Na Mohamed Akida
TIMU ya vijana wenye umri wa miaka 20 ya Simba B, juzi ilikalia usukani wa kundi B katika michuano ya Uhai Cup inayoshirikiha timu za vijana za klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuifunga Toto Afrika mabao 3-1 inayofanyika
Uwanja Karume, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo licha ya Simba, kuibuka na ushindi huo mnono lakini ilionesha kandanda safi kiasi cha kufanya mashabiki wake waliofurika uwanjani hapo kuwashangilia kila wakati.
Ikicheza pasi fupi fupi, Simba iliandika bao la kwanza dakika ya 14 kupitia kwa Haruna Athumani, kwa shuti kali ambalo lilikwenda moja kwa moja wavuni.
Simba ilipata bao la pili katika dakika ya 44 lililofungwa, Edward Cristopher na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa na mabao hayo mawili.
Kipindi cha pili Toto Afrika, ambayo sehemu yake ya ushambuliaji iliingia kwa nguvu na kuliandama lango la wapinzani wake mara kadhaa, lakini hata hivyo washambuliaji wake hawakuwa makini kufunga mabao.
Simba nayo ilizidi kutakata na katika dakika ya 65, ilifunga mabao la 3-1 kupitia kwa winga wake Ramadhani Yahya, ambaye aliwalamba chenga walinzi wa Toto na kufunga kirahisi.
Toto Afrika licha ya kufungwa mabao hayo, wachezaji wake walijituma kwa nguvu kutaka kupata mabao na katika dakika ya 75 jitihada zao zilizaa matunda, baada ya kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Sebastian Bahati aliyepiga shuti lililombabatiza beki wa Simba na kutinga wavuni.
Simba ambayo ndiyo kinara wa kundi hilo kesho itapambana na Yanga yenye pointi.
No comments:
Post a Comment