22 December 2010

Jaji anusa rushwa kesi ya rada

Na Willibroad Mathias

KESI ya mkataba tata kati ya Tanzania na Kampuni ya uuzaji wa vifaa vya kijeshi ya BAE System ya Uingereza imeingia katika sura mpya baada ya Jaji wa Mahakama ya Southwark Crown kunusa rushwa katika mgawo kwa mawakala wa
biashara hiyo.

Rushwa hiyo ni ile inayodaiwa kutumika kuwalainisha vigogo wa serikali ya Tanzania ili kukubali maozo hayo yaliyofanyika kwa bei kubwa zaidi ya ilivyotakiwa.

Kampuni hiyo ya BAE, mapema mwaka huu ilifikia makubaliano na Taasisi ya Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) baada ya kukiri kuwapo makosa katika hesabu zake,  kwamba haikutoa rushwa kuwashawishi vigogo wa Tanzania ili kupata mkataba wa zaidi ya sh biliobi 70 kuizuia rada hiyo ya kijeshi, lakini ikaelezwa kuwa iliwalipa mawakala kuwashawishi.

Lakini jana, Jaji Justice Bean aliuliza maswali kuhusu madhumini ya malipo hayo, huku akirudia kusema kuwa kampuni hiyo inaonekana kuhusika katika mazingira ya rushwa, na iliwahonga watoa maamuzi nchini Tanzania.

Aliieleza mahakama hiyo kwamba inavyoonekana kampuni hiyo ya BAE ilitaka kulipwa chochote ama kutoa chochote kinachohitajika ili kupata mkataba huo kutoka kwa Tanzania.

Aliongeza kuwa inaonekana wazi kwamba kampuni hiyo ya BAE haikutaka ionekane kuzigusa fedha hizo na badala yake ilichotaka ni kazi hiyo kufanyika. "Wao walitaka tu kazi ifanyike wala isisikike kwa wabaya na wala kuonwa na maadui," alisema.

Februari mwaka huu kmapuni hiyo ya BAE iliingia makubaliano na SFO na waendesha mashtaka wa Marekani kukiri makosa ili kumaliza kipindi kirefu cha uchunguzi kuhusu tuhuma za rushwa inazozitumia katika njia za biashara zake.

Katika makubaliano hayo, kampuni hiyo ya Uingereza ilikiri hatia ya kutohifadhi taarifa sahihi kuhusu kuiuzia Tanzania rada huku mabingwa hao wa kuuza silaha wakikubali kulipa fidia ya pauni milioni 30 (zaidi ya sh biliono 70) baada ya kukiri kuwepo mapungufu katika kanuni za akaunti zake kuhusu mkataba wa kuiuzia Tanzania rada.

Hatua ya BAE kukiri makosa hayo ni sehemu ya makubaliano baina yake na idara inayopambana na ufisadi ambapo BAE ilitakiwa kutoa majibu kuhusu kesi kadhaa za ufisadi.

Ilielezwa kuwa kampuni ya BAE Systems ilimteua raia wa Tanzania, Bw. Shailesh Vithlani kama wakala wa kisiri wa kuisadia kupata zabuni ya kuiuzia Tanzania mtambo wa radar.

Wakala huyo alipelekewa malipo yake kupitia kampuni moja iliyosajiliwa katika visiwa vya Virgin nchini Uingereza vilivyopo Amerika ya Kusini.

BAE Systems inakiri kwamba fedha hizo zilikusudiwa kumlipa kwa kazi aliyofanya ya kuishawishi serikali ya Tanzania kuipendelea kampuni hiyo katika kutoa zabuni.

Mahakama imeelezwa haingewezekana kubaini ni jinsi gani Bw. Vithlani alizitumia vipi fedha hizo.SFO inasema haikuishtaki kampuni ya BAE kwa rushwa, ila kwa kukosa kuhifadhi mahesabu sahihi ya biashara hiyo, jambo ambalo limesababisha Tanzania kushindwa kuwashtaki vigogo wake, waliotuhumiwa kuhusika na tatizo hilo.

Jaji Bean aliyesikiliza kesi hiyo anasema kampuni hiyo haikutaka kuhusishwa na fedha hizo wala kujua ni kiasi gani cha pesa kilicholipwa wala nani aliyepokea malipo, na kwamba wao walichotaka ni kazi hiyo itekelezwe.

