Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa timu ya soka ya Azam FC, umesitisha mkataba wa Kocha, Itamar Amorin, sasa timu hiyo itakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Habib Kondo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa, alisema wameamua kusitisha mkataba huo kwa nia nzuri na si kwa ugomvi wowote.
"Timu yetu ipo katika nafasi nzuri, tumeona haina haja ya kuendelea na Itamar, na ndio maana tumekaa naye na kukubaliana kusitisha mkataba wake," alisema.
Alisema kusitisha mkataba wa kocha huyo, si kwa nia mbaya, ni makubaliano ya pande zote mbili, na kwamba, ni kocha mzuri na ameiwezesha timu yao kushika nafasi ya nne, wakiwa na pointi 17, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Idrissa alisema, kwa kipindi ambacho wanamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa wamebakiza mechi moja, timu hiyo itakuwa chini ya kocha wake msaidizi Kondo.
Alisema kuanzia mzunguko wa pili wataanza mikakati ya kumtafuta kocha wa kuziba pengo lake, na wanamtakiwa kila la kheri Kocha Itamar, kwani alikuwa ni kocha mzuri na ametoa mchango wake mzuri kwa timu yao.
No comments:
Post a Comment