13 December 2010

Exim Bank yapata tuzo ya NBAA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

BENKI ya Exim imeibuka mshindi wa jumla kwa Utayarishaji  mzuri wa mahesabu kwa mwaka 2009 katika hafla ya Tuzo za kila mwaka zinazoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) iliyofanyika
Arusha mwisho wa wiki.

Benki ya Exim ambayo inamilikiwa na Watanzania wazalendo na ambayo inakuwa kwa kasi kubwa nchini iliweza pia kuibuka mshindi kwa upande wa sekta ya benki kwa kuandaa vema mahesabu ya mwaka.Hii ni mara ya pili kwa benki hii kuibuka mshindi wa tuzo hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka 12 iliyopita. Benki hii pia ilishinda tuzo hii mwaka 2008.

Mshindi wa pili katika kinyang’anyiro hicho ni Benki M na mshindi wa tatu ni Diamond Trust Bank.

Naye Meneja Mwandamizi wa benki ya Exim, Bi. Lydia Kokugonza alisema tuzo hizo ni heshima kubwa sana kwa benki yake na kutambulika rasmi na bodi ya wataalamu ya NBAA kwa juhudi za kufanya kazi zake kwa uwazi ni mafanikio makubwa sana.

“Juhudi zetu kutaka kutoa huduma iliyotukuka kwa jamii na kwa utaalam mkubwa imeweza kutufanya kufikie mafanikio hayo makubwa. Tunayo furaha kubwa sana,” alisema.Kiwanda cha Cement cha Tanga kimeibuka mshindi katika sekta ya uzalishaji na usambazaji ikifuatiwa na kampuni ya Scania Tanzania Limited na ya tatu ikawa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC).

Kwa upande wa mashirika yanayojishughulisha na pensheni, Mfuko wa Pensheni kwa Serikali za Mitaa (LAPF) imeibuka mshindi likiwashinda Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Umma (GEPF).

Upande wa mashirika ya bima, shirika la ‘The Tanzania National Re Insurance Corporation Limited’ limeibuka mshindi likifuatiwa na Phoenix of Tanzania Assurance Ltd na African Life Assurance (T) Ltd.

Katika kinyang’anyiro hicho kampuni na taasisi 27 zilishiriki ambapo kwenye sekta ya kibenki yalikuwa makampuni nane, sekta ya uzalishaji na usambazaji kampuni sita, sekta ya bima kampuni nne na sekta ya pension kampuni tatu.Kwa upande wa kampuni za umma ambazo hufanya kazi kama mawakala wa serikali, hakuna mshindi aliyepatikana katika kundi hili mara baada ya kupata kura chini ya asilimia 75.

No comments:

Post a Comment