Na Peter Mwenda
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Bw. Shamsi Vuai Nahodha ameliagiza Jeshi la Polisi kuendeleza mpango wa kuzawadia na kutunuku maofisa na askari waliotekeleza majukumu yao kwa umakini na uadilifu.Akizungumza wakati wa gwaride la
kutunuku sifa na zawadi kwa Jeshi la Polisi jana, Bw. Nahodha alisema utaratibu wa kutoa zawadi utaongeza motisha, ari na moyo wa kujituma kwa waliopata zawadi hizo kuongeza tija.
"Wataalamu wa menejimenti wanasema mfanyakazi anapopewa tuzo huongeza tija na ufanisi kazini, lakini mfanyakazi huyo anapofanya vibaya hapana budi pia apewe adhabu ili abadili tabia," alisema Bw. Nahodha.
Alisema utaratibu huo utaleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa Jeshi la Polisi, na kuahidi kutekeleza mambo yote yenye lengo la kuimarisha utendaji kazi.
Awali, wakati akitunuku tuzo kwa askari waliofanya vizuri kwa kukataa kupokea rushwa, kupambana na majambazi wa kutumia silaha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2010, Bw. Nahodha alilitaka jeshi hilo kuwa wabunifu na wachapa kazi.
Pia aliwataka wananchi kuchangie na kushirikiana na Jeshi la Polisi kuleta amani ambayo alisema ndiyo njia ya haraka ya kufikia maendeleo kufanana na nchi nyingine kama Dubai.
Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na Mkuu wa zamani Jeshi la Polisi, Bw. Omari Mahita, IGP wa sasa, Said Mwema alisema jeshi hilo limepokea maagizo ya waziri na kuahidi kuyafanyia kazi.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova alikabidhi baiskeli 100 zilizotolewa na Kampuni ya Home Shipping Centre zenye thamani ya sh. mil.25.
Kampuni nyingine iliyotoa mchango wake kwa jeshi hilo ni Benki ya Akiba ambayo ilitoa mchango wa sh. mil. 1 kwa ajili ya kuzawadia askari hao.
No comments:
Post a Comment