13 December 2010

Afa ajalini akienda harusini

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MTU mmoja amekufa na mwingine kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wanasafiria kwenda harusini Dar es Salaam wakitokea Arusha, kupinduka katika kijiji cha Kasiga, Kata ya Mazinde, tarafa ya Mombo wilayani Korogwe.Mganga
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Dkt. Rashid Said alimtaja marehemu kwa jina la mama Rama (28) ambaye ni mkazi wa Moshi ambapo alikuwa anakwenda Dar es Salaam kwenye harusi ya bintiye.Dkt. Rashid alimtaja majeruhi alielazwa kuwa ni Bi. Moshi Machemba (50) mkazi wa Arusha eneo la Ngarenaro, na ameumia sehemu ya kifua na kichwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari akiwa amelazwa wodi namba mbili Bi. Machemba ambaye pia ni mmiliki wa gari  aina ya Toyota Nadia yenye namba T 617 BAW lililopata ajali, alisema mkasa huo uliowakuta jana saa mbili asubuhi ulichangiwa na dereva wake, Bw. Mbwana Hassan (65).

Bi. Machemba alisema walipofika kijiji cha Mazinde, Bw. Hassan alizozana na mke wake, baada ya kumwambia hawezi kupata nafasi ya mtoto wake kukaa sababu gari imejaa, kitendo kilichomfanya Bw. Hassan kuondoa gari kwa hasira na kukanyaga gunia la mchele lililokuwa pembeni ya barabara.

Mwenye gunia alitaka kulipwa, lakini Bw. Hassan hakumjali na kuondoa gari ambalo lilipinduka kilomita mbili baada ya hapo, baada ya hapo, wakati Bw. Hassan alipokata kona kwa nguvu, na kupinduka mara tatu.

"Tangu tunatoka Arusha nilimwambia dereva kama leo hutaki kuniendesha ungesema mapema, kwani alipofika Moshi alituingiza kwenye matuta, baada ya kumkemea akapunguza mwendo kabisa hadi kimometa 20 kwa saa. Lakini alipandwa na hasira baada ya mzozo na mkewe, na nilimwambia tulipaswa kumlipa mwenye mchele akapuuza, hatukufika mbali tukapinduka," alisema Bi. Machemba.


Bi. Machemba alisema walikuwa wanakwenda kwenye harusi Desemba 18, mwaka huu ambapo mtoto wake wa kiume Bw. Salum Machemba anamuoa Bi. Hamida ambaye marehemu ni mama yake mdogo.

Alisema wengine ambao walikuwa kwenye gari hilo lakini hawakuumia ni mtoto wa marehemu mwenye mwaka mmoja aitwae Rahma, Bi. Grace Stephen (20) na mwanafunzi wa kidato cha pili Abdul Yahaya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Bw. Libaratus Sabas hakupatikana, lakini Mkuu wa Polisi Wilaya ya Korogwe Bw. Zubeir Shemndolwa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment