13 December 2010

Rahaaa, utamu

*Kili kidedea Chalenji

Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', jana imetwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji 2010,  baada ya kuichapa Ivory Coast bao 1-0, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Bao pekee lililoipa ubingwa Kili Stars,  lilifungwa na
nahodha Shadrack Nsajigwa dakika ya 40, kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki wa Ivory Coast N'goran Kouasi, kushika mpira ndani ya eneo la hatari, akiwa katika harakati za kuokoa shuti lililopigwa na Salum Machaku.

Kwa kutwaa ubingwa huo, Kili Stars ilikabidhiwa mfano wa hundi ya dola 30,000 na kikombe, huku Ivory Coast wakipewa mfano wa hundi ya dola 20,000, mabingwa waliopita Uganda 'The cranes', ilipata dola 10,000, baada ya kuifunga Ethiopia mabao 4-3.

Mbali na zawadi hizo, kipa wa Kili Stars, Juma Kaseja aliibuka kipa bora,  na Nsajigwa aliibuka mchezaji bora huku mshambuliaji wa Zambia, Felix Sunzu, akiibuka kinara wa kupachika mabao kwa kufunga mabao matano.Katika mchezo huo wa jana, Kili Stars ilianza kucheza soka la taratibu huku ikionekana kuwasoma wapinzani wao,  lakini dakika ya nane, Ivory Coast ilifanya shambulizi la kushtukiza,  baada ya Dion Marc kupiga shuti lililodakwa na Kaseja.

Wakati mchezo huo ukiendelea, Kili Stars ilipata pigo dakika ya 11, baada ya Idrissa Rajab kutolewa nje baada ya kuumizwa vibaya na Kone Mahamoud, na nafasi yake kuchukuliwa na Kigi Makasi.

Dakika ya 17, Jabir Aziz wa Kili Stars alipiga shuti nje ya eneo la hatari,  lakini lilipanguliwa na kuwa kona tasa. Kili Stars iliendeleza mashambulizi na dakika ya 40,  Nsajigwa aliwainua mashabiki kwa kufunga bao kwa mkwaju wa penalti.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Ivory Coast ikifanya mabadiliko, Mahamoudy alitoka na kuingia Kipre Tchetche na kufanya safu ya ushambuliaji ya Ivory kuimarika,  kwani walizidisha mashambulizi.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ambapo kwa nyakati tofauti Machaku ambaye alionekana mwiba kwa Ivory Coast, alipiga krosi zilizokosa wamaliziaji na nyingine kutoka nje ya goli.

Lakini, katika hali isiyotarajiwa,  shabiki mmoja ambaye hakuweza kufahamika jina lake mara moja,  aliingia uwanjani na kumpa jezi kipa Kaseja na baadaye maaskari walimtoa nje ya uwanja.

Katika mchezo wa kwanza wa kutafuta mshindi wa tatu, Uganda iliichapa Ethiopia mabao 4-3, mabao ya Uganda yalifungwa na Andrew Mwesiga dakika ya tano, Henry Kiseka dakika ya 48, Tonny Maweje dakika ya 52 na la ushindi lilifungwa na Matovu Sula dakika ya 72.

Mabao ya Ethiopia yalifungwa na Omod Okwury dakika ya pili na kuongeza lingine dakika ya 33 na Tesfaye Alebachew alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tatu dakika ya 67.Katika hatua nyingine, Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), kitaandaa mechi maalum ya kuipongeza Kili Stars kwa kutwaa ubingwa, timu itakayocheza nayo, itatangazwa baadaye.

No comments:

Post a Comment