30 December 2010

Balotelli: Mambo shwari Man City

LONDON, England

MSHAMBULIAJI, Mario Balotelli amesema kwamba anajisikia furaha akiwa  Manchester City na akajitetea kuhusu kutoshangilia, wakati anapofunga mabao.Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Italia, juzi aliifungia mabao matatu katika mchezo ambao
timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Aston Villa, lakini akashindwa kushangalia alipokuwa akipachika mabao hayo.

Mabao hayo yamemfanya, Balotelli kufikisha mabao manane katika michezo 11 aliyoichezea timu hiyo, tangu ajiunge nayo akitokea Inter Milan, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 anasema kufunga mabao ni sehemu rahisi katika kazi yake.

"Mara zote huwa nafurahi licha ya kuwa sitoi tabasamu," aliiambia tovuti ya klabu."Lakini najihisi kuwa mshambuliaji ninapokuwa nimefunga mabao na hii ndiyo maana huwa sitabasamu," aliongeza na akasema kuwa bado anajisikia mwenye furaha na anaweza kufunga mabao zaidi.

Kukosa kushangilia kwa nyota huyo kumezua tetesi za kuwa huenda anakabiliwa na ugonjwa wa kuwaza nyumbani lakini, Balotelli anapinga vikali madai hayo ya kwamba hajisikii vizuri kukaa Manchester City.

"Najisikia mwenye furaha kubwa, licha ya waandishi wa habari wa Italia kusema kuwa nataka kurudi Milan," alisema."Nipo mahali hapa nitajituma kwa nguvu mazoezini, nahitaji kuwa mtu muhimu katika timu hii na matokeo yatakuwa uwanjani," aliongeza.

Kiwango cha Balotelli, kimemuweka njia panda kocha wa timu hiyo, Roberto Mancini katika uteuzi wa kikosi chake kwa ajili ya mechi ya Jumamosi dhidi ya  Blackpool wakati nahodha wa timu hiyo, Carlos Tevez akitarajiwa kurejea uwanjani baada ya kupumzishwa wakati wa mechi dhidi ya Aston Villa.

No comments:

Post a Comment