30 December 2010

Bundi bado airandia Yanga

Na Elizabeth Mayemba

BUNDI ameanza kuranda tena ndani ya klabu ya Yanga, baada ya kundi la wanachama wenye nguvu ndani ya klabu hiyo, kupanga kumwandikia barua Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga ili aachie ngazi.Hatua hiyo imekuja siku chache, baada ya
wachezaji wa klabu hiyo kuitisha mgomo ili walipwe fedha zao za usajili.

Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana ndani ya klabu hiyo, zinadai kuwa wanachama hao walisema Mwenyekiti huyo ameshindwa kuiongoza klabu hiyo, hivyo ni vyema akajiuzulu mwenyewe kwa maslahi ya klabu na wana-Yanga wote.

"Jana baadhi ya wanachama tulikuwa na kikao cha faragha na wote kwa kauli moja, tulipendekeza kumwandikia barua Nchunga ili atuachie Yanga yetu, tunaona wazi hawezi kuongoza," alisema mmoja wa wanachama hao.

Alisema haikuwahi kutokea hata siku moja wachezaji kugoma na mara nyingi walikuwa wakidai mishahara, ambapo viongozi walikuwa wakikaa na wachezaji kabla mambo hayajaharibika na kuwatuliza, lakini wanashanga kuona, Nchunga anasubiri wachezaji wagome ndiyo atafute suluhu.

Naye mwanachama mwingine ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini alisema, kwa kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lilipiga marufuku kufanya mapinduzi ya uongozi, wameona watumie busara kumwandikia barua Mwenyekiti huyo, ili ajiuzulu mwenyewe.

Alisema hawakupenda wafikie hatua hiyo, lakini wanaona kila siku mambo yanazidi kuharibika hivyo ni bora awaachie Yanga yao, waje viongozi ambao wataweza kuongoza.

Hata hivyo Nchunga alipopigiwa simu yake ya mkononi ili kujibu tuhuma za wanachama wake, simu yake iliita bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment