29 December 2010

Wachezaji Yanga kulipwa fedha zao

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umepanga kuwalipa wachezaji wake deni lao Januari 10, mwakani na kuwataka kusitisha mgomo waliodhamiria kuufanya.Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, iliyokutana
juzi ambayo ilikuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ya mgomo wa wachezaji ambao, Ijumaa iliyopita waligoma kufanya mazoezi wakishinikiza kulipwa fedha zao za usajili wa msimu huu.

Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana ndani ya kikao hicho, zilisema kuwa uongozi wa klabu hiyo uliwataka wachezaji hao, kusitisha mgomo kwa kuwa fedha wanazodai watalipwa Januari 10, mwakani.

"Kamati iliamua kwamba mpaka kufikia Januari 10 wachezaji watakuwa wamelipwa fedha wanazodai, hivyo iliwataka wasitishe mgomo wao na kuendelea na mashindano yao kama kawaida," kilidai chanzo hicho.

Hata hivyo kuna taarifa kwamba wachezaji hao nao wameweka msimamo wao kwamba, wanataka walipwe fedha hizo Januari 7, mwakani, vinginevyo watagoma tena kwani wamechoka kufanyishwa kazi bila malipo.

Wachezaji hao kwa ujumla wanaidai Yanga sh. milioni 70, ambazo walidaiwa kulipwa kwa awamu kitu ambacho kimeshindwa kufanyika.

Mbali ya suala hilo, kamati hiyo pia ilimjadili kiungo wa timu hiyo, Athuman Idd 'Chuji', ambaye suala lake lipo mikononi mwa Kocha Mkuu, Kostadin Papic ambaye anatakiwa kutoa ripoti ya mchezaji huyo na kamati ndiyo itatolea maamuzi.

Suala lingine lililojiri katika kikao hicho ni ushiriki wa timu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (CAF) na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa hizo zilidai kuwa katika hicho wajumbe wa Kamati ya Utendaji walipeana majukumu mbalimbali, huku  Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Ahmed Seif akitakiwa kuendelea na kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment