31 December 2010

Mahakama ya Rufaa yakataa kubatilisha uamuzi

Na Grace Michael

MAHAKAMA ya Rufaa nchini imekataa kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu na kutoa dhamana kwa washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uvuvi katika Bahari ya Hindi eneo la Tanzania na badala yake imeamuru kurejeshwa kwa ombi hilo
Mahakama Kuu.Akisoma uamuzi uliofikiwa na Jopo la Majaji watatu ambalo liliongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Bw. John Mgeta alisema kuwa majaji hao wameamuru ombi hilo la dhamana lisikilizwe haraka iwezekanavyo na Mahakama Kuu kwa kuwa dhamana ni haki ya kila mshtakiwa.

Jopo hilo liliamua hayo baada ya kubaini uamuzi uliokuwa umetolewa awali na Mahakama Kuu ambao uliweka masharti magumu ya dhamana, ambayo yalipingwa na walalamikiwa, yamepitwa na wakati.

Kupitwa na wakati kwa masharti hayo inatokana na hatua ya Upande wa Mashtaka kubadili hati ya mashtaka wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Razia Sheikh ambapo mabadiliko hayo hayakuonesha kiasi chochote cha fedha.

Mashtaka ya awali ya washtakiwa hao, yalionesha kuwa thamani ya samaki waliokamatwa ilikuwa ni zaidi ya sh. bilioni 2, hivyo washtakiwa hao walitakiwa kila mmoja kuweka nusu ya gharama hiyo mahakamani, hatua iliyowafanya wakate rufaa kutokana na masharti kuwa magumu.

Uamuzi huo ulisema kuwa pamoja na mabadiliko hayo, hakuna upande wowote katika kesi hiyo ulioifahamisha mahakama juu ya mabadiliko hayo, hivyo Jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa likasema haliwezi kufanya kazi ambayo inatakiwa kufanywa na Mahakama Kuu ya kuangalia dhamana za washtakiwa baada ya mabadiliko hayo.

Awali, wakati rufani hiyo ikisikilizwa, upande wa Mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Stanslaus Boniface ulimwomba Jaji Mkuu Mstaafu kujitoa kusikiliza rufaa hiyo kwa kuwa tayari alikuwa amenukuliwa na vyombo vya habari akitoa msimamo wake juu ya kesi hiyo.

Katika msimamo huo, ilidaiwa kuwa Jaji Ramadhan aliweka bayana kuwa washtakiwa hao hawakustahili kushtakiwa wote, hivyo, upande huo uliomba ajitoe kwa kuwa asingetenda haki kwa upande mmoja.Katika hoja hiyo, upande wa washtakiwa uliokuwa ukiongozwa na wakili Bw. John Mapinduzi uliomba mahakama kuendelea kusikiliza rufani hiyo kwa kuwa upande wa mashtaka hawakuwa na hoja ya msingi na katika rufani hiyo hakuwa jaji mmoja peke yake. 

Hata hivyo, Jaji Ramadhan aligoma kujitoa na kuendelea kusikiliza rufani hiyo ambayo kwa msimamo wa pamoja wameamuru kurejeshwa kwa maombi hayo ya dhamana Mahakama Kuu ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment