13 December 2010

Wambura amrithi Kaijage TFF

Na Zahoro Mlanzi

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewateua Angetile Osiah kuwa Katibu Mkuu na Boniface Wambura kuwa Ofisa Habari wa shirikisho hilo.Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa shirikisho hilo, Leodeger Tenga, alisema
uteuzi huo umetokana na nafasi zilizoachwa wazi na aliyekuwa Katibu Mkuu, Fredrick Mwakalebela na Ofisa Habari, Florian Kaijage, ambapo mikataba yao ilimalizika tangu Julai, mwaka huu.

Alisema walipokea maombi 64 kwa nafasi ya ukatibu na 44 kwa nafasi ya ofisa habari, ambapo katika mchujo wa awali uliofanywa na Kampuni ya AMARON, 17 walipita kwa upande wa ukatibu na 11 kwa uofisa habari.

"Kamati hiyo ilikutana jana (juzi) katika kikao maalumu na kuteua majina hayo pamoja kumteua Jimmy Kabwe kuwa Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, kwani wanaamini Kabwe ataiweza nafasi hiyo katika masuala ya uhamasishaji na kufuatilia wadhamini," alisema Tenga.

Akimzungumzia Osiah, alisema ana Shahada ya Sayansi ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amehudhuria kozi nyingi katika taaluma yake ya uandishi wa habari, ni Mhariri wa Habari wa magazeti ya Mwananchi.

Kwa upande wa Wambura, alisema ni msomi wa Shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, na Stashahada ya Tasnia ya Habari, amehudhuria kozi mbalimbali za uandishi wa habari na pia ni Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo.Aliongeza, viongozi hao walioteuliwa wataanza kazi baada ya kumalizia majukumu yao katika kampuni wanazotoka kwa kuweka mambo sawa.

No comments:

Post a Comment