Kutokana na kukiri makosa hayo, BAE imesamehewa kesi zote za ufisadi zilizokuwa zinachunguzwa mkiwemo suala la kuiuzia silaha Saudi Arabia, Jamhuri ya Czech na Afrika Kusini.BAE imesema imechukua hatua madhubuti kuhakikisha inatimiza maadili ya hali ya juu katika biashara.

Lakini hata hivyo jana, Bw. Victor Hekalu, Ofisa Mwandamizi wa SFO, aliiambia Mahakama kuwa kampuni ya BAE imejenga mfumo wa kuwawezesha mawakala wake kuuza silaha sehemu mbalimbali duniani.Alisema kuwa wakati washauri wakiendesha kazi zao kwa uwazi, kuna mawakala wa BAE ambao wanaedesha kazi hiyo kwa usiri mkubwa.

Alisema kuwa Sir Richard Evans, ambaye ni Mwenyetiki wa  BAE, binafsi alishathibitisha kumtumia Bw. Sailesh Vithlani kama wakala wa siri kwa ajili ya kufanikisha ununzi wa rada ya Tanzania, pia kumtumia Bw. Mike Turner ambaye baadaye alikuja kuwa Mkurugenzi Mkuu wa BAE.

Bw. Temple alisema kuwa katika kuhakikisha mpango huo unakamilika, kampuni ya BAE ilimlipa Bw. Vithlan dola milioni 12.4 kati ya mwaka 2000 na 2005 ambazo ni sawa na robo tatu ya thamani ya mkataba huo wa rada.

Kampuni hiyo ya BAE inadaiwa kulipa kiasi hicho kupitia kampuni ya Red Diamond, inayomilikiwa na Bw. Vithlani.Pia jana mahakma hiyo ilisikia kuwepo makubaliano kadha wa kadha kati ya SFO na BAE ambayo yalifikiwa kabla ya kufika mahakamani, ambayo jaji huyo aliyaita kama  "sehemu muhimu" ya kesi, ana akarudia kuhoji mlungula huo kwa ajili ya SFO na BAE ulikuwa utumike kwa matumizi yapi.

Akitilia shaka zaidi makubaliano hayo, jaji huyo alisema, "Nilichogundua kilichotokea kama fedha hazikutumika katika mazingira ya rushwa ni kwa nini asilimia 97 ilipwe kupitia katika kampuni ya BVI, ambayo inamilikiwa na BAE ambao ni mkondo mwingine unaomilikiwa na Vithlani?"

Wakati Bw. Temple aliposema kuwa Bw. Vithlani alikodishwa kwa ajili ya kuisaidia BAE, jaji huyo alihoji kuwa kama ni hivyo, ni kwa nini alilipwa fedha nyingi kwa ajili ya kazi hiyo, huku Bw. Temple akisema kuwa kazi ya ushawishi ni kazi halali. "Kwa kushawishi ni jambo moja, na rushwa ni jambo jingine".

Bw. David Perry, ambaye ni mwakilishi wa kampuni hiyo ya  BAE,alisema kwa kuwa kampuni hiyo haikukiri kosa lololte kuhusiana na rushwa, hivyo inapaswa kuhukumiwa kwa kosa moja la kasoro katika hesabu zake.

Ilielezwa kuwa baada ya marumbano hayo jaji alitishia kuita mashahidi wapya akitaka kufahamu madhumini ya kutolewa fedha hizo, lakini badaye akaamua kuendelea na kesi ili kutoa hukumu yake leo.

2 comments:

  1. Hii ndio hali halisi ya nchi yetu. Nashukuru serikali ya Uingereza kulivalia njuga swala la rada, lakini zaidi ya yoote. Nchi husika ambayo ni Tanzania haikua na upelezi juu ya hili swala kitu cha kushangaza saana. Tofauti na kashfa ya rada, ni mikataba mingapi ambayo haifaamiki ambayo nchi imeingia kinyemela kupitia watu binafsi! Tanzania tuamke, je tunajua tunapoelekea au hata ardhi tunayokalia si yeetu itafika mda tutaondolewa.

    ReplyDelete
  2. Mwenye macho haambiwi tazama. Hata kama kesi yenyewe imehukumiwa ki-mtego mtego, ukweli umejulikana. Laana ya hayo waliyotufanyia inaendelea kumkumba mmoja baada ya mwingine; mara wagonge vibajaji, mara watuhumiwe uchawi bungeni...........

    ReplyDelete