30 December 2010

Warundi 200 warudi nyumbani

Na Prosper Kwigize, Kigoma

WAKIMBIZI 200 wa Burundi waliokuwa wakiishi katika Kambi  ya Mtabila, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wamerejeshwa nchini mwao baada ya kuhamasishwa na kupewa vitu mbalimbali ikiwemo fedha tasilimu, vyombo vya ndani na
baiskeli kwa kila familia.

Msafara wa wakimbizi hao ambao waliishi Tanzania kwa takribani miaka 17 uliondoka juzi kutokana na mpango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi kusitisha utoaji wa fedha na samani nyingine baada ya mwezi huu.

Kwa mujibu wa UNHCR, wakimbizi wote wanao hiyari kurejea nchini mwao, kila mmoja anapewa fedha taslimu sh. 130,000 lengo likiwa ni kuwawezesha kuanza vema maisha yao nchini Burundi.

UNHCR kwa kushirikiana na mashirika mengine yaliyoko Burundi inatoa mabati 20 kwa kila mkimbizi kwa ajili ya kujenga nyumba, chakula cha kutosha miezi sita ya mwanzo baada ya kurejea pamoja na matibabu bure kwa kipindi cha miezi sita.

Wakizungumza na Majira katika kambi hiyo, wakimbizi hao walisema kuwa, kuamua kwao kurudi Burundi ni kutokana na kupata taarifa za uhakika kuwa sasa nchi yao ina amani ya kutosha na kwamba waliotangulia wanaishi kwa amani.

Kwa upande wake, Bw. Hakizimana Daniel ambaye aliondoka Burundi tangu mwaka 1993 alilieleza Majira kuwa kuamua kwake kurejea Burundi ni kutokana na serikali ya Tanzania kufunga shule zote katika kambi yao na hivyo watoto kukosa masomo.

Nimeamua mwenyewe kurejea Burundi ili wanangu wapate fursa ya kusoma, maana hapa kambini serikali ya Tanzania pamoja na UNHCR walifunga shule tangu mwaka jana sasa watoto hawasomi, ninawaza watakuwa watu wa aina gani kama hawatapata elimu, wakati wenzao huko Burundi wako wanasoma,” alisema Bw. Daniel kabla ya kupanda gari kwenda Burundi.

Ofisa wa Idara ya Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, Bw. Fredrick Nisajire alisema kuwa mpango wa kuendelea kuwaacha wakimbizi wa Burundi kuamua kwa hiyari kurejea Burundi pamoja na kupewa hamasa ya fedha na samani mbalimbali unamalizika mwezi huu na kwamba kuanzaia January serikali itaamua lipi lifanyike kwa watakaokuwa wamekaidi kurejea kwa hiyari yao.

Bw. Nisajile alisisitiza kuwa, hadi sasa kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Mtabila ina zaidi ya wakimbizi 30,000 na kwamba licha ya misaada mingi kuongezwa kwa wanaorejea bado inaonekana wakimbizi hao wamegomea hatua hiyo, licha ya Burundi kuwa na amani ya kutosha na utayari wa kuwapokea.

Mkuu wa UNHCR wilayani Kasulu, Bw. Kazuhiro Kaneko amebainisha kuwa, msafara wa mwisho wa Warundi kurudi kwao kwa hiyari utafanyika Ijumaa na baada ya hapo shirika hilo halitatoa tena ufadhili wowote kwa wakimbizi hao hadi pande tatu, yaani Tanzania, Burundi na UNHCR zitakapotoa uamuzi mbadala.

Wakimbizi wa Burundi walikimbia na kuishi Tanzania tangu mwaka 1993 mara tu serikali ya Merikiory Ndadaye kuangushwa na yeye mwenyewe kuuawa na majeshi waasi na zaidi ya Warundi 500,000 walikimbilia Tanzania katika mikoa ya Kigoma na Kagera.

Kwa sasa mkoa wa Kigoma una wakimbizi 100,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanaoishi katika kambi mbili za Nyarugusuna Mtabila.

No comments:

Post a Comment