30 December 2010

Mtibwa Sugar yaipiga Majimaji 4-0

Na Addolph Bruno

TIMU ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Mtibwa, jana iliianza vyema michuano ya Uhai Cup baada ya kuifunga Majimaji mabao 4-0.Michuano hiyo inashirikisha timu za vijana za klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania, inachezwa katika
Uwanja wa Karume Dar es Salaam.

Mtibwa iliuanza mchezo huo kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika 26, kupitia kwa Michael Mgimwa.

Baada ya kufungwa bao hilo, Majimaji nayo ilijikakamua kutaka kusawazisha bao hilo, lakini hata hivyo juhudi zao zilishindwa kuzaa matunda baada ya mabeki wa Mtibwa kuondoa hatari zote.

Kipindi cha pili Mtibwa walikianza tena kwa kasi kwa kuliandama mfululizo lango la Majimaji na dakika ya 54 iliandika bao la pili, lililofungwa na Mgimwa baada ya kumlamba chenga kipa, Rajabu Mtamila na kufunga kirahisi.

Licha ya kufungwa mabao hayo Majimaji, ilitulia na kucheza kwa kasi lakini hata hivyo washambuliaji wake walishindwa kuzitumia nafasi walizozipata.Bao la tatu la Mtibwa lilifungwa dakika ya 74 na Mgimwa kwa mkwaju wa penalti, ambayo ilitolewa na mwamuzi baada ya kipa wa Majimaji kumchezea vibaya Hamis Mroki, huku bao la nne likifungwa dakika ya 80 na Mgimwa ambaye jana alikuwa nyota ya mchezo kwa shuti kali la karibu.

No comments:

Post a Comment