28 December 2010

Wajumbe WDC wamsusia diwani wa CHADEMA

Na Said Njuki, Arusha
 
WAJUMBE wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ya Elerai wamemkataa mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. John Bayo kwa sababu ni diwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Bw. Bayo ambaye pia ni
msemaji wa CHADEMA na Mwenyekiti wa Serikali wa Mtaa wa Ngurumo, alikumbwa na mkasa huo mwishoni mwa wiki, baada ya wajumbe hao kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kudai hawamtabui.

Walisema wamechukua hatua hiyo kwa sababu chama chake, CHADEMA, hakiwatambui Rais Jakaya Kikwete, Meya wa Jiji la Arusha, Bw. Gaudance Lyimo wala Naibu meya, Bw. Michael Kivuyo (TLP), hivyo na wao hawawezi kumtambua mwenyekiti huyo. 
 
Diwani wa Kata ndiye Mwenyekiti wa WDC bila kujali anatoka chama gani, na kwa kata ya Elerai, Bw. Bayo anatoka CHADEMA akiwa na wajumbe wa mitaa wawili tu kutoka chama chake, huku wengine 13 wakitoka CCM, hali inayotishia mustakabali wa mipango ya maendeleo katika kata hiyo na
zingine nane zenye madiwani kutoka CHADEMA kati ya kata 19
zinazounda jimbo hilo.
 
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Bw. Charles Sanai zimeeleza kuwa hali ya hewa ilianza kuchafuka mara baada ya mtendaji huyo kutambulisha wajumbe wa kikao hicho, kisha kusoma agenda za kikao akitaraji kumkaribisha mwenyekiti huyo kufungua kikao, ambapo mmoja wa wajumbe hao alinyanyua mkono na kutoa hoja hiyo ya kutomtambua diwani huyo kama mwenyekiti wa kikao.
 
“Mwenyekiti wa kikao ni diwani kutoka CHADEMA, chama ambacho hakikuhudhuria kikao cha kumtangaza mshindi wa kura za urais, ambapo Dkt. Jakaya Kikwete alitangazwa kuwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kuapishwa kwake na pia kususia hotuba yake bungeni. Mbaya zaidi kumkataa Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Bw. Lyimo na naibu wake  Bw. Kivuyo kutoka TLP, vipi leo tuongozwe na mwenyekiti kutoka CHADEMA?” alihoji mwenyekiti wa mtaa wa Chuma, Bw. Ramadhani Nyagawa.
 
Bw. Nyagawa aliongeza kudai kuwa baada ya uchaguzi sasa taifa linatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/15 hayo maazimio ya kikao atayafikisha katika halmashauri inayoongozwa na meya waliyemkataa au yule waliyemchagua wao, CHADEMA, ambaye ni Bw. Estomi Malla na kueleza kwamba hawako tayari kujadili chochote hadi viongozi wa CHADEMA watakapomtambua Rais Kikwete, Meya wa Jiji la Arusha na Naibu wake.
 
Mwenyekiti wa mtaa wa SACON, Bw. Losioki Laizer alieleza kuwa wanaheshimu maamuzi ya wananchi ya kupiga kura na kuchagua viongozi wao, lakini Mwenyekiti wa WDC wa Kata hiyo anayetokana na CHADEMA, ndiye msemaji mkuu wa madiwani wa jimbo hilo na ameshatangaza kwenda mahakamani kupinga meya na naibu wake hivyo wasingeweza kumruhusu aongoze kikao hicho muhimu.
 
Kukubali diwani huyu kuendesha kikao hiki ni kuwaunga mkono viongozi ambao bado hawajawatambua viongozi halali akiwemo Rais Kikwete, Meya na Naibu wake, hatutabadili msimamo wetu huu. Ni vizuri wakatambua WDC inaendeshwa kisheria na si kiushabiki, tunahitaji kufuata sheria hizo ikiwa ni pamoja na miradi yote iliyoibuliwa awali inaheshimiwa na si vinginevyo,” alionya Bw. Laizer.
 
Hoja hizo ziliungwa mkono na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mama Musa, Bw. Yasini Selemani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Tawi la Elerai Magharibi alimtaka mtendaji kukubaliana na hoja hizo akidai kuwa diwani huyo hata baada ya kuukwa udiwani alitishia kuwafuta baadhi ya  wenyeviti kutoka CCM katika kata yake akiwemo yeye (Yasini), jambo ambalo haliwezi kwani alichaguliwa na wananchi na si kiongozi moja.
 
Baada ya muvutano huo uliodumu takribani dakika 20, mtendaji huyo aliwataka wajumbe ambao hawawezi kuendelea na kikao hicho kutoka nje, ndipo wajumbe wote 13 wa CCM walipotoka na kuwaacha wawili wa CHADEMA ambao ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo, Bi. Sara Mrema na diwani huyo, hali iliyomlazimu mtendaji huyo kusitisha kikao. Mtendaji huyo alisema kuwa angetoa taarifa sehemu husika kwa mujibu wa sheria zilizopo na kwamba anachosubiri na maelekezo kutoka ngazi za juu.
 
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Arusha, Bw. Lyimo alipohojiwa alikiri kupata taarifa hizo na kueleza kuwa ni haki ya wajumbe hao kumsaidia mwenyekiti huyo licha ya kuwa anatoka chama pinzani kwani ni diwani halali na mwenyekiti wa WDC.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Bw. Estomih Chang'ah alikiri kupata taarifa na kueleza kuwa bado hajapata taarifa rasmi, hivyo anasubiri taarifa hiyo ndipo atakapoangalia kanuni za Serikali za Mitaa zinaelekeza nini juu ya tukio hilo.

3 comments:

  1. Kaaazi kwelikweli, vyama au wananchi? kama ni vyama kwanza hatuna haja ya kupiga kura. nadhani haya matukio yataendelea kupunguza idadi ya wapiga kura,uchaguzi ujao. kura haina heshima hata kidogo. Tumieni busara ndogo za kawaida kumaliza tofauti na sio kuzikuza. ugomvi wa baba na mama waachiwe wenyewe. wenzetu wako bize na maendeleo , sisi tuko bize na siasa za ujima!!! inatisha. ndio maana watu wanatoza ushuru hadi saa 6 usiku wakizani maendeleo yanaletwa na kutoza shilingi 1000!!!! fufueni viwanda (General tyre Kilitex nk)jengeni barabara. Acheni ujima.

    ReplyDelete
  2. HAWA VIONGOZI WA CCM NI WAPUMBAVU SANA. NA HAWA WANANCHI WALIOPIGA KURA , CCM IWAHESHIMU. NI UJING KUSUSIA KIKAO CHA MAENDELEO YENU WENYEWE. PUMBAVU SANA HAWA WAJUMBE WA WDC. NYIE MNAONA KULIKUWA NA UCHAGUZI WA MEYA NA NAIBU???MNASALI WAPI NYIE? HAMWOGOPI HATA MWENYEZI MUNGU???

    ReplyDelete
  3. Safi kabisa CCM. dawa ya moto ni moto akochomae mchome. Sasa Chadema mnalalmika nini; au mkuki nikwa nguruwe tu, kwa binadamu mchungu?
    Mwamdeka

    ReplyDelete