13 December 2010

Wailamu watakiwa kuepuka mgawanyiko kisiasa

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

VIONGOZI wa madhehebu ya dini ya kiislamu mkoani Shinyanga wameshauriwa kujiepusha na ushabiki wa kisiasa ambao unaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa waumini wake kwa misingi vya vyama vya kisiasa.Ushauri huo
ulitolewa jana na Sheikh wa mkoa wa Shinyanga, Sheikh Ismail Habibu Makusanya alipokuwa akiwahutubia waumini hao katika maadhimisho ya sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu wa 1432 Hijria zilizofanyika katika viwanja vya ShyCom mjini hapa.

Sheikh Makusanya alisema viongozi wa kiislamu wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanajenga umoja ndani ya uislamu badala ya kuwagawa waumini wake na kwamba wasitumie kofia ya kuwa viongozi wa dini kwa kuhubiri mambo ya siasa misikitini.
 Ndugu zangu viongozi wa kiislamu, eleweni suala la umoja katika nchi yetu ni suala muhimu sana, bila ya kuwa na umoja ni wazi tutakuwa na utengano mkubwa miongoni mwetu, hasa utengano unaosababishwa na mambo ya kisiasa ni mbaya zaidi dunia kote.

“Viongozi tusitumie kofia ya kuwa viongozi kuhubiri siasa katika misikiti, kumbukeni siasa ikitumiwa vibaya ina madhara makubwa mbele ya jamii, ni wajibu wetu kuchunga mipaka, kila muumini wa kiislamu ana uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa, lakini katika dini tunakuwa kitu kimoja,” alieleza Bw. Makusanya.

Sheikh huyo aliwataka waumini wa kiislamu kuhakikisha wanawaheshimu viongozi wa serikali walioko madarakani hata kama wao hawakuwachagua na kwamba kiongozi akiishachaguliwa na umma anapaswa kuheshimiwa.

“Ndugu zangu tusitumie kivuli cha dini kuwadhalilisha viongozi wetu wa kiserikali, ni lazima tuwaheshimu, hata kama kiongozi huyo wewe hukumchagua, lakini kwa vile
amechaguliwa kwa kura nyingi na umma hatuna budi kumuheshimu, hata Mtume wetu Muhammad (S.A.W) aliwahi kuongozwa na dola isiyokuwa ya kiislamu,Lakini aliiheshimu dola hiyo iliyokuwepo madarakani na kuishi kwa amani mpaka pale dola ya kiislamu nayo ilipopata nafasi kuongoza nchi, hakuwahi hata siku moja kuwadharau viongozi waliokuwepo madarakani japo hawakuwa waislamu,” alieleza Sheikh Makusanya.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Sheikh Salum Fereji ambaye ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza aliwataka waumini hao kuweka mkazo kutafuta elimu na kwamba bila ya kuwa na elimu hakuna lolote la maana linaloweza kufanikiwa.

No comments:

Post a Comment