Na Peter Mwenda
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC)limewataka wapangaji ambao wamepangishwa na wateja wa shirika isivyo halali, wajitokeze ili kupewa mikataba halali.Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa NHC, Bi. Suzan Omari alisema jana kuwa
wapangaji wengi wa aina hiyo walijitokeza na kupewa mikataba halali ya upangaji na shirika lakini idadi kubwa ya wapangaji hawajafanya hivyo.
Alisema NHC inatoa nafasi nyingine kwa wapangaji wote wenye upangaji kama huo kujitokeza ili waweze kufuata taratibu zilizopo za upangaji na kutambuliwa rasmi.
Bi. Suzan alisema utaratibu huo utakapofungwa rasmi shirika hilo halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kuwa bado na upangaji ambao ni kinyume na taratibu zilizowekwa na shirika.
Alisema hivi karibuni kumezuka wimbi la watu kununua upangaji wa nyumba za NHC kwa matarajio kwamba watafaidika kwa kuuziwa na shirika hapo baadaye katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema kununua upangaji bila kufuata taratibu zilizowekwa na shirika ni uvunjaji wa sheria na kuwatahadharisha wananchi wanaonunua nyumba hizo kuwa shirika litauza nyumba zake kamwe wanadanganyika.
Alisema shirika hilo lina mikakati ya kuvunja nyumba hizo ili kujenga majengo mengi ya ghorofa ambazo zitapunguza tatizo la nyumba kwa familia na kuuziwa wananchi.Naye Meneja Miliki wa NHC, Bw. Joseph Mganga alisema mpango wa miradi hiyo itaanza mwakani na wananchi watafahamishwa pale utekelezaji utakapoanza.
Katika hatua nyingine kazi ya ukusanyaji madeni ya sh. bil 9 linaendelea kutia moyo lakini bado kuna wadeni sugu wenye malimbikizo makubwa wakiwemo Wizara na taasisi za Serikali. Alisema kazi ya kuwatoa wadaiwa sugu kwenye nyumba za shirika hilo imeanza na shirika halitasita kuwachukulia hatua.
No comments:
Post a Comment