Na Nickson Mkilanya, Morogoro,
MABINGWA wa soka wa zamani wa Mkoa wa Morogoro, timu ya kiwanda cha kusindika tumbaku cha Alliance One Morogoro, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa soka Ligi ya Taifa Wilaya ya Morogoro vijijini.Katibu wa Chama cha Mpira Wilaya ya
Morogoro vijijini, Charles Kajilu, amesema timu ya Alliance One imefanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kujikusanyia pointi tisa na kuzibwaga timu nyingine nne.
Kajilu alisema katika ligi hiyo iliyokuwa ikichezwa kituo cha Kinole, Morogoro vijijini, Tumbaku Morogoro imeshika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi tisa sawa na Alliance, lakini ilizidiwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mshindi wa tatu katika ligi hiyo ni wenyeji wa kituo hicho, Yetu Afrika ya Kinol iliyopata pointi sita.
Kwa mujibu wa katibu huyo, timu tatu zitacheza fainali za Ligi ya Taifa Mkoa wa Morogoro.Kwa upande wa Manispaa ya Morogoro, Kaizer Chief FC inaongoza hatua ya fainali ya Ligi ya Taifa Wilaya ya Morogoro Mjini, baada ya kujikusanyia pointi nne.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Morogoro Mjini, Jimmy Lengwe, alisema Kaizer Chief inaongoza baada ya kuichapa timu ya Mzinga United mabao 2-1.
Dundee FC inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi tatu sawa na Kaizer Chief baada ya kuifunga Moro Kids bao 1-0.
No comments:
Post a Comment