31 December 2010

Waziri Nahodha aikuna BASATA

Na Addolph Bruno

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limeguswa na kauli ya Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mheshiwa Shamsi Vuai Nahodha ya kuzitaka idara za Serikali kutumia sanaa katika kutoa elimu kwa Umma.Akizungumza Ofisini kwake jana
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema, kauli hiyo inaonyesha wazi kwamba Waziri Nahodha anatambua umuhimu wa sanaa katika kufikisha ujumbe kwa jamii na kwamba BASATA inamuunga mkono na kumpongeza sana kwa kuwa na mtazamo huo chanya kuhusu sanaa.

Waziri Nahodha hivi karibuni, alitoa agizo kwa idara za serikali kutumia sanaa kama njia ya kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi ili ujumbe uweze kuwafiki wananchi wengi hasa kwa kuwa wananchi wanapenda sana kuangalia vipindi vya sanaa kuliko vipindi vingine.

Kwa kauli hiyo ya Nahodha Ghonche amesema inayofaa kuungwa mkono si kwa sababu amezungumzia masuala ya sanaa bali ni kwa sababu ameona umuhimu wa kutumia mbinu inayokubalika  na kuaminiwa katika katika kufikisha ujumbe.

"Sanaa ni chombo chenye nguvu katika kufikisha ujumbe na inafahamika hivyo, sisi kama wadau wa masuala ya sanaa tunamshukuru Waziri Nahodha kwa kuliona hilo na kutoa wito kwa idara za Wizara yake kutumia sanaa katika kuwaelimisha wananchi juu ya masuala mbalimbali, kwa kweli tumefarijika sana kuona mtu ambaye si mwana sanaa anatambua hilo na kulisema hadharani," alisema Ghonche.

Amesema pamoja na kauli hiyo ya Waziri Nahodha ni vyema idara na asasi zingine zinazotaka kutumia sanaa katika kuelimisha jamii zikawatumia wasanii waliosajiliwa na BASATA na wenye vibali badala ya kutumia tu wasanii wasiotambuliwa.

"Katika kutekeleza hili ni vyema wakatumika wasanii ambao wamesajiliwa na wanatumbuliwa na BASATA ili kuepusha ubabaishaji," alisema Ghonche.

No comments:

Post a Comment