30 December 2010

EWURA yasitisha bei ya maji kupanda Kahama

Na Patrick Mabula, Kahama

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imesimamisha kusudio la Mamlaka ya Majisafi na Majitaka ya Wilaya ya Kahama (KUWASA) juu ya ombi lake la kutaka kuongeza gharama ya akra ya maji kwa wateja wake.Katika kikao
cha wadau wa maji kilichoitishwa na EWURA wiki hii, mamlaka hiyo ilikataa sababu zilizotolewa na kuainishwa na KUWASA kuhusu kuwaongezea gharama za maji wateja wa Kahama.

EWURA ilisema hatua hiyo imekuja baada ya KUWASA kuonekana na dosari za kiutendaji, ikiwemo mahesabu yake kutokaguliwa tangu kuanzishwa kwake.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Mutaekulwa Mutegeki alisema kabla ya kikao walishapitia sababu zilizotolewa na KUWASA juu ya kusudio na maombi yao juu ya kuongeza bei na kuona zina mapungufu mengi.

Katika kikao hicho wananchi na wateja wanaopatiwa huduma hiyo walipinga kuongezewa gharama za malipo ya maji, zikiwemo za kuingiza huduma hiyo majumbani mwao.Walisema tangu mradi huo uzinduliwe miaka miwili iliyopita hata gharama wanazotozwa katika akra zao ni kubwa, na hivyo kuiomba EWURA iwapunguzie kwa kuwa maji hayo hawayatumii kibiashara.

Awali katika taarifa yake, Meneja wa KUWASA wa Wilaya ya Kaham, Bw. Joel Rugemarila alisema mamlaka yake inakabiliwa na changamoto nyingi za uendeshaji ndiyo maana wanataka gharama ziongezwe.

1 comment:

  1. KUWASA hawamuhurumii mwananchi wa kawaida.
    gharama za maji Kahama zinataka kuwa kubwa kuliko sehemu nyingine za nchi , mfano mwanza, dar es salaam.
    eti wanasema maji yanatoka mbali,
    kwani watu wa mgodi hawachangii.
    maji ni huduma ya msingi kwa raia wa tanzania,
    tunawapongeza EWURA.

    ReplyDelete