29 November 2010

Warushiwa bomu la mkono kwa wivu.

* Wawili wafa, wengine wajeruhiwa

Na Theonestina Juma, Ngara.
 WATU wawili wameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya kurushiwa na bomu la kutupwa kwa mkono katika tukio linalodaiwa kuwa ni kutokana na wivu wa
mapenzi.

Tukio hilo lilitokea saa 3.30 usiku katika Kijiji cha Kumwendo, Kata ya Mbuba, Tarafa ya Rulenge wilayani Ngara, Novemba 26, mwaka huu.

Waliouawa ni Bw. Philimon Ngaingera (67) na William Willias (35) wote wakazi wa kijiji hicho, na Walijeruhiwa ni Bi. Anna William (25) mke wa
marehemu Willias aliyejeruhiwa sehemu ya paja ya kulia na Bw. Stephen Philemon (25) ambaye ni mtoto wa marehemu Bw. Philimon aliyevunjika mkono wa kushoto na uti wa mgongo karibu na shingo.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu William, Bw. Mwafrika Willias, siku ya tukio watu hao walikuwa wakiwa nyumbani kwa Bw. Willias wakinywa pombe ya kienyeji aina ya rubisi, ghafla walishtukia watu wasiowafahamu wakifungua mlango bila kubisha hodi na kuwarushia mabomu.

Alisema inasemekana kuwa marehemu Philimon alikuwa na visa na mtu mmoja ambaye miaka miwili walikuwa wakigombania mwanamke.

Alisema kutokana na ugomvi kuwepo kati yao, mtuhumiwa alimjeruhi Bw. Philemon na kukamatwa na polisi na kukaa rumande takribani miezi minane na kuachiwa 
Februari mwaka huu, ambapo aliporudi tena uraiani  aliendeleza ugomvi huo.

Alisema kutokana na hali hiyo, ilifikia hatua hadi wakasuluhishwa na wazee wa kijiji hicho chini ya mwenyekiti wa kijiji, Bw. Paulo Rutashobya na mtuhumiwa alipigwa faini ya sh. 280,000 kwa ajili ya kulipa gharama ya matibabu ya Bw. Philimon, jambo ambalo halitekeleza huku visa vikiwa vinazidi hadi hiyo juzi alipodaiwa kurusha bomu hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Bw. Henry Salewi ingawa alisema hakauwa ofisini,  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema katika tukio hilo, mtu mmoja anashikiliwa na polisi wilayani lakini hakuweza kumtaja, ingawa habari zaidi zinaeleza kuwa ni Bw. Oswald Buchumu na uchunguzi unaendelea na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Wakati huo huo, habari zaidi kutoka katika Kijiji na Kata ya Mugoma wilayani hapa zinaeleza kuwa watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupatikana na mabomu tisa ya kutupwa kwa mkono na risasi 80, wakiyatafutia soko.

Watu hao wanadaiwa kuwa ni rai wa Burundi, lakini Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Bw. Salewi alidai kuwa hajapata taarifa hiyo.

1 comment:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 29, 2010 at 9:55 AM

    Hii kali.Hapa uchunguzi wa kina wahitajika.Yawezekana kuwa ni jaribio la ujambazi badala ya suala hilo la mapenzi.

    ReplyDelete