29 November 2010

Wakesha nje kuhofia 'popobawa'.

Na Theonestina Juma, Ngara.

WANANCHI wa Kata ya Muganza wilayani Ngara mkoani Kagera wanakesha nje ya nyumba zao huku wakipiga ngoma na kukoka moto kwa madai ya kuhofiwa kuvamiwa na
'popobawa'.

Popobawa ni dhana ya kufikirika ambayo imekuwa ikizushwa katika maeneo mbalimbali nchini kuwa hujitokeza na kufanya ngoni au kulawiti wananchi.

Lakini kwa wakazi hao, imani hiyo potofu imewaathiri na kwenda mbali huku wakidai kuwa popobawa ametumiwa na mchungaji wa kanisa moja aliyepiga kambi porini takribani miezi minne sasa, akidai anamsubiri Mungu ashuke.

Kama ilivyo maeneo mengi, dhana hiyo imekanushwa vikali na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Salum Nyakoji wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake.

Kanali Nyakoji alisema pamoja na taarifa hizo kuenea huku zikiwataka wananchi kupiga ngoma bila kukoma usiku wote kwa lengo la kuwafukuza mapopobawa, kamati yake ya ulinzi na usalama imefanya uchunguzi na kubaini kuwa ni suala la uzushi.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya amepiga marufuku wananchi kupiga ngoma nyakati za usiku kwa lengo hilo, na badala yake wapuuze uvumi huo na kulala kwa amani na utulivu.

"Huu ni uvumi, nawashauri wananchi kuachana nao, na kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendelo kwa amani na utulivu.

Kanali Mstaafu Nyakoji alisema taarifa potofu zilizozagaa katika maeneo mbalimbali kama Murusagamba, Rulenge na kwingineko, ni kwamba kuna popobawa wawili ambao ni dume na jike wanaozunguka katika nyumba za wananchi wa maeneo hayo nyakati za usiku, ambapo jike kufanya ngono na baba mwenye nyumba huku dume likifanya ngono na mama.

Kwa mujibu wa uvumi huo, popobawa hao wamedaiwa kutoka katika nchi jirani, lakini kwa mujibu wa mkuu wa wilaya na wananchi waliozungumza na Majira, hakuna mtu yeyote aliyethibitika kuingiliwa na popobawa hao.

Mkuu wa Wilaya alisema uvumi wa kuwapo  kwa popobawa hao, ulienezwa kwa malengo mabaya, ambayo hakufafanua.

Wakati DC Nyakoji akisema hayo, wakazi wa Kitongoji cha Nyakafandi, Kijiji cha Mukubu, Kata ya Muganza  wilayani humo walionekana kuamini uvumi huo na hivyo kulazimika kukesha wakipiga ngoma kwa woga.

Bw. Lucas Joseph (31) aliiambia gazeti hili kuwa, wananchi hao wanaamini popobawa ametumwa na mchungaji Bi. Anamaria Mutangera (46), ambaye wananchi wengi wanapingana na imani yake, wakidai kuwa ni ya upotoshaji.

Bw. Joseph ambaye gazeti hili lilifika nyumbani kwake saa 6:00 mchana na kumkuta amelala, alidai kuwa analazimika kulala mchana kutokana na kukesha usiku kwa kuhofiwa popobawa.

Kwa upande wake, Bi. Matrilda Sylvester (24) mkazi wa kitongoji cha Nyakafandi alisema sababu inayofanya waamini kuwa popobawa wameletwa na mchungaji huyo ni kutokana na kile alichokuwa akiwaeleza kuwa wanaopinga anayohubiri watakuja kuona.

Lakini Mchungaji Mulengera alipozungumza na Majira katika pori la Nyakafandi, alikanusha kuwatumia wananchi popobawa, kwa kuwa yeye na waumini wake wapatao 20 waliopiga kambi porini, hawaiombei nchi wala wilaya mambo mabaya, bali yanayowapata wananchi hao yanatokana na matendo yao kwa kuwa hawataki kumpokea Yesu.

3 comments:

  1. Kazi kweli kweli! basi hao watu wakiambiwa waue albino ili popobawa asije watafanya hivyo haraka sana! Bado tuna safari ndefu sana kuondokana na primitiveness!

    ReplyDelete
  2. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 29, 2010 at 9:50 AM

    Pamoja na kupinga vikali imani za mtindo huu,Kamanda wa Polisi ameniachia maswali haya:Uchunguzi wa Polisi ulifanywaje? Zilitumika mbinu gani? Ripoti ya uchunguzi iliandikwaje? Ndugu zangu,kila aaminiye atapona.

    ReplyDelete
  3. Tuulizane maswali machache tu kabla ya kukubali au kukataa kweli kama popobawa wapo.
    1.Kwanza katika eneo wanaloishi wanamtegemea Mungu gani?
    2.Kweli huyo mungu wao ni kiziwi hasikii akielezwa shida za watu.
    3.Kuna hali au tabia gani iliyoruhusu eneo hilo likumbane na hali hiyo ngumu.
    Sasa natoa nafasi ya tofauti kati kuamini na kujua.Kujua jambo fulani ni lazima macho ,masikio, pua ,kuonja na kugusa kukusaidie kujua kwako au kujua kwangu.Kuamini ni jinsi mtu anavyolipokea jambo ambalo hajaliona na anatarajia matokeo yake.
    Popobawa huwezi kumwona kwa macho hata siku moja .Lakini ninakwambia akikutembelea ni lazima utatambua uwepo wake tu.Kuna Mungu Mkuu sana huyo hakika popobawa hakohoi kwake.Eneo husika liachane na hiyo miungu midogomidogo ambayo silolote katika mpambano huo.Wamwangalie Mungu Mkuu sana ambaye anaweza kuwasaidia, hizo ngoma hazitamwondoa huyo popobawa

    ReplyDelete