31 December 2010

Aliyesahaulika mkasi tumboni afariki dunia

Na Waandishi Wetu

MGONJWA aliyefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kudaiwa kusahaulika mkasi tumboni, Scolastika Rwambo (43), mkazi wa Kigogo, alifariki usiku wa kuamkia jana hospitalini hapo.Kwa mujibu wa msemaji wa
familia hiyo, Bw. Peter Rwambo, ndugu yao, ambaye ni kocha wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Matokeo, Kigogo Luhanga, alifariki saa 9 usiku wa kuamkia jana, wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Alisema wamepata na mshtuko kutokana na kifo cha ndugu yao huyo na wameiomba serikali kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha uzembe huo na kuwawajibisha wote waliohusika.

Wanandugu hao wameshangazwa na baadhi ya watendaji wa hospitali hiyo kuwakataza kuchukua picha ya mgonjwa huyo ICU iliyopigwa na kuonyesha mkasi huo tumboni na risiti walizolipia kwa ajili ya huduma hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa Bw. Rwambo wanafanya jitihada kuendelea kufuatilia vielelezo hivyo na endapo watashindwa kuvipata watawasiliana na wanaharakati wa haki za binadamu ili waweze kuwasaidia kuvipata.

Mgonjwa huyo alikufa saa chache baada ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Deo Mtasiwa, kusema wizara yake imeagiza uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili madaktari dhidi ya mgonjwa huyo zifanyike haraka iwezekanavyo.

Ofisa Uhusiano wa MNH, Bw. Aminiel Aligaesha alisema suala hilo linashughulikiwa na majibu yatatolewa baada ya uchunguzi kufanyika.
Scolastika alifikishwa hospitalini hapo mwishoni mwa Septemba mwaka huu, ambapo alilazwa na kufanyiwa upasuaji wa tumbo Oktoba 4, mwaka huu.

Baada ya upasuaji huo aliruhusiwa kurudi nyumbani lakini katika kipindi chote nyumbani tumbo lilikuwa likimsumbua na kulazimika kurudishwa hospitalini hapo ambapo alipimwa na kugundulika kuwa kuna mkasi tumboni mwake.

9 comments:

  1. Haya, kesi nyingine hiyo ya muhimbili, mara wa kupasuliwa kichwa achinjwe mguu, wa mguu kichwa, mtoto mchanga achomwe sindano siyo mkono umeoza ukatwe, leo mikasi isahauliwe tumboni, kesho hata sijui lipi lipo jikoni Mungu ndie ajuae! Sikwambii matusi na ukali wa ma-nurse utadhani wao ndio mwisho wa reli Kigoma!

    ReplyDelete
  2. Inaudhi halafu hiyo tume utasikia inaundwa na madaktari wenyewe unategemea nn hapo. Waandishi shupalieni hili mpaka kieleweke, hawa jamaa wamezoea sasa. Wao wanajua baada ya muda tutasahau so waandishi komalieni tuone mwisho wake.

    ReplyDelete
  3. Haya hapo tena uchunguzi ufanywe nini kilichosababisha, au ndiyo daktari kamwachia nesi au mwanafunzi amalizie kazi?

    ReplyDelete
  4. mtatumaliza kwa uzembe wenu...kwani mmelazimishwa kufanya hizo kazi?? achieni wenye wito jamani...sishangai ndo maana wakubwa wanakimbilia nje..maana wameshindwa kukabiliana na hou uozo...

    Mwasi

    ReplyDelete
  5. AMBANI
    Huu ni uzembe usiostahili kuvumiliwa, mhusika lazima awajibike, hawa ni watoto wa vigogo wanaochakachua Elimu wakiingia kazini wanaharibu. Masikini mama wa Watu kapoteza maisha kutokana na uzembe wa mtu?

    ReplyDelete
  6. jamani muende mbele mkirudi nyuma,kwani madaktari ni malaika hata hawakosei?mema yote wafanyayo kuwatibia binaadamu na kujitolea mpaka kuhatarisha maisha yao, wengine wanapata hadi ukimwi na magonjwa mabaya lakini yote hayaonekani iwapo atakosea mara moja. wao walikuwa na nia njema ya kuokoa maisha yake ndio wakamfanyia operation ya kwanza,hivi tujiulize muhimbili wanalazwa wagonjwa wangapi?mbona wengi wanapona na kuendelea na maisha yao?kifo ni mipango ya mungu na kila mmoja wetu ameshapangiwa sababu yake ya kumuondosha duniani.

    ReplyDelete
  7. uzembe hauvumiliki

    ReplyDelete
  8. Madaktari sio malaika huo ni uzembeeeeeeeee!!!!
    sitaki hata kuzungumzia kwa kirefu. sijui nana wewe unfananisha daktari na malaika strange!

    ReplyDelete
  9. Tukiwafananisha madaktari na malaika inaonyesha jinsi ambavyo tuko nyuma kimawazo katika kutatua matatizo yanayoweza kuzuilika. Je unashangaa kwanini tuko nyuma kimaendeleo? ni mawazo finyu na kutotaka kutafuta utatuzi wa matatizo yanayotukabili kila siku. hiyo ni pamoja na kusema sisi ni masikini hatuwezi........most mistakes are preventable. ASK ME HOW!!!!!!!!!! acheni kuwaonea madaktari aibu

    ReplyDelete