14 December 2010

Poulsen awashukuru mashabiki wa soka

Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kuiwezesha Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', kutwaa ubingwa wa Chalenji 2010, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen,  amewashukuru mashabiki na wachezaji kwa ushirikiano waliompa na kutamba, Tanzania ikiwezeshwa,  inaweza.Ubingwa
huo ni wa tatu kwa Tanzania Bara kutwaa, tangu mashindano hayo yaanzishwe, ikiwa imepita miaka 16 ya ukame wa kombe hilo, mwaka huu imetwaa baada ya kuichapa Ivory Coast bao 1-0.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo juzi,  kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Poulsen alisema anajisikia furaha kutwaa ubingwa huo kwani ni changamoto ambayo imekuwa ikihitajika kwa muda mrefu nchini.

Alisema maandalizi mazuri waliyofanya na kushirikiana bega kwa bega na benchi lake la ufundi ambalo liliundwa na Kocha Msaidizi, Silyvester Marsh, kocha wa makipa, Juma Pondamali na Meneja Leopard Mukebezi, ndio waliofanikisha ubingwa huo ubaki nchini.

"Najisikia furaha sana kuona mashabiki wakijitokeza kuishangilia timu yao tangu mwanzo, nawashukuru sana pamoja na wachezaji wangu ambao kama si kujituma kwao,  tusingeweza kutwaa huu ubingwa," alisema Poulsen.

Alisema kutokana na kiwango kilichooneshwa katika mashindano hayo, ana imani kwamba, Tanzania sasa imepiga hatua kubwa na ina uwezo wa kucheza na timu yoyote barani Afrika, kwani wamepata uzoefu wa kutosha.

Poulsen aliongoza kuwa, timu hiyo katika mashindano hayo baada ya kushinda michezo saba mpaka fainali, huku ikipoteza mchezo mmoja dhidi ya Zambia katika hatua ya makundi kwa kufungwa bao 1-0.Kili Stars ilizifunga Somalia mabao 3-0, Burundi 3-0 na robo fainali ikaifunga Rwanda bao 1-0, nusu iliifunga Uganda kwa mikwaju ya penalti 5-4.

1 comment:

  1. Bravo Poulsen. Tatizo letu wabongo tunakata tamaa mapema sana. Nasema mwacheni mwalimu afanye kazi yako wale msiwe kimbelembele kumuingilia katika kazi yake. Tuvute subira hata kombe la dunia tunaweza kulichukua

    ReplyDelete