa baraka zote kama viongozi," alisema.
No comments:
Post a Comment