Na Tumaini Makene
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo Bw. John Mnyika ameanza kusaka hoja za kuwasilisha bungeni, kwa kukutana na makundi ya watu mbalimbali katika eneo lake, kabla ya bunge la Februari mwakani, ambapo ameanza na kundi la wasomi kutoka vyuo
mbalimbali vilivyoko Dar es Salaam.
Katika mkakati wake huo, ambao amesema kuwa utamsaidia kwenda bungeni akiwa na hoja zinazotokana na wananchi wa jimboni kwake badala ya hoja zake binafsi, alitumia siku ya mwisho wa wiki iliyopita kusikiliza maoni ya vijana wasomi katika Kongamano la Maendeleo ya Jimbo la Ubungo.
Kongamano hilo, ambalo Bw. Mnyika alikuwa mgeni rasmi, lilihudhuriwa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Tiba za Afya na Sayansi (MUHAS), Chuo cha Maji, Chuo Kikuu cha Ardhi (UCLAS), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ambavyo karibu vyote viko Jimbo la Ubungo.
Katika kongamano hilo wanafunzi kutoka kila chuo waliwasilisha hoja juu ya kero mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya wakazi wa Ubungo kulingana na fani zao katika vyuo wanavyosoma.
"Mimi nashukuru, kwa kweli kongamano la leo lilikuwa ni kusikiliza zaidi na ku-note masuala kama yalivyowalisilishwa hapa na ninyi wasomi, hoja mbalimbali zimewekwa hapa, matatizo ya hakimiliki za ardhi, elimu, afya, usafiri na maji.
Bw. Mnyika aliwaambia wanafunzi hao kuwa si rahisi kwa mbunge mmoja kufanya masuala karibu yote peke yake, kama vile kuandaa hoja binafsi za kuwasilisha bungeni, kwani atajikuta anatumia muda mrefu katika suala moja kisha kusahau kero zingine zinazowasumbua wakazi wa jimbo husika.
"Hili ni la muhimu, mbunge akitaka afanye kazi zote hizi peke yake, itakuwa ngumu atajikuta anatumia muda mwingi kuandaa hoja binafsi... niwaombe kwamba kila mmoja katika eneo ambalo ana uwezo nalo, ajitahidi kufanya utafiti na uchambuzi wa kina.
Bw. Mnyika alisema baadaye atakutana na makundi mbalimbali kama vile mamantilie, wafanyabiashara ndogondogo kabla ya bunge la Februari mwakani.
No comments:
Post a Comment