05 November 2010

Vodacom yatangaza zawadi mbio za baiskeli.

Na Amina Athumani



KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacoma jana imetangaza zawadi za washindi wa mbio za baiskeli za Vodacom Mwanza Cycle Challange ambapo
mshindi wa kwanza ataondoka na sh. milioni 1.5.

Akitangaza zawadi hizo Dar es Salaam jana, Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Rukia Mtingwa alisema mashindano hayo yatafanyika Novemba 12 na 13 mwaka huu jijini Mwanza.

Rukia alisema mshindi wa pili katika mbio hizo ataondoka na sh. milioni moja, wa tatu sh. 700,000, wa nne hadi wa 10 sh. 500,000 kila mmoja, washiriki wa 11 hadi wa 20 watapata sh. 250,000 kila mmoja na wa 21 hadi 30 wakijinyakulia sh. 90,000 kila mmoja.

Alisema katika mbio za kilometa 80, ambazo watakimbia  wanawake mshindi wa kwanza atapewa sh. milioni 1.1, wa pili sh. 800,000, wa tatu sh. 600,000, wakati wa nne hadi wa 10 kila mmoja atapew sh. 350,000. Washiriki kuanzia wa 11 hadi ya 20 katika mbio hizo watapewa sh. 130,000 kila mmoja na wa 21 hadi wa 30 wataondoka na sh. 70,000 kila mmoja.

Rukia alisema mbali na zawadi hizo pia kwa mbio za kilometa 10, ambazo zitawahusu watu wenye ulemavu washindi wawili wa kwanza watapewa sh. 400,000 kila mmoja na wengine wawili watakaoshika nafasi ya pili watakabidhiwa sh. 250,000, nafais ya tatu nao wakikabidhiwa sh.150,000 kila mmoja na wanne hadi 10 wataondoka na sh. 70,000 kila mmoja.

“Mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na tunawaomba waendesha baiskeli kujitokeza kwa wingi, kwani tumeboresha zawadi, ubora na viwango,” alisema Rukia.

Alisema huu ni mwaka wa tano kwa Vodacom  kudhamini mashindano hayo wakiwa kama wadhamini wakuu huku Kampuni za Alphatel, Knight Support na SBC nazo pia zimejitosa kutoa udhamini.

No comments:

Post a Comment