*TASWA yanena kwa majonzi
*Yanga yatoa ubani 500,000/-
Na Zahoro Mlanzi
MKURUGENZI Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Juliana Yasoda na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
, jana waliongoza mazishi ya aliyekuwa Kocha wa viungo na mshauri wa saikolojia wa timu ya Simba, Syllersaid Mziray, yaliyofanyika katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kabla ya kwenda kuzika, maelfu ya wadau wa michezo na watu mbalimbali walitoa heshima za mwisho kwa kocha huyo kwa kumuaga katika viwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam.
Wakati shughuli ya kumuaga ikiendelea, ghafla kuliripuka shangwe baada ya mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azan, kutokea na watu kuanza kushangilia huku kila mmoja akiwa na kiu ya kutaka kujua kama ameshinda au vinginezo.
Kutokana na kuzongwa na watu wengi, Azan ilimbidi azungumze kwa kuwataka wavute subira mpaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itakapotangaza matokeo rasmi.
Akizungumza kabla ya shughuli za kumuaga kocha huyo, Yasoda alisema serikali inatambua kwamba, imempoteza kocha muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho nchi ipo katika mkakati wa kuinua michezo zaidi nchini.
"Ninaungana na familia ya marehemu katika wakati huu mgumu na hata kwa wadau wa michezo, hususan timu ya Simba, serikali inatoa pole na inajua imempotea mtu muhimu," alisema.
Naye, Tenga alisema kuondoka kwa Mziray ni pengo kubwa ambalo halitazibika katika medani ya soka nchini, na alitoa pole kwa wana-familia ya kocha pamoja na Simba.
Mbali na viongozi hao, pia Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Llody Nchunga, alipata nafasi ya kuzungumza ambapo kwa niaba ya Yanga na mashabiki wao, walitoa sh. 500,000 ikiwa ni pole kwa familia na kwamba, licha ya kuwa na utani wa jadi wakiwa michezoni, lakini husaidiana katika mambo mbalimbali ya kijamii.
Kwa upande wa Simba, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alizungumza kwa niaba ya timu kwa kusema timu yao ipo katika majonzi kwa kuondokewa na mtu muhimu ambaye aliipa mafanikio.
Alisema hivi karibuni waliingia mkataba mpya na kocha huyo ili azidi kuleta mafanikio kitu ambacho hakijafanyika na kwamba, ameondoka wakati bado wanamhitaji.
Wakati huohuo, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimesikitishwa na kifo hicho kwani bado mchango wake ulikuwa ukihitajika katika medani ya soka nchini.
Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Pinto, alisema mbali na kusikitishwa na kifo hicho, pia wanasikitishwa na kitendo cha familia ya kocha huyo kwa kushindwa kutoa ushirikiano wakati alipokuwa akiumwa.
Alisema kocha huyo ni mtu wa watu, hivyo waandishi wa habari za michezo walipokuwa wakihitaji taarifa zake, familia kushindwa kutoa ushirikiano halikuwa jambo la kiungwana na wana imani sasa, watapata ushirikiano wa kutosha.
Kocha huyo ameacha mke na watoto wawili, ambapo alizaliwa Novemba 11, 1957 na kupata elimu ya msingi katika shule ya tofauti tofauti za Ifunda, Low Academic (Iringa), Mpechi (Njombe), Songwe (Mbeya), Butimba (Mwanza), Lukajunge (Karagwe) na kumalizia Wami (Morogoro).
Elimu ya sekondari aliipatia katika shule za Malangali (Iringa) na Milambo iliyopo Tabora na baadaye kujiunga na Jeshi la Kejenga Taifa (JKT), na mwaka 1981 alikwenda kusoma nchini Bulgaria na kupata shahada ya pili ya michezo.
Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.
No comments:
Post a Comment