30 December 2010

Ajali yauwa watano Same

Na Martha Fataely, Same

WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa vibaya baada ya magari mawili madogo kugongana uso kwa uso katika eneo la Mabilioni-Hedaru wilayani Same, Mkoa wa  Kilimanjaro.Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa
Wilaya ya Same, Bw. Ibrahimu Marwa na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Yusuph Ilembo ilieleza kwamba ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi katika eneo hilo.

Bw. Marwa alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T 707 APS aina ya Prado iliyokuwa ikitoka Moshi kwenda Dar es Salaam na gari jingine aina hiyo hiyo yenye namba T 891 AMX iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi.

Aliwataja waliofariki kuwa ni dereva wa gari lenye namba T 707 APS, Inocent Massawe, na wengine Ludovick Downson, Abuu Muro, Neema Muro na Neema Hatibu waliokuwemo katika gari lililokuwa likitoka Dar es Salaam.

Majeruhi katika ajali hiyo waliotajwa ni Hassan Mohamed, Seleman Mohamed, Hassan Abeid, Hussein Abdul, Yohana Idrisa na Blandina Mrema wakazi wa Dar es Salaam na Moshi ambao hali zao ni mbaya na wamelazwa katika Hospitali ya KCMC Moshi.

Bw. Marwa alisema majeruhi wengine wanne wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same na wanaendelea na matibabu ambapo hali zao kiafya si mbaya.Hata hivyo Marwa alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana na Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi ambapo taarifa kamili itatolewa baadaye.

No comments:

Post a Comment