*Afikiria zawadi ya kuwapa
Na Amina Athumani
RAIS Jakaya Kikwete amesema anafikiria zawadi ya kuwapa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', kutokana na furaha kubwa waliyoileta kwa Watanzania baada ya kunyakuwa ubingwa wa
Chalenji juzi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika hafla iliyofanyika Ikulu kwa ajili ya kukabidhiwa kombe la Chalenji, Rais Kikwete alisema atakaa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Emmanuel Nchimbi, kujadili zawadi hiyo na kuwakabidhi wachezaji hao kama pongezi kwa ushindi walioupata katika michuano hiyo.
Rais Kikwete amewataka wachezaji wa Kilimajnaro Stars kuhakikisha ubingwa huo uliokosekana kwa kipindi cha miaka 16, wanaendelea kuushikilia katika michuano ya mwakani ili kuendelea kulinda heshima ya nchi na soka la Tanzania.
Sanjari na hilo, Rais Kikwete amewataka wachezaji wa Kilimanjaro Stars ambao pia wengi wao ni wachezaji wanaounda timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', kuhakikisha wanapigania kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2012, ili kuiweka Tanzania katika mazingira mazuri ya kupiga hatua katika soka kujiimarisha katika kushiriki fainali za kombe la Dunia.
"Bado kiwango chetu hakijawa kikubwa sana cha kuweza kusema tunaweza kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, hiyo itakuwa ni danganya toto, lakini tutakapoweza kufanikiwa kushiriki Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani na Mataifa ya Afrika, tunaweza kuona mwanga wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 au 2022," alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ameishukuru CECAFA na uongozi bora wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kazi nzuri inayofanywa pamoja na ushirikiano wanaoutoa kwa Kocha Mkuu wa Kimataifa, Jan Paulsen, na kwamba, kiwango cha soka la Tanzania kimebadilika na kupiga hatua mbele.
Rais Kikwete amempongeza Rais wa TFF, Leodeger Tenga, na uongozi mzima kwa kutoingiza ushabiki wa vyama katika shirikisho hilo kwa kuwa, shirikisho hilo lipo kwa ajili ya kuijenga timu ya Taifa na siyo ushabiki wa vyama.
"Ninachoweza kusema, ninawaomba mwendelee kuijenga TFF nzuri ili kupata mafanikio zaidi, ushindi huu ni mwanzo tu, na ndio kwanza unachomoza kwenye mafanikio, safari yetu bado ndefu sana, tukitilia mkazo tunaweza kushinda," alisema Rais Kikwete.
Wakati huo huo, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanznaia (TASWA), kimemtunukia tuzo Rais Kikwete ya kutambua na kuthamini mchango wake katika jitihada za kuendeleza michezo, utamaduni na muziki nchini.Akikabiddi tuzo hiyo kwa Rais Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa TASWA, Maulid Kitenge, alisema juhudi anazozifanya Rais Kikwete ni mfano wa kuigwa na kupongezwa na kila mdau anayependa maendeleo ya michezo nchini.
Rais Kikwete alisema tuzo hiyo itamuongezea changamoto ya kuweza kuzidi kuisaidia michezo nchini, huku akiahidi kukutana na viongozi wa riadha kujua chanzo cha kutofanya vizuri wakati wana kocha wa kimataifa.
No comments:
Post a Comment