29 November 2010

Wasomi wameisaliti nchi-Askofu.

Na Charles Mwakipesile, Mbeya.

ASKOFU Kiongozi wa Kanisa la Moravian Tanzania  mhashamu Alinikisa Cheyo amesema kuwa kuwa chanzo cha ufisadi na uhujumu mkubwa nchini ni wasomi walioamua kuisaliti nchi baada ya
kusomeshwa kwa kodi za watanzania.

Akitoa salamu zake wakati wa mhafali ya tatu Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji kinachomilikiwa na kanisa   hilo jijini Mbeya, Askofu Cheyo aliwaasa wahitimu wa shahada na stashahada katika chuo hicho kutofuata mkumbo wa wasomi wengi ambao alidai wamewaibia Watanzania kwa kuwasaliti.

Alisema kuwa kama wasomi wangelisimama kwenye nafasi yao, ni wazi kuwa Tanzania ingefikia katika malengo yaliyowekwa ya kupata maisha bora  na kuondokana na umaskini mkubwa unaowakabili wananchi.

Askofu Cheyo alisema kuwa wasomi ndio wenye nafasi ya kuzuia mianya ya rushwa kwa kutoa elimu waliyojifunza sanjali na kupiga vita vitendo vya kifisadi, ambavyo alisema vimeifikisha nchi mahali pa kuweka matabaka  ya walio nacho na wasio nacho.

Aliwataka kuitumia elimu waliyoipata katika kuwatumikia Watanzania kwa lengo la kuwakomboa katika hali mbaya zinazowakabili, kwa kuibua mbinu mbalimbali mbadala za kutatua matatizo ili kufikia hatua ya kuwa nchi isiyo na vitendo viovu  vinavyosababisha unyonyaji wa haki za wanyonge.

“Wasomi wameshindwa kuwa sehemu ya ukombozi kwa Watanzania na hivyo kuonekana wazi kuwasaliti na wao kuongoza katika vitendo vya kifisadi, rushwa na hivyo wamewanyonya Watanzania kwa kuwa ndio waliowasomesha kwa kodi za wakitegemea kulipwa,” alisema.

Katika hotuba yake iliyovuta usikivu mkubwa wa wahitimu na wageni waalikwa wakiongozwa na mgeni rasmi, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Millie Mbonile, Askofu Cheyo alisema kuwa ifike wakati wasomi watambue kuwa wao wana sehemu kubwa katika kuijenga nchi kwa kutumia elimu.

Askofu Cheyo ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Limulu nchini Kenya,  aliwataka wahitmu hao kwenda kukitangaza chuo hicho kwa vitendo katika kila eneo watakaopangiwa kufanya kazi uraiani.

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Tuli Kazimoto, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho kimepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na maendeleo makubwa ya kasi ya udahili ambapo hadi sasa chuo kina wanafunzi zaidi ya 3,000 kutoka 200 waliokuwepo wakati kikianza.

2 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 29, 2010 at 9:43 AM

    Kauli ya Askofu huyu ina ukweli kiasi fulani.Kwanza nijuavyo mimi,msomi ni mtu yeyote aliyefika ngazi ya Chuo Kikuu katika elimu yake...fani yoyote ile.Hao tupo wengi tu....tumejaa tele.Ni kweli tumesoma kwa fedha za wananchi wenzetu.Kati yetu,tupo tulioisaliti nchi kama Askofu anavyodai.Tumeshindwa ima kwa makusudi au kwa bahati mbaya kuonyesha matarajio ya wananchi kutokana na elimu yetu.Tumekuwa mbwa wa chama tawala ambaye akimuona mfugaji wake atamrukia kwa furaha huku akitingisha mkia wake huku akisahau kuwa ni jana tu bosi wake huyo alimchapa bila kosa la msingi.Maumivu yetu tunayasahau mapema kwa matarajio ya kupewa lishe.Tupo tuliolazimishwa kuwa mafisadi.Tulikosa wenzetu wa kupinga nao pamoja...wasomi wenzetu wanaomrukia bosi.Si ni kweli kwamba ukishindwa kupambana nao unajiunga nao? Tupo wenye mioyo safi ya kizalendo.Tunajaribu kupenyesha harajkati zetu na maneno yetu ya kizalendo na kimatarajio kuwafikia nyinyi mliotusomesha.Nyinyi hamtusikilizi.Mnasema,hatuyajui vizuri maisha..hatuna 'experience'.Tunakatishwa mno tamaa.Tukionyesha uzalendo,nyinyi mnaungana na mabosi kutuambia kuwa sisi tunahatarisha amani na utulivu wa nchi.Kweli yetu inakuwa kisu kikali.Mnatunyang'anya.Tunabaki bila silaha.Akija adui bosi,tunashindwa kupambana naye na kuonyesha uzalendo wetu.Nyinyi tena mnatulaumu.Sisi tufanyeje? Tushike silaha gani tena? Mko tayari kujiunga nasi? Tuanze basi na hili la Katiba.Tuwaunge mkono wasomi wachache wa CHADEMA waliotuma ujumbe kwa bosi mkuu juu ya hili.Tukiwa pamoja,tutamjua vyema nani yu msaliti.

    ReplyDelete
  2. Askofy Cheyo na Bw Mselewa wote mmesema kweli tupu na ilitakiwa kunenwa toka zamani. Kwetu sisi raia wa kawaida tumeshindwa kumtegemea Mwenyezi Mungu ktk maisha yetu kwa kusema kweli tu na kutegemea nguvu za Mola wetu kutuongaza. Lakini baya zaidi ni la hao viongozi wa kiroho kushindwa kukataa hadharani michango ya fedha na zawadi nono toka kwa hao mafisadi kwa nia ya kujinunulia nafasi ya raia wema. Sasa kama kanisa limeshindwa kuonyesha dira ya kukemea maovu au mwenendo usiojenga jamii kama ilivyokusudiwa na Mwenyezi Mungu ni rahisi kwa waumini kuona mali dunia ni bora kuliko kumcha Mungu.

    ReplyDelete