31 December 2010

Mbwete abeza vyuo vya bweni

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria nchini, Prof. Tolly Mbwete ameishangaa na kuibeza mikakati ya serikali kuhusu kujenga vyuo vikuu vya bweni kila kanda kwa kuwa mpango huo ni kupoteza mabilioni ya Watanzania bila faida.Akizungumza wakati
wa sherehe ya kuwapongeza wahitimu wa  chuo hicho, Tawi la Mbeya katika ngazi ya cheti, shahada na shahada ya uzamili, Prof. Mbwete alisema kuwa inashangaza kuona wakati dunia kwa sasa inaweka mkazo katika vyuo vikuu huria, Tanzania inataka vyuo vya bweni.

"Mimi nasema wazi ndio maana viongozi wa serikali tena wakuu wanashindwa kutambua mchango mkubwa chuo chetu  ambacho ndicho kinachoongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi waliodahiriwa wakiwemo viongozi wengi,"alisema Prof. Mbwete.

Alisema kuwa katika ulimwengu wa sasa Watanzania wanapaswa wapatiwe elimu huru itakayowawezesha kupata nafasi ya kusoma bila kuharibu ratiba zao na hivyo mpango wa kujenga vyuo vikuu vya bweni unaonesha jinsi ambavyo serikali iko tayari kupoteza  mabilioni ya fedha bila huruma.

Prof. Mbwete alisema kuwa mabilioni ya fedha yaliyotumika kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma yangetumika kujenga vyuo vikuu huria vingi ambavyo vingesaidia Watanzania wengi waliokosa nafasi kwenye vyuo vyuo vikuu vya bweni.

Aidha Prof. Mbwete aliitaka serikali kutambua juhudi zinazofanywa na chuo hicho wakati wote inapozungumzia  hali halisi ya elimu ya juu Alisema chuo hicho kimekuwa kikisahaulika na viongozi hao huku wakiujua kuwa ndicho chuo kikuu pekee kinachofanya kazi nzuri nchini.

Alisema kuwa chuo hicho kimepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa na  mwaka huu wamedahiri zaidi ya wanachuo 40,000 idadi ambayo  ni ya juu kutokana na mwamko mkubwa wa Watanzania kupenda kukitumia chuo hicho.

Alisema kutokana na mafanikio wanatoa huduma katika kanda  nyingi na sasa wameanunua eneo la wazi karibu wakiwa na  mpangoo kujenga Hotel ya Kisasa kwa ajili ya kitega uchumi.

No comments:

Post a Comment