Na Mwandishi Maalumu
Rais Jakaya Kikwete jana asubuhi katika Ikulu ya Dar es Salaam alipokea Hati za Utambulisho za Mabalozi kutoka Sweden na Norway na kufanya nao mazungumzo yanayohusu ushirikiano baina ya nchi zao na Tanzania.Wote kwa nyakati tofauti
walimpongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.Wa kwanza kuwasilisha hati alikuwa ni Balozi Lennarth Hjelmaker wa Sweden ambapo rais alianza mazungumzo kwa kutoa pole kwa nchi ya Sweden kwa kukumbwa na mashambulio ya mabomu ya kigaidi katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo wa Stockholm, Jumamosi iliyopita.
Uhusiano wa Tanzania na Sweden ni mkongwe ambapo Tanzania imekuwa ikipokea misaada ya maendeleo, mazingira na pia katika kusaidia jitihada mbalimbali za sekta binafsi. Aliyefuatia kuwasilisha Hati za Utambulisho alikuwa ni Balozi mpya wa Norway nchini, Bi. Ingunn Klepsvik wa Norway.
Bi. Klepsvik alianza mazungumzo yake kwa kumpongeza Rais Kikwete kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa Visiwani Zanzibar.
Katika kuzungumzia suala hilo, Rais Kikwete alimweleza Bi. Klepsvik kuwa hata yeye amefarijika sana na matokeo ya muafaka wa Zanzibar kwa sababu tangu kuingia madarakani aliweka azma ya kuanza mazungumzo ambayo yataleta maridhiano kwa manufaa ya Visiwa vya Zanzibar, watu wake na Tanzania kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